May 04, 2016 10:40 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (122)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni wakati mwingine wa kujiunga nanyi wasikilizaji wapenzi ili tupate kusikiliza kwa pamoja sehemu nyingine ya mfululizo wa vipindi hivi ambavyo kama mnavyojua hujadili na kujibu maswali mbalimbali yanayohusiana na itikadi ya Kiislamu.

Mnakumbuka kuwa katika vipindi kadhaa vilivyopita tumekuwa tukijibu maswali yanayohusiana na sifa ambazo Imam maasumu anapasa kuwa nazo ili afae kuongoza umma wa Kiislamu. Swali la wiki hii linasema kuwa sheria ya Mtume Muhammad (saw) ndiyo sheria ya mwisho inayomwongoza mwanadamu, na Mtume Mtukufu (saw) aliwabainishia vyema walimwengu sheria hiyo, nayo Qur’ani Tukufu imehifadhiwa na kulindwa vyema na Mwenyezi Mungu mwenyewe ili isije ikapatwa na kasoro zozote. Kwa kutilia maanani hilo, je, kuna haja gani ya kuwepo Imam maasumu katika kila zama kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu, baada ya kuaga dunia Mtume?

Jibu la swali hili limejibiwa katika maandiko mengi matakatifu yakibainisha sababu tofauti za kuwepo haja hii ambapo katika kipindi hiki tutaashiria moja ya sababu hizo kwa msingi wa mafundisho ya Qur’ani Tukufu. Hivyo basi endeleeni kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

**********

Kwanza kabisa wapenzi wasikilizaji tunaashiria aya ya 59 ya Surat an-Nisaa ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hilo ndilo bora zaidi na mwisho mzuri.

Kabla ya kuzungumzia kwa urefu kidogo aya hii na maana yake, hebu tugusie aya nyingine ya 83 ya Sura hiyohiyo ambayo inaikamilisha aya iliyotangulia kwa kusema: Na linapowafikia jambo lolote linalohusu amani au la kitisho wao hulitangaza. Na lau wangelipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wangejua wale wanaochunguza katika wao. Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema Yake mngemfuata shetani ila wachache wenu tu.

Maulama na wanazuoni wengi wamefanya utafiti mwingi na wa kina katika kuthibitisha kwamba aya hii inathibitisha udharura wa kuwepo Imam maasumu katika kila zama kutoka miongoni mwa wenye madaraka ili kutiiwa kwake kuwe sawa na kutiiwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Sisi hapa hatutazichambua aya mbili hizi kwa mtazamo huu, bali kwa mtazamo mwingine ambao unafafanua umuhimu na rehema kubwa aliyowajaalia Mwenyezi Mungu waja wake ambapo bila shaka ufafanuzi wa mtazamo huo utajibu swali la kipindi cha juma hili. Endeleeni kuwa nasi.

**********

Ndugu wasikilizaji, upande tunaouchambua katika aya hizi tukufu ni ule ambao umetajwa kuwa ni rehema kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kutokana na ukweli kwamba amewajaalia walii na kiongozi maasumu ambaye amefanywa kuwa marejeo yao wakati hitilafu zinapoibuka miongoni mwao. Walii huyu aliye na uwezo mkubwa wa kufahamu hukumu za mwenyezi Mungu kutoka kwenye sheria zake ndiye anayepasa kuwa hakimu na msuluhishi wa tofauti na hitilafu ibuka na hivyo kauli yake kuwa ya mwisho katika utatuzi wa migogoro na ufafanuzi wa mambo. Kauli hiyo ndiyo inayotajwa mwishoni mwa aya ya kwanza kama ‘jambo bora zaidi na mwisho mzuri.’ Kama ambavyo kuheshimu na kutii kauli ya marejeo hayo ndiyo njia ya wokovu na kuepuka kumfuata shetani ambaye hufanya kila analoweza ili kueneza chuki, ugomvi na mivutano miongoni mwa watu. Na hili ndilo jambo linalobainishwa wazi katika aya ya pili yaani aya ya 83 ya Surat an-Nisaa ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema Yake mngemfuata shetani ila wachache wenu tu.

