Ijumaa, Disemba 18, 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 3 Mfunguo Nane Jamadil Awwal mwaka 1442 Hijria mwafaka na tarehe 18 Desemba 2020 Miladia.
Siku kama ya leo, miaka 150 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Abu Abdillah, Sheikhul-Islami Zanjani, msomi mkubwa na mshairi wa Kiislamu. Msomi huyo mkubwa, alizaliwa mwaka 1224 Hijiria huko Zanjani, moja ya miji ya Iran na kuelekea Isfahani kwa ajili ya masomo akiwa kijana mdogo. Akiwa Isfahan, Ayatullah Mirza Abu Abdillah alipata kusoma katika hauza ya kielimu ambayo ilikuwa na itibari kubwa kielimu wakati huo. Baada ya kuhitimu masomo yake alirejea eneo alikozaliwa na kujishughulisha na kulea na kuto elimu kwa wanafanzu wake. msomi huyo ameandika vitabu kadhaa vikiwemo vya 'Hujjatul-Abraar' na 'Hidaayatul-Muttaqin'.
##########
Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ismail Sadr, alimu na mujtahidi wa ngazi ya juu mjini Kadhimiya, Iraq. Alisoma masomo ya awali ya dini ya Kiislamu kwa kaka yake na kisha akaelekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi katika uwanja huo. Akiwa mjini Najaf alijifunza elimu ya sheria za Kiislamu (fiqhi), elimu ya akhlaq na elimu nyingine tofauti za kidini. Baada ya kufariki dunia mwalimu wake mkubwa Ayatullah Mirza Shirazi, Ayatullah Sayyid Ismail Sadr alichukua jukumu la ufundishaji mjini Karbala nchini humo.
##########
Miaka 106 iliyopita katika siku kama ya leo, Uingereza iliikoloni rasmi Misri. Inafaa kukumbusha kwamba, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa Othmania ulikuwa mwitifaki wa madola yaliyokuwa yakiipinga Uingereza yaani Ujerumani na Austria. Uingereza nayo ikiwa na lengo la kukabiliana na kitendo hicho, iliikalia kwa mabavu Misri, ambayo hadi katika kipindi hicho ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Othmania. Harakati za ukombozi za wananchi wa Misri dhidi ya mkoloni Mwingereza zilizaa matunda mwaka 1922, ambapo nchi hiyo ilijitangazia uhuru wake.
##########
Tarehe 18 Disemba miaka 41 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha makubaliano ya kufuta aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake. Makubaliano hayo yana lengo la kuondoa dhulma zinazofanywa dhidi ya wanawake duniani. Hata hivyo makubaliano hayo, kama yalivyo mengine mengi ya kimataifa, yanatawaliwa na mitazamo ya kimaada ya Magharibi inayosisitiza usawa wa jinsia mbili za mwanamke na mwanaume katika kila kitu. Hii ni katika hali ambayo mwanamke na mwanaume wanatofautiana kimwili na kiroho. Kwa sababu hiyo dini za Mwenyezi Mungu hususan Uislamu zinasisitiza kuwa njia ya kuwakomboa wanawake ni kuwatayarishia mazingira ya uadilifu kwa kutilia maanani uwezo wao wa kimwili na kiroho.
#########
Na siku kama ya leo miaka 82 iliyopita msomi wa Ujerumani, Otto Hahn, alifanikiwa kupasua kiini cha atomu, hatua ambayo ilikuwa mwanzo wa zama za atomu. Mtaalamu huyo wa kemia alizaliwa mwaka 1879 huko Frankfurt na kupata shahada ya uzamivu katika taaluma ya kemia. Tangu wakati huo alijishughulisha na utafiti katika taaluma ya fizikia. Baada ya utafiti mkubwa na katika siku kama hii ya leo Otto Hahn alifanikiwa kupasua kiini cha atomu. Hatua hiyo iliibua nishati kubwa ambayo baadaye ilianza kutumika katika vinu na mabomu ya nyuklia. Mwaka 1944 Otto Hahn alitunikiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya kemia.