Jumatatu tarehe 27 Aprili mwaka 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 3 Ramadhani mwaka 1441 Hijria sawa na Aprili 27 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1028 iliyopita inayosadifiana na tarehe 3 Ramadhani 413 Hijria, alifariki dunia Muhammad bin Nu'uman maarufu kwa lakabu ya Sheikh Mufiid, faqihi, mtaalamu wa elimu ya hadithi, Qur'ani Tukufu na historia ya Kiislamu. Sheikh Mufid alikuwa hodari na mwanafikra aliyepevuka na aliweza kujibu masuala ya kifiqihi kwenye midahalo kulingana na madhehebu yoyote aliyotakiwa kufanya hivyo. Kutokana na uhodari wake huo, maulamaa wengi wa Kiislamu katika zama hizo walimpa lakabu ya Mufiid. Sheikh Mufiid ameandika vitabu vingi miongoni mwa hivyo, ni al Kalaam Fii Dalaailil Quran', al Arkaan' na 'Kashful Saraair'.

Tarehe kama ya leo miaka 499 iliyopita, Ferdinand Magellan, baharia wa Kireno aliuawa na wenyeji wa Ufilipino kutokana na kuingilia mambo yao. Alizaliwa mwaka 1470 na kuanzia mwaka 1519 Miladia baharia huyo alianza safari yake kubwa ya baharini akiwa na meli tano. Ferdinand Magellan aligundua lango bahari huko kusini mwa bara la Amerika baada ya kuwasili katika pwani ya Amerika ya Latini. Lango bahari hilo limepewa jina la baharia huyo wa Kireno yaani Lango Bahari la Magellan.

Miaka 60 iliyopita katika siku inayofanana na hii ya leo, nchi ya Togo ilipata uhuru. Wareno walikuwa watu wa kwanza kuikoloni Togo na nchi hiyo ilijulikana sana kwa jina la "Pwani ya Watumwa" kwa kuwa nchi za Ulaya zilikuwa zikiitumia nchi hiyo kama kituo cha kusafirishia watumwa kuelekea Ulaya. Togo inapakana na nchi za Ghana na Benin na mji mkuu wake ni Lome.

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Sierra Leone moja ya makoloni makongwe ya Uingereza magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru. Sierra Leone ilianza kukoloniwa na Ureno tangu karne ya 15 na nchi hiyo ilikuwa mojawapo ya vituo muhimu vya kuuzia watumwa waliokuwa wakipelekwa Ulaya. Uingereza ilianza kuikoloni Sierra Leone mwishoni mwa karne ya 18 hadi mwaka 1961 wakati nchi hiyo ilipopata uhuru. Baada ya uhuru, nchi hiyo ilikumbwa na mapinduzi na uasi mwingi. Kijiografia Sierra Leone iko magharibi mwa Afrika ikiwa na ukubwa wa kilomita mraba 71,000 na inapakana na Guinea na Liberia.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita alifariki dunia Kwame Nkrumah, mwanasiasa mashuhuri wa Kiafrika ya mwasisi wa uhuru wa Ghana. Mkrumah alizaliwa mwaka 1909 na baada ya kupata shahada ya uzamivu nchini Marekani alianza kujishughulisha na masuala ya kisiasa. Baadaye Kwame Nkrumah aliasisi chama cha Kitaifa cha Watu wa Ghana na kuanza mapambano dhidi ya wakoloni wa Kiingereza. Mwaka 1951 alishiriki katika uchaguzi wa Bunge na kuwa Waziri Mkuu. Baada ya Ghana kupata uhuru mwaka 1960 Kwame Nkrumah alikuwa Rais wa nchi hiyo lakini Februari 24 mwaka 1966 aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi na wafuasi wa nchi za Magharibi akiwa safari nchini Uchina. Baadaye alielekea Guinea ambako aliishi hadi kufariki dunia. Kwame Nkrumah anatambuliwa kuwa miongoni mwa wanamapambano mashuhuri wa Afrika waliofanya jitihada kubwa katika kupata uhuru na kujitawala nchi za bara hilo.

Tarehe 8 Ordibehesht miaka 32 iliyopita watawala wa kizazi cha Aal Saud walikata uhusiano wa Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya utawala wa Saudia kufanya mauaji ya umati ya mahujaji wa Irani wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu mjini Makka katika siku iliyopewa jina la Ijumaa ya Damu hapo tarehe 9 Mordad 1366 Hijria Shamsia, uhusiano wa Iran na nchi hiyo ulifika kiwango cha chini zaidi na wanadiplomasia wa Iran nchini Saudia wakapunguzwa kwa kiasi kikubwa. Wanadiplomasia wa Saudia mjini Tehran walikuwa tayari wamekwishaondoka. Hatimaye uhusiano wa nchi hizi mbili ulikatwa kikamilifu tarehe 28 Aprili 1986. Safari za Wairani waliokuwa na hamu ya kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Makka na Harama tukufu ya Mtume Muhammad (saw) mjini Madina pia zilisimamishwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Uhusiano wa nchi hizo mbili ulikatwa katika kipindi ambacho Saudi Arabia ilikuwa msaidizi mkubwa wa kifedha wa utawala wa Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Iran na hatua hiyo ilichukuliwa sambamba na siasa za Marekani za kubana na kuzidisha mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
