Jumatano tarehe 7 Aprili 2021
Leo ni Jumatano tarehe 24 Shaabani 1442 Hijria sawa na Aprili 7 mwaka 2021.
Katika siku kama ya leo miaka 300 iliyopita, Peter the Great mfalme wa wakati huo wa Russia aliivamia Sweden. Ruussia na Sweden zikishirikiana na Poland na Denmark kuanzia mwaka 1700 zilikuwa katika vita vya kaskazini. Wakati jeshi la Russia linaishambulia Sweden nchi hiyo ilikuwa imefikia mapatano na nchi nyingine zilizokuwa pamoja vitani na ilikuwa na mpango wa kupatana na Russia pia. Hata hivyo Peter the Great ambaye alikuwa na nia ya kupanua mamlaka yake, akiwa na jeshi lililojizatiti aliishambulia Sweden na baada ya kuishinda akaitwisha nchi hiyo mkataba wa amani.
Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, alizaliwa mtaalamu wa masuala ya Kiislamu wa Ujerumani Bi Annemarie Schimmel. Bibi Schimmel alipendelea mno kutalii na kupata maarifa kuhusu ustaarabu wa Kiislamu na alipata shahada ya uzamivu katika taaluma ya masuala ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Berlin akiwa na umri wa miaka 19. Prf. Annemarie Schimmel alifundisha kwa miaka mingi historia ya dini na irfani ya Kiislamu katika vyuo vikuu vya Marekani, Ujerumani na Uturuki. Mbali na kujua lugha za Kijerumani