Na msighafilike na ukweli huu, wapenzi wasikilizaji kwamba, juhudi za shetani za kuzua na kuenza fitina, ugomvi, chuki na mifarakano miongoni mwa wanadamu zingali zinaendelea hadi Siku ya Kiama, kama ambavyo ugomvi, mivutano na hitilafu baina ya wanadamu ni jambo la kawaida. Kwa msingi huo merejeo ya kuaminika yanapasa kuwepo daima kwa lengo la kutatua tofauti na mivutano hiyo inayotokea katika jamii ya Waislamu na hivyo kuwaepusha hatari ya kumfuata shetani. Hivyo basi marejeo hayo ni yapi?

Tunazirejea tena aya mbili hizi tukufu ambapo tunapata kwamba ya kwanza inasema wazi bali inawaamrisha Waislamu kumrejea Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) katika jambo ambalo wanatofautiana na kuhitilafiana kwalo. Mwenyezi Mungu anasema: Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hilo ndilo bora zaidi na mwisho mzuri.

Ni wazi kwamba kumrejea Mwenyezi Mungu Mtukufu hutimia kwa kukirejea Kitabu chake Kitakatifu na Mtume wake (saw), jambo ambalo huwezekana kirahisi katika maisha na uhai wa Mtukufu huyo (saw). Hali inakuwaje anapoaga na kuondoka humu duniani? Hili ndilo swali linalojibiwa na aya ya pili ambayo ni ya 83 ya Surat an-Nisaa ambapo inaongeza maneno ‘wenye mamlaka’ kwa Mtume Mtukufu (saw) na kuwataka Waislamu kuwarejea wanapozozana na kugombana katika maisha yao ya kawaida katika zama za kuwepo amani au vita na hofu. Kwa msingi huo kuwarejea wenye mamlaka inakuwa ni sawa na kumrejea Mwenyezi Mungu na Mtume wake Mtukufu (saw), yaani kuirejea Qur’ani Tukufu. Hawa ni watukufu ambao wana uwezo mkubwa wa kufafanua na kuelewa vyema hukumu za Mwenyezi kutoka kwenye kitabu hicho na wala hawawezi kufanya makosa katika kufahamu hukumu hizo kutokana na kinga na umaasumu waliopewa na Mwenyezi Mungu mwenyewe.

Ni wazi kuwa kuwarejea watukufu hawa walio na mamlaka ni sawa na kuzirejea sunna safi za Mtukufu Mtume (saw) ambazo zimehifadhiwa kwao kwa njia bora zaidi na hivyo kutokumbwa na hatari ya kupotoshwa kimatamko au kimaana. Kwa hivyo kuwarejea wenye mamlaka hawa huwa ni sawa na kurejea marejeo halisi ya Mwenyezi Mungu ambako kunamdhaminia mwanadamu wongofu na kumuepusha kumfuata shetani na mbinu zake zote.

*********

Kwa hivyo tunafupisha somo tulilojifunza katika kipindi cha juma hili kwa kusema kwamba rehema kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake ilimfanya awachagulie marejeo na watu ambao wangewaepusha kumfuata shetani wakati wa kuzuka hitilafu na migangano miongoni mwao, kwa sababu watukufu hao huwabainishia hukumu za Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw) pamoja na njia sahihi ya kufuatwa wakati wa kutokea hitilafu kama hizo maishani. Na hii ndiyo sababu muhimu zaidi ya kuhitajia kuwepo Imam maasumu asiyetenda dhambi katika kila zama. Jambo hili linabainishwa na kusisitizwa wazi na aya za 59 na 83 za Surat an-Nisaa. Kuna hadithi nyingi mno ambazo zimeashiria maana hii muhimu ya udharura wa kuwepo Imam maasumu miongoni mwa Waislamu ili awaongoze kwenye njia safi na iliyonyooka kuelekea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Tutakujulisheni na kuashiria baadhi ya hadithi hizo katika kipindi kinachokuja cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain, Inshallah. Basi hadi wakati huo panapo majaaliwa, hatuna la ziada kutoka hapa mjini Tehran isipokuwa kukutakieni kila la heri na usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vilivyosalia. Wassalaam Aleikum Warhmatullahi Wabarakatuh.