Dec 17, 2020 02:48 UTC
  • Alkhamisi Disemba 17, 2020

Leo ni Alhamisi tarehe Pili Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 17 Desemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1051 iliyopita alifariki dunia Abu Is'haq Kisai Marvazi, malenga mashuhuri wa Iran. Marvazi alizaliwa mwaka 341 Hijiria mjini Marv, moja ya miji ya zamani ya Iran ambao hii leo unapatikana nchini Turkmenistan. Kipindi cha ujana wake kilienda sambamba na kumalizika utawala wa Samanid na kuanza utawala wa Ghaznavid. Ni kwa ajili hiyo ndio maana beti zake za mashairi zilihusu tawala hizo mbili. Aidha Abu Is'haq Kisai Marvazi alijulikana kwa kuwasifu sana katika mashairi yake Ahlu Bayti wa Mtume (saw) hususan Imam Ali Bin Abi Twalib. Kadhalika alikuwa akitoa mawaidha na hekima kupitia mashairi ya lugha ya Kifarsi. Abu Is'haq Kisai Marvazi ameacha athari nyingi katika uwanja huo ambazo zimehifadhiwa katika maktaba mbalimbali nchini Iran.

Abu Is'haq Kisai Marvazi

 

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sheikh Ali Akbar Nahavandi, msomi mkubwa mwenye zuhdi. Ayatullah Ali Akbar Ibn Mula Muhammad Hussein Nahavandi, ni mwenye asili ya mji wa Nahavand katika mkoa wa Hamadan nchini Iran ingawa alizaliwa mjini Mash'had. Awali alijifunza masomo ya Kiislamu mjini Tehran kwa Allamah Haj Mirza Hassan Ashtiyani kisha akaelekea mjini Najaf Iraq na kupata kusoma kwa Allamah Haj Mirza Habibullah Rashti na Shariat Isfahani. Mwaka 1328 Hijiria Ayatullah Sheikh Ali Akbar Nahavandi alielekea mjini Mash'had na kuweka huko makazi yake. Vitabu vya 'Al Bayaanur Rafii fii Ahwaali Khawaajah Rabii' 'Golzaar Akbari' na 'Lole Zaar' ni miongoni mwa athari za msomi huyo. Ayatuullah Sheikh Ali Akbar Nahavandi alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 90 na kuzikwa katika mji wa Mash'had.

Ayatullah Ali Akbar Ibn Mula Muhammad Hussein Nahavandi

Siku kama ya leo miaka 250 iliyopita alizaliwa Ludwig van Beethoven, mtunzi na muimbaji mashuhuri wa muziki wa nchini Ujerumani. Alizaliwa mjini Bonn mwaka 1770 Miladia. Akiwa kijana mdogo alikumbwa na matatizo mbalimbali lakini pamoja na hayo alienda kujifunza kwa wataalamu wakubwa wa fani hiyo wa zama zake kama vile Mozart na Joseph Haydn. Baadaye alikumbwa na tatizo la kutosikia huku akiwa kiziwi kabisa alipofikisha umri wa miaka 49. Ludwig van Beethoven anafahamika kwa kubuni Symphony namba tisa ambayo hii leo inatumika miongoni mwa Symphony zingine za muziki. Alifariki dunia Machi 26 mwaka 1826.

Ludwig van Beethoven

Siku kama ya leo miaka 242 iliyopita, alizaliwa Humphrey Davy mwanakemia na mwanafikizia wa Kiingereza. Katika majaribio yake ya kimaabara, msomi huyo aliweza kutenganisha elementi za Sodium, Potassium, Calcium, Barium, Magnesium na Strontium miongoni mwa elementi nyinginezo na hatua hiyo ilihesabiwa katika zama hizo kuwa mafanikio makubwa katika sayansi ya kemia. Davy mbali na kuwa mwasisi wa elimu inayojulikana kama "electrochemical", aliweza pia kuwasilisha nadharia ambayo iliitaja gesi ya Hydrojen kuwa gesi inayoweza kuzitambua asidi. Mwanakemia huyo wa Kiingereza alifariki dunia mwaka 1829.

Humphrey Davy

Miaka 117 iliyopita katika siku kama ya leo, ndege ya kwanza yenye injini ilitengenezwa duniani. Baada ya kufanyiwa majaribio mara kadhaa hatimaye ilipaa angani kwa karibu dakika moja. Ndege hiyo ilitengenezwa na ndugu wawili waliojulikana kwa jina la "Wright Brothers" na kufanyiwa majaribio katika jimbo la Carolina ya Kaskazini nchini Marekani. Ndugu hao wawili walikuwa wakitengeneza baiskeli na baada ya kushuhudia ndege zikipaa bila ya injini, walipatwa na hamu ya kufanya jitihada kubwa na hatimaye wakafanikiwa kutengeneza ndege ya kwanza yenye injini na kuirusha angani.

Wright Brothers

Na tarehe 17 Disemba miaka 10 iliyopita kijana mmoja wa Kitunisia kwa jina la Tariq Mohamed Bouazizi alijiteketeza kwa moto na kuanzisha harakati ya ukombozi wa wananchi wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa kidikteta wa Habib Bourguiba na Zainul Abidin bin Ali uliodumu kwa kipindi cha nusu karne. Kujichoma moto kwa Bouazizi ilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi. Bouazizi ambaye alikuwa na shahada ya chuo kikuu alikuwa akiuza bidhaa za mkononi mitaani aliponyang'anywa bidhaa zake na kudhalilishwa na afisa wa kike wa halmashauri ya mji na ndipo akaamua kujiteketeza kwa moto, kitendo ambacho kiliamsha hasira za wananchi wa Tunisia na kuwa chachu ya harakati iliyohitimisha utawala wa dikteta Zainul Abidin. Dikteta huyo alikimbia nchi na kupewa hifadhi na watawala wa kifalme wa Saudi Arabia na hatimaye kuaga dunia Septemba 19, 2019.

Tariq Mohamed Bouazizi