Hadithi ya Uongofu (40)
Assalamu alaykum wapenzi wasikilizaji. Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kuchunguza na kupeleleza aibu za wengine ni miogoni mwa tabia mbaya na chafu ambayo huleta hali ya kutoelewana katika jamii na huondoa amani na utulivu wa mtu.
Tabia kutafuta na kupekua aibu za watu huandaa uwanja wa kuweko mtazamo mbaya, ugomvi, utengano na hata utumiaji mabavu na pengine kutawala anga ya kutoamiana baina ya watu. Akthari ya uhusiano wa wafanyakazi, marafiki, familia, jamaa na jamii mbalimbali husambaratika na kuvurugika kutokana na kuweko kwa tabia hii. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 40 ya mfululizo huu kitazungumzia maudhui hii na hadithi zinazohusiana na suala la kutafuta, kuchunguza na kufichua aibu za wengine. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
*********
Kwa hakika kutafuta na kuchunguza aibu na mapungufu ya watu ni moja ya maradhi ya kimaadili na kiakhlaqi ambayo hupelekea kuondoka na kuporomoka heshima ya watu wengine. Wapekuaji wa aibu za watu kwa kitendo chao hicho kilicho dhidi ya maadili huharibu heshima na thamani ya watu na hivyo kupelekea kuweko hali ya kudhaniana vibaya baina ya watu, suala ambalo hatimaye hupelekea kuibuka ufisadi. Sifa na tabia hii mbaya inatambuliwa na kioo cha mafundisho ya Uislamu kuwa ni katika madhambi makubwa. Qur’ani Tukufu imewaahidi adhabu watu wanaopekua na kuchunguza chunguza aibu na ambao kazi yao ni kueneza uvumi miongoni mwa watu.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya kwanza ya Surat Humazah:
Ole wake kila safihi, msengenyaji!
Katika asili neno Hamaza fasili na maana yake ni kuvunja na kuharibu; hii inatokana na kuwa, kuchunguza na kutaja aibu za watu ni kuharibu heshima na shakhsia yao. Sura ya Humazah imeanza na tishio na laana kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Laana na kemeo ambalo linawalenga watu ambao wanawafanyia maskhara na kebehi watu wengine na kupepekua pekua aibu zao.
Tunalopaswa kutambua hapa ni kwamba, mtu ambaye tabia yake ni kuchunguza aibu za watu na kuzitaja na hivyo kuharibu heshima na shakhsia ya waumini, Mwenyezi Mungu pia hufichua siri na aibu zake.
Mtume saw amenukuliwa akisema: Msichunguze na kutafuta aibu za Waislamu. Kila ambaye atafuatilia aibu za ndugu yake, Mwenyezi Mungu atafuatilia aibu zake. Na kila ambaye Mwenyezi Mungu atafuatilia aibu zake humuumbua hata kama atakuwa ndani ya nyumba yake.
Kuchunguza aibu za watu husambaratisha mshikamano na urafiki miongoni mwa watu.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 10 hadi ya 12 za Surat al-Hujuraat:
Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe. Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio wenye kudhulumu. Enyi mlio amini! Jiepusheni na dhana nyingi, kwani baadhi ya dhana ni dhambi. Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo! Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.
Aya zilizotangulia zinazitaja tabia kama za mtu kumdharua mwenzake, kuvunjiana heshima, kuitana majina ya kejeli, kuwa na dhana nyingi, kupeleleza na kupekua mambo ya watu, kusengenya na mengineyo kwamba, ni sababu ya kuondokana hali ya mshikamano na maelewano baina ya watu.
*********
Akthari ya matatizo ya jamii hutokea pale kila mtu anapoamua kuingilia maisha ya mwengine na kuchunguza aibu na mapungufu ya mwenziwe. Hapana shaka kuwa, mtu anapoamua kupekua na kupeleleza aibu za mwengine hatoishia tu katika kufahamu mapungufu na aibu za mwenzake huyo bali hatua inayofuata ni kusengenya na kutoa tuhuma jambo ambalo lenyewe hilo ni kutenda dhambi kubwa.
Aya ya 19 katika Surat Nuur inasema:
Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
Nukta muhimu katika aya hii ni kwamba, hapa Qur’ani haisemi “Watu wanaoeneza uchafu na mambo mabaya baina ya waumini watakumbwa na adhabu” la hasha bali inasema: Wale wanaopenda uenee uchafu kwa walioamini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera. Hii yenyewe ni ushahidi kwamba, heshima ya Waislamu mbele ya Mwenyezi Mungu ni jambo lenye kuzngatiwa na Allah hatoi idhini ya kuzungumziwa na kutajwa watu wengine kila ambalo linasemwa au linasikiwa kuhusiana na waumini. Hii ni kutokana na kuwa mtu hana haki ya kufichua siri ya mtu endapo atashuhudia kwa macho yake mtu fulani anafanya dhambi, seuze kusikia tu kutoka kwa watu na yeye hajashuhudia kwa macho yake.
Tunakiendeleza kipindi chetu kwa kisa kifuatacho:
Inanukuliwa kwamba, Bwana mmoja alikwenda kwa Imam Mussa bin Ja’afar al-Kadhim (a.s) na kumwambia:
Niwe mhanga wako Ewe Imam mwema! Nimeambiwa jambo na baadhi ya watu kuhusiana na ndugu yangu muumini ambalo kwa hakika halijanifurahisha. Nimemuuliza mhusika kuhusiana na mambo aliyosema kunihusu mimi, lakini amekana, ilihali kuna watu wa kuaminika ambao wameninukulia hilo. Baada ya Bwana yule kumaliza kuzungumza Imam Mussa al-Kadhim (a.s) akasema:
Usiyakubali unayoyasikia kuhusiana na ndugu yako Mwislamu, hata kama watatokea watu khamsini na wakala kiapo kwamba, bwana huyu amefanya jambo fulani lakini mwenyewe anasema hakufanya. Basi kubali maneno yake na uyakane ya wanaosema amefanya. Katu usieneze jambo ambalo ni chimbuko la aibu, fedheha kwake na kwa shakhsia yake katika jamii, kwani kufanya hivyo utakuwa miongoni mwa wanaowatuhumu watu ambao Mwenyezi Mungu anasema kuwahusu kwamba:
Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini, watapata adhabu chungu katika dunia na Akhera.
*********
Kwa hakika dini tukufu ya Kiislamu inalipa umuhimu maalumu suala la thamani na heshima ya watu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana dini hii tukufu inakataza kupeleleza na kuchunguza watu na maisha yao binafsi.
Hata hivyo kuna wakati mwingine aibu na mapungufu ya mtu fulani yako wazi na wadhiha lakini mhusika mwenyewe anapuuza aibu hiyo au hana habari kabisa. Hapa ni jukumu la rafiki mzuri kumueleza rafiki yake kuhusiana na aibu na mapungufu fulani aliyonayo ili aweze kujirekebisha.
Tab’an, jambo hili linapaswa kufanyika kwa njia ya siri ili lisitoe pigo kwa heshima na shakhsia ya mtu anayehusika.
Imam Hassan al-Askari (as) anasema kuwa:
Mtu ambaye anampa nasaha ndugu yake katika dini katika faragha na siri huwa ni pambo kwake; lakini kama atamnasihi mbele za watu, basi hatua hiyo humfanya ahisi aibu na fedheha.
Imam Ja’afar Swadiq (a.s) anasema kuwa: Miongoni mwa ndugu zangu katika dini ambaye ninampenda zaidi ni yule ambaye anayenizawadia aibu zangu.
Hivyo basi kama ambavyo kuchunguza na kupeleleza aibu za watu ni jambo baya na lililoharamishwa, vile vile kuficha aibu pia ni hiana na usaliti, kwani muumini anapaswa kuwa kioo cha muumini mwenzake na amuoneshe ndugu yake katika dini mabaya mazuri yeye mwenyewe na sio kuyapeleka kwa watu na hivyo kuweka vikao vya kusengenya na kutaja aibu za watu.
Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa kutokana na muda wa kipindi hiki kutupa mkono. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Ninakuageni nikimuomba Mwenyezi Mungu atuepushe na sifa mbaya ya kupeleleza na kuchunguza aibu za watu wengine.
Wassalaamu alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh