Sep 28, 2020 03:02 UTC
  • Jumatatu tarehe 28 Septemba 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 10 Mfunguo Tano Safar 1442 Hijria sawa na 28 Septemba 2020.

Siku kama ya leo miaka 1113 iliyopita, alifariki dunia msomi mashuhuri wa Iran, Abul-Fadhl Bal'ami. Bal'ami alikuwa mtu wa Bukhara, moja ya miji maarufu ya nchi ya Uzbekistan ya leo. Alijulikana kwa jina la Bal'ami kutokana na mmoja wa mababu zake kuishi mji wa Bal'am huko Asia ya Kati. Abul-Fadhl Bal'ami alikuwa waziri mwenye hekima na msomi mkubwa enzi za utawala wa Wasamani na aliandika vitabu mbalimbali. Kitabu cha tarjama ya ‘Taarikh Twabari’ ni moja ya vitabu vinavyonasibishwa na msomi huyo na kilichopata umashuhuri katika karne ya nne Hijiria. Kitabu kingine maarufu cha msomi huyo ni ‘Taarikh Balaam’ ambapo ameashiria masuala mbalimbali ya historia.

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, alifariki dunia rais wa zamani wa Misri, Gamal Abdel Nasser. Abdel Nasser alizaliwa mwaka 1916. Alishiriki katika vita vya kwanza vya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel hapo mwaka 1948 na kufanya mapinduzi ya kijeshi kwa kushirikiana na Jenerali Najib, dhidi ya Mfalme Faruq 1952 na kuung'oa utawala wa kisultani nchini humo. Miaka miwili baadaye Gamal Abdel Nasser alimuondoa madarakani mshirika wake Jenerali Najib na kuchukua jukumu la kuiongoza Misri sambamba na kufanya juhudi za marekebisho, kupambana na ukoloni na utawala ghasibu wa Israel. Mwaka 1956 aliutaifisha mfereji wa Suez na kuufanya kuwa mali ya taifa la Misri, hatua iliyozifanya nchi za Ufaransa, Uingereza na utawala wa Kizayuni kuishambulia nchi hiyo.

Gamal Abdel Nasser

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, mwafaka na tarehe 7 Mehr 1360 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Hujjatul Islam Sayyid Abdul Karim Hasheminejad mwanachuoni na mwanamapambano shupavu wa Iran katika mji wa Mash'had. Sayyid Hasheminejad aliuawa shahidi baada ya kupigwa risasi na mmoja wa wanachama wa kundi la kigaidi la Munafikiin (MKO). Mwanachuoni huyo alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi nchini Iran dhidi ya utawala wa Shah na aliwahi kuteswa na kuwekwa gerezani mara kadhaa.

Sayyid Abdul Karim Hasheminejad

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, makamanda 5 wa ngazi za juu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliaga dunia katika ajali ya ndege. Viongozi hao walikuwa wakirejea kutoka katika oparesheni za kuukomboa mji wa Abadan ulioko kusini magharibi mwa Iran. Mji huo wa Abadan ulikuwa umezingirwa na jeshi vamizi la dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein. Makanda hao ni Shahidi Fallahi, Shahidi Fakuri, Shahidi Namjuu, Shahidi Kolahduz na Shahidi Jahan Ara aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu mjini Khoram Shahr. Katika ujumbe wa kusifu na kushukuru mchango wa mashahidi hao baada ya tukio hilo Imam Khomein MA aliwataja kuwa mashahidi wa Uislamu.

makamanda wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio likiutaka utawala wa Kizayuni kukomesha operesheni ya kuchimba mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Rasimu ya azimio hilo ililaani uchimbaji huo wa mashimo kinyume cha sheria chini ya eneo hilo takatifu. Hata hivyo upinzani wa Marekani ulipelekea kuondolewa kipengee hicho katika azimio hilo.

Uchimbaji huo wa mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa unaofanywa na Israel ulizusha machafuko ya umwagaji damu mkubwa hapo tarehe 23 Septemba 1996 kati ya askari wa utawala huo ghasibu na Wapalestina ambapo askari hao waliua na kujeruhi mamia ya Wapalestina.

Na siku kama ya leo miaka 20 iliyopita Intifadha ya wananchi wa Palestina kwa mara nyingine tena ilipamba moto. Hatua ya Ariel Sharon kiongozi wa chama chenye misimamo mikali cha Likud na mhusika mkuu wa mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika kambi za Sabra na Shatila ya kuingia katika Msikiti wa al Aqswa na kuuvunjia heshima msikiti huo mtukufu, iliwatia hasira Wapalestina na kuwafanya waanzishe maandamano na mapambano makubwa dhidi ya utawala huo wa Israel.