Jumapili tarehe 13 Septemba 2020
Leo ni Jumapili tarehe 24 Mfunguo Nne Muharram 1442 Hijria sawa na tarehe 13 Septemba 2020.
Siku kama ya leo miaka 1393 iliyopita, vilimalizika vita vya miaka 24 baina ya utawa wa Iran na Roma. Khosrow Parvēz, mfalme wa Kisasani baada ya mashambulizi mtawalia, aliweza kudhibiti maeneo ya Mesopotamia, Syria, Palestina, Misri na Asia Ndogo na kupanua mamlaka yake hadi Istanbul ya leo. Mwaka 591 Miladia, kulifikiwa mapatano baina ya pande hizo mbili baada ya kutiwa saini makubaliano baina ya mfalme Khosrow Parvēz na mfalme wa Roma. Hata hivyo tarehe 5 Juni mwaka 603 Miladia, kuliibuka tena vita vilivyodumu kwa muda wa miaka 24 baina ya nchi hizo mbili. Katika vita hivyo, jeshi la Iran lilipata ushindi mtawalia katika ardhi ya Roma kiasi cha kudhibiti karibu eneo zima la Roma ya Mashariki. Baadaye jeshi la mfalme Khosrow lilidhoofika na mfalme huyo akakimbilia eneo la Ctesiphon, moja ya tawala za Wasasani. Aidha kutokana na Mfalme Khosrow Parvēz kuchana barua ya Mtume Muhammad (saw) na kulaaniwa na mtukufu huyo, utawala wa mfalame huyo ulidhoofika na hatimaye kushindwa na Waroma. Baadaye raia wa Iran, kwa kushirikiana na jeshi la taifa, walimuondoa madarakani mfalme huyo na kumtia jela kabla ya kuuawa kwake.

Siku kama ya leo miaka 770 iliyopita, vilianza vita vya Mansuriya katika silsila ya Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu. Vita hivyo vya kihistoria vilianzishwa katika eneo lililojulikana kwa jina hilo huko Misri na mfalme Saint Louis wa Ufaransa ambaye alikuwa na lengo la kuidhibiti Misri. Katika vita vya Mansuriya Jeshi la Msalaba lilipigwa vibaya na wapiganaji wa Kiislamu wa Misri waliokuwa wakiongozwa na Sallahuddin Ayyubi. Hatimaye Saint Louis alikamatwa mateka na Waislamu na kufungwa jela katika ikulu ya Loken ambayo hii leo inatumika kama jumba la makumbusho.
Siku kama ya leo miaka 240 iliyopita, lifti au elevator kwa Kingereza ilivumbuliwa. Mvumbuzi wa lifti hiyo ya kwanza alikuwa raia wa Marekani kwa jina la John Bikbart. Lifti hiyo ilifanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza katika mji wa Chicago nchini Marekani. Katika majaribio hayo, watu kadhaa waliingia ndani ya lifti hiyo na kwenda juu na chini. Lifti ya kwanza ya umeme ilitengenezwa mwaka 1889, huku ile ya otomatiki ikitengenezwa mnamo mwaka 1915.
Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Septemba 1885, alizaliwa Aquilino Ribeiro mwandishi na mwanamapinduzi wa Ureno. Baada ya kumaliza masomo yake, Ribeiro alitumbukia kwenye uwanja wa kisiasa na kufungwa jela kwa miaka kadhaa. Mnamo mwaka 1961, Aquilino Ribeiro alifanikiwa kupokea tuzo ya Nobel katika fani ya fasihi, na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1963 akafariki dunia.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita yani tarehe 23 Shahrivar mwaka 1357 Hijria Shamsia kulifanyika maandamano makubwa hapa nchini kuwaenzi mashahidi waliokuwa wameuawa na vibaraka wa Shah siku kadhaa kabla yake. Siku hiyo umati mkubwa wa watu ulimiminika katika makaburi ya Behest Zahraa mjini Tehran kuwaenzi mashahidi hao. Askari wa utawala wa Shah walikuwa na nia ya kuzuia maandamano hayo lakini umati mkubwa wa wananchi walioshiriki maandamano ulidumisha malalamiko yao dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah huko wakipiga nara za: “Iran ni nchi yetu na Khomeini na kiongozi wetu.”
Siku kama hii ya leo miaka 27 iliyopita, mwafaka na tarehe 13 Septemba 1993 Yasir Arafat, kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na Yitzhak Rabin waziri mkuu wa wakati huo wa utawala haramu wa Israel walisaini mkataba wa mapatano kwa jina la "Makubaliano ya Ghaza-Jericho" huko Washington, Marekani. Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na utawala wa Kizayuni zilitambuana rasmi katika makubaliano hayo yaliyosainiwa miaka miwili baada ya kuanza mazungumzo eti ya amani kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni.