Jumapili, 27 Desemba, 2020
Leo ni Jumapili tarehe 12 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe 27 Desemba 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 489 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu Ibn Tulun Dimashqi, aliyekuwa faqihi, mwanafasihi na mwanahistoria huko mjini Damascus, Syria. Ibn Tulun alizaliwa mwaka 880 Hijiria mjini Damascus na katika umri wake wote alifanya jitihada kubwa za utafiti, kufundisha na kuandika vitabu vya taaluma mbalimbali. Ibn Tulun Dimashqi ameandika vitabu vingi vya thamani kuhusiana na historia ya Kiislamu na katika uwanja wa tafsiri ya Qur'ani Tukufu, hadithi, lugha, tiba na irfani. Kitabu cha 'al-Safiinatu al-Tuluuniyyah' ni miongoni mwa athari za mwanazuoni huyo. ***
Miaka 198 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Louis Pasteur, tabibu na mwanakemia wa Kifaransa. Akiwa shuleni Louis Pasteur alisoma kwa bidii na jitihada kubwa. Baada ya kumaliza masomo yake alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika kemia na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Strasbourg huku akijihusisha uhakiki na utafiti kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ulianzishwa. Miongoni mwa yaliyokuwa malengo muhimu ya mfuko huo, ni kuandaa nafasi zaidi za ajira, udhibiti wa thamani ya sarafu za kigeni na kuhakikisha kwamba, kunakuweko ukuaji wenye uwiano katika masoko ya kimataifa. Makao Makuu ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa yako mjini New York Marekani. ***
Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, kufuatia kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, mkataba wa kihistoria wa kuigawa Peninsula ya Korea ulitiwa saini mjini Moscow. Mkataba huo ulitiwa saini na wawakilishi wa nchi tatu za Uingereza, Marekani na Umoja wa Sovieti. Kwa mujibu wa mkataba huo, Peninsula ya Korea ambayo hadi katika zama hizo ilikuwa nchi moja ikagawanywa katika sehemu mbili. Kwa utaratibu huo, kukatokea nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Kusini mgawanyiko ambao ungalipo hadi leo. ***
Katika siku kama ya leo miaka 46 iliyopita inayosadifiana na tarehe 7 Dei 1353 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Ayatullah Hussein Ghaffari mmoja wa wanazuoni na mwanamapambano wa Kiislamu. Ayatullah Ghaffari aliuawa shahidi akiwa katika jela ya utawala wa wakati huo wa Kifalme hapa Iran. Ayatullah Ghaffari aliendesha harakati za kupambana na utawala wa kidikteta wa Mfalme Shah kwa kuandika vitabu na majarida mbalimbali. Baadaye alitiwa mbaroni na kutiwa jela na kufa shahidi katika siku kama ya leo, baada ya kuvumilia mateso mengi gerezani humo. ***
Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 7 Dei mwaka 1357, wananchi wa mji wa Qazwin Iran walifanya maandamano makubwa wakitangaza upinzani wao dhidi ya utawala wa kifalme wa Shah. Maandamano hayo yalifanyika sambamba na kushika kasi mapinduzi ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa kidikteta wa Kipahlavi. Vyombo vya usalama vya utawala wa Shah viliyakandamiza maandamano hayo na kupelekea umwagaji damu mkubwa ambapo watu 20 waliuawa shahidi. ***
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Dey mwaka 1358 Hijria Shamsia, Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alitoa amri ya kuanzishwa harakati ya kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika. Imam Khomeini alitoa amri kwa wananchi wote wa Iran kushirikiana bega kwa bega kwa shabaha ya kumtokomeza adui ujinga. Hivi sasa kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika nchini Iran kimeongezeka sana, na kufikia hatua kwa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kuiweka Iran kwenye kundi la nchi zenye idadi kubwa ya watu wanaojua kusoma na kuandika. ***
Katika siku kama ya leo miaka 13 iliyopita Bi Benazir Bhutto kiongozi wa Chama cha Wananchi cha Pakistan (PPP) aliuawa kwa kufyatuliwa risasi na mlipuko wa bomu uliofanywa na magaidi huko Rawalpindi kaskazini mashariki mwa Pakistan. Mbali na Bi Benazir Bhutto, watu wengine karibu 20 wafuasi wa chama cha PPP waliuawa pia katika mlipuko huo. Bhutto alikuwa Waziri Mkuu wa Pakistan kwa mara ya kwanza mwaka 1988 baada ya kuenguliwa madarakani serikali ya kijeshi iliyokuwa ikiongozwa na Jenerali Muhammad Zia ul Haq. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha hujuma kubwa na ya pande zote dhidi ya Ukanda wa Gaza magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wakazi wa eneo hilo waliwakasirisha viongozi wa Kizayuni kutokana na kupambana kwao kishujaa dhidi ya uchokozi na mashambulizi ya Wazayuni na pia hatua yao ya kuiunga mkono serikali halali ya Palestina iliyokuwa ikiongozwa na harakati ya Hamas. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Ukanda wa Gaza ukawekwa chini ya mzingiro wa kiuchumi wa utawala haramu wa Israel kwa karibu mwaka moja na nusu kabla ya mashambulizi hayo, mzingiro ambao unaendelea kuwasababishia Wapalestina wa eneo hilo matatizo chungu nzima kama vile ukosefu wa chakula na dawa. ***