Jul 10, 2020 02:26 UTC
  • Ijumaa tarehe 10 Julai 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 18 Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Junai 10 mwaka 2020.

Miaka 279 iliyopita ardhi ya Alaska iligunduliwa na mvumbuzi wa Kidenmark kwa jina la Vitus Bering. Mvumbuzi huyo aligundua ardhi ya Alaska inayopatikana kaskazini magharibi mwa Canada akiwa katika safari yake kuelekea Urusi. Hadi kufikia mwaka 1867 eneo tajiri kwa mafuta la Alaska lilikuwa sehemu ya mamlaka ya Urusi ya Kitezari. Hata hivyo mwaka huo Urusi iliiuzia Marekani ardhi ya Alaska kwa kiasi cha dola milioni saba, eneo ambalo leo hii linahesabiwa kuwa jimbo la 49 la Marekani.

Vitus Bering

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita inayosadifiana na 10 Julai 1940 Jemedari Henri Petain Waziri Mkuu wa muda na afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Ufaransa, alichukua uongozi baada ya Ufaransa kushindwa na Wanazi wa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa mkataba wa kivita uliosainiwa na nchi mbili hizo tarehe 22 Juni 1940, eneo la kaskazini mwa Ufaransa, ukiwemo mji wa Paris lilibaki chini ya himaya ya jeshi la Manazi wa Ujerumani.

Henri Petain

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, alifariki dunia msomi mashuhuri wa Kiislamu Muhammad Hussein Kashiful Ghitaa. Ayatullah Kashiful Ghitaa alizaliwa katika mji mtakatifu wa Najaf katika familia ya wasomi na wacha-Mungu na kuanza kutafuta elimu akiwa bado mtoto mdogo. Baada ya kukamilisha elimu ya msingi, Ayatullah Kashiful Ghitaa alihudhuria darsa za maulamaa wakubwa wa zama hizo na kukwea daraja za juu za elimu katika kipindi kifupi. Alifanikiwa kulea wasomi na maulamaa wakubwa na kufanya safari katika nchi nyingi za Kiislamu kwa ajili ya kueneza elimu na maarifa. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu pia alikutambua kushiriki katika masuala ya kisiasa na kutilia maanani masuala ya serikali na utawala kuwa ni katika mambo ya wajibu na alikuwa na mchango mkubwa katika kuanzisha Harakati ya Kitaifa ya Iraq. Ayatullah Kashiful Ghitaa alishiriki vilivyo katika mapigano ya jihadi ya wananchi wa Iraq wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia dhidi ya jeshi vamizi la Uingereza. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali.

Ayatullah Kashiful Ghitaa

Na miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Bahamas huko Amerika ya Kati vilipata uhuru kutoka Uingereza na siku kama ya leo hufahamika visiwani humo kama siku ya taifa. Visiwa vya Bahamas viligunduliwa mwaka 1492 na mvumbuzi wa Ulaya Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania. Visiwa vya Bahamas vilipata uhuru mwaka 1973 na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Visiwa vya Bahamas viko kaskazini mwa Cuba na kusini mashariki mwa Marekani. 

Bendera ya Bahamas