Oct 25, 2020 05:36 UTC
  • Jumapili, 25 Oktoba, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 8 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 25 Oktoba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1182 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria,  inayosadifiana na tarehe 8 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 260 Hijria, aliuawa shahidi Imam Hassan al Askari (AS) mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu SAW katika mji wa Samarra nchini Iraq. Imam Askari AS alizaliwa mwaka 232 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Hadi (AS). Kipindi cha Uimamu wake kilikuwa kigumu na nyeti sana kutokana na kuzaliwa Imam wa Zama Mahdi (AS) wakati huo. Alichukua hatua kubwa za kuhuisha Uislamu na kueneza maarifa sahihi na asili ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu. Imam Hassan al Askari aliuawa shahidi kwa kupewa sumu na utawala wa Bani Abbas. ***

Kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hassan al-Askary (AS)

 

Katika siku kama ya leo miaka 209 iliyopita, alizaliwa karibu na mji mkuu wa Ufaransa, Paris Évariste Galois, mtaalamu wa hesabati. Hadi kufikia umri wa miaka 12, Galois hakufunzwa na mtu yeyote isipokuwa mama yake na alianza kusoma vitabu vya jiometri na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa.  Galois aliuawa  akiwa na umri wa miaka 21 hapo tarehe 29 mwezi Mei mwaka 1832 baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani. ***

Évariste Galois

 

Miaka 139 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Pablo Picasso mchoraji mashuhuri wa Kihispania. Picasso alikuwa mwasisi wa harakati ya Cubist ambayo ilienea kwa kasi kubwa miongoni mwa wachoraji wa Ufaransa. Pablo Picasso alichora picha nyingi na daima alikuwa akifanya juhudi za kuendeleza harakati hiyo. Mchoro wa 'The Girls of Avignon' wa mchoraji huyo ndio uliokuwa mwanzo wa mtindo wa Cubism na kazi kubwa zaidi ya Picasso katika mtindo huo ni 'Guernica'. Katika mchoro huo Pablo Picasso anaonesha hofu iliyompata kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za Ujerumani na Italia dhidi ya mji wa Guernica. Picasso alifariki dunia Aprili mwaka 1973. ***

Pablo Picasso

 

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, Imam Ruhullah Khomeini baada ya kuachiwa huru kutoka katika jela ya utawala wa Shah alitoa hotuba kali akishambulia vikali kitendo cha kupasishwa sheria ya Capitulation au sheria ya kuwapatia kinga ya kutofikishwa mahakamani raia wa Marekani waliofanya uhalifu nchini Iran. Katika hotuba hiyo Imam Khomeini alizishambulia vikali Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Hotuba hiyo iliwaamsha wananchi na kuukasirisha utawala wa kiimla wa Shah kiasi kwamba uliamua kumuwekea vizuizi vingi kiongozi huyo wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu. Siku chache baadaye Imam alipelekwa uhamishoni nchini Uturuki na baadaye Iraq. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, televisheni ya taifa ya Iran ilianza kurusha matangazo yake kwa majaribio. Katika muongo wa 1330 Hijria Shamsia kulijadiliwa suala la kuanzishwa televisheni ya taifa ya Iran ingawa utekelezaji wa mpango huo uliakhirishwa kwa miaka mingi. Uzalishaji wa picha tena kwa masaa kadhaa tu, halikuwa jambo rahisi kwani lilihitajia fedha na uwekezaji binafsi na wa kila wiki. Ni kwa msingi huo, ndio maana Habibullah Thabit Pasal mwekezaji wa sekta binafsi akaipendekezea serikali ya wakati huo ya Iran ianzishe mnara wa televisheni, pendekezo ambalo lilikubaliwa. Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran redio na televisheni ya taifa ilibadilishwa jina na kuwa Shirika la Utangazaji la Radio na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kupiga hatua kubwa mno katika uwanja huo. Hii leo shirika hili lina makumi ya kanali za televisheni na radio zikiwemo zile za kitengo cha matangazo ya ng'ambo ambapo kuna makumi radio na televisheni za lugha za kigeni kama, Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili, Kihispania, Kiarabu, Kihindi, Kipashto, Kiurdu, Kihausa na kadhalika. ***

نشان سازمان رادیو تلویزیون ملی ایران

 

Na miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Khorramshahr wa Iran ulikaliwa kwa mabavu na jeshi la dikteta wa zamani Iraq Saddam Hussein. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane. Mji huo ulikombolewa tarehe 3 Khordad ambayo inajulikana katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa jina la "Siku ya Istiqama na Ushindi. ***

Khorramshahr