Feb 11, 2021 09:26 UTC
  • Alkhamisi tarehe 11 Februari mwaka 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 28 Jamadithani 1442 Hijria sawa na Februari 11 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 10 iliyopita Hosni Mubarak aliyekuwa amejitangaza Rais wa maisha wa Misri aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya wananchi. Mubarak ambaye awali alikua makamu wa Rais Anwar Saadat wa Misri alishika madaraka ya nchi mwaka 1981 baada ya kuuawa kiongozi wa nchi hiyo. Saadat aliuawa kwa kumiminiwa risasi na Khalid Islanbuli kutokana na kutia saini makubaliano ya Camp David na utawala ghasibu wa Israel na kusaliti malengo ya taifa la Palestina. Baada ya kushika madaraka Mubarak alifuata nyayo za Saadat na hadi anang'olewa madarakani alikuwa kibaraka na mtekelezaji mkubwa wa siasa za Marekani na waitifaki wake katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.

Hosni Mubarak

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita Mzee Nelson Mandela kiongozi wa harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini aliachiwa huru baada ya kufungwa jela kwa kipindi cha miaka 27. Mandela alikamatwa mwaka 1963 na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa sababu ya mapambano yake dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Mwaka 1991 alifikia makubaliano na makaburu wa nchi hiyo juu ya jinsi ya kukomesha utawala wa ubaguzi wa rangi na miaka kadhaa baadaye yaani mwaka 1994 alichaguliwa kuwa rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini.

Nelson Mandela

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita serikali ya mpito ya Mapinduzi ya Kiislamu ilianza rasmi kazi zake katika siku za mwanzo kabisa za umri wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Wakati huo huo wananchi waliendeleza mapambano ya kuangamiza kikamilifu mabaki ya utawala wa Shah. Baadhi ya makundi ya wananchi yalichukua jukumu la kulinda taasisi muhimu za serikali katika miji mbalimbali. Wakati huo ulidhihiri udharura wa kuwepo chombo cha kushughulikia kadhia hiyo na kukabiliana na vibaraka na mabaki ya utawala wa Shah. Kwa msingi huo Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini alitoa amri ya kuundwa Kamati ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Miaka 1140 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, alifariki dunia alimu na mwanafasihi wa Kiirani Mirza Muhammad bin Sulaiman Tonekaboni. Mbali na Tonekaboni kubobea katika elimu ya fiq'hi, pia alikuwa mtaalamu wa fasihi na mshairi mkubwa katika kipindi chake. Msomi huyo ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Al Fawaidu fii Usulud Din" na "Qasasul-Ulama."

Siku kama hii ya leo na miaka 852 iliyopita alifariki dunia Abul-Qasim al-Shatwibi, msomi mashuhuri wa Qur'ani na maarufu kwa jina la Imamul Qurra. Abul-Qasim alizaliwa mnamo mwaka 538 Hijria. Mbali na kuwa mtaalamu mkubwa katika usomaji wa Qur'ani, alikuwa pia mtaalamu wa taaluma ya tajweed, tafsiri ya Qur'an, hadithi, nahau, lugha na elimu nyinginezo za dini ya Kiislamu. Licha ya kuwa kipofu Shatwibi alikuwa hodari sana na alifanikiwa kuhifadhi hadithi nyingi kifuani. Shatwibi ameacha athari kwa vizazi vya baada yake na miongoni mwa athari hizo ni pamoja na kitabu cha "Al Qasidatus Shatwibiyyah" kinachohusiana na elimu ya tajweed.

Na siku kama ya leo miaka 2681 iliyopita mfalme wa kwanza wa Japan maarufu kwa jina la Jimmu alishika madaraka ya nchi. Kwa utaratibu huo mfumo wa kale zaidi na uliobakia kwa kipindi kirefu wa kifalme dunia ambao unaendelea hadi sasa, ulianzishwa. Wafalme wa Japan huwa na cheo cha heshima tu na Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa masuala ya nchi.

Bendera ya Japan

 

Tags