Oct 15, 2020 03:49 UTC
  • Alkhamisi tarehe 15 Oktoba 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Safar 1442 Hijia saa na Okoba 15 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 478 iliyopita alizaliwa Abolfat'h Jalal al-Din Muhammad Akbar, mfalme aliyekuwa na nguvu kubwa wa silsila ya Teimurian nchini India. Mfalme huyo alikuwa maarufu kwa jina la Akbar Shah na alichukua madaraka akiwa na umri wa miaka 13 baada ya kufariki dunia baba yake, Homayun. Kwa kipindi cha miaka mitano aliongoza nchi akiwa na cheo cha naibu mtawala chini ya usimamizi wa Bairam Khan. Baada ya kushika madaraka kikamilifu alianza kupanua wigo wa utawala wake katika maeneo ya Bengal, Kashmir, Sindh, Punjab, Ahmednagar na Kandahar. Mfalme Abolfat'h Jalal al-Din Muhammad Akbar alikomboa kisiwa cha Dakan huko kusini mwa India kutoka mikononi mwa Wareno. Akbar Shah alifariki dunia mwaka 1605.

Abolfat'h Jalal al-Din Muhammad Akbar

Siku kama ya leo miaka 176 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Wilhelm Nietzsche. Baada ya kuhitimu masomo, Nietzsche alianza kufunza katika Chuo Kikuu cha Basel. Mwanafalsafa huyo alikuwa akipinga dini na misingi ya kimaadili na katika falsafa na mitazamo yake alikuwa akiamini nadharia ya "Superman", kwa maana ya mtu mwenye uwezo kupita kiasi. Nietzsche alikuwa akiamini kwamba, mtu mwenye uwezo kupita kiasi au Superman ni matokeo ya irada na matashi ya mwanadamu na huwa juu ya mema na mabaya yote. Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na Beyond Good and Evil, The Birth of Tragedy na Thus Spoke Zarathustra. Katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wake Friedrich Wilhelm Nietzsche alipoteza mlingano wa kifikra na alifariki dunia mwaka 1900.

Friedrich Wilhelm Nietzsche

Katika siku kama ya leo miaka 126 iliyopita yaani tarehe 15 Oktoba mwaka 1894, ilianza kesi ya Alfred Dreyfus mjini Paris Ufaransa. Dreyfus alikuwa afisa wa jeshi la Ufaransa mwenye asili ya Kiyahudi ambaye kesi yake ni miongoni mwa matukio yaliyozusha makelele mengi katika karne ya 19 nchini humo. Afisa huyo wa jeshi alituhumiwa kuisaliti nchi yake na kutoa siri za jeshi la Ufaransa kwa Ujerumani. Alivuliwa cheo chake na akahukumiwa kifungo cha maisha jela. Baada ya kuhukumiwa kifungo hicho, ilithibitika kwamba Alfred Dreyfus hakuwa na hatia yoyote. Kwa utaratibu huo aliachiwa huru na kurejeshewa heshima na vyeo vyake. Hukumu ya kifungo cha maisha jela ya Dreyfus na kisha kutambuliwa kwake kuwa hakuwa na hatia, kadhia ambayo inatambuliwa kwa jina la Dreyfus Affair, ilitumiwa na Wazayuni katika propaganda za urongo kudai kwamba Wayahudi wamedhulumiwa barani Ulaya. Wazayuni walitumia vibaya kadhia hiyo kujiimarisha zaidi.

Katika siku kama ya leo tarehe 24 Mehr miaka 42 iliyopita, kulitokea maafa makubwa kwenye Msikiti Mkuu wa Kerman, huko magharibi mwa Iran baada ya vikosi vya polisi na askari usalama wa utawala wa mfalme Muhammad Reza Pahlavi kuwashambulia kwa risasi wananchi waliokusanyika kwenye eneo hilo la msikitini kwa shabaha ya kuadhimisha 40 ya mashahidi waliouawa tarehe 17 Shahrivar mjini Tehran. Shambulio hilo la vikosi vya usalama vya Shah liliamsha hasira na wimbi jipya la harakati za wananchi za kupinga utawala kibaraka wa Mfalme Muhammad Reza Pahlavi.

Mapigano ya wananchi na askari wa utawala wa Kipahlavi

Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari mwanachuoni mashuhuri wa Iran. Ayatullah Sabzawari alizaliwa mwaka 1290 Hijiria Shamsia, sawa na mwaka 1911 Miladia, katika mji huo uliopo kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanachuoni huyo licha ya kujipatia elimu ya msingi katika mji wa Sabzawar na kisha kusoma elimu ya dini mjini Mash’had, alielekea Najaf nchin Iraq na kujipatia elimu ya juu ya maarifa ya Kiislamu. Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari ameandika vitabu vingi na maarufu zaidi ni tafsiri ya Qur'ani ya ‘Mawaahibul-Rahman fii Tafsirul-Qur’an’ chenye juzuu 20, ‘Muhadh-Dhibul-Ahkaam fii Bayaanil-Halali wal-Haraam’ chenye juzuu 30 na ‘Tahdhibul-Usuulu’ chenye juzuu mbili.

Na leo tarehe 15 Oktoba ni Siku ya Vipofu Duniani. Suala la usalama wa vipofu na haki zao za kijamii daima lilikuwa likipewa umuhimu maalumu katika jumuiya za kimataifa na kwa msingi huo mwaka 1950 Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na Baraza la Kimataifa la Vipofu zilikutana na kupasisha sheria ya Fimbo Nyeupe na kuitangaza tarehe 15 Oktoba kuwa ni Siku ya Fimbo Nyeupe au Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Vipovu. Miongoni mwa vipengee vya sheria hiyo ni pamoja na haki ya vipofu kutumia suhula zote za hali bora ya kimaisha katika jamii, kuwahamasisha watu wa jamii hiyo kushiriki katika masuala ya serikali na kupewa ajira serikalini, kulinda haki za vipofu wakati wa kuvuka barabara na kadhalika.

Siku ya Vipofu Duniani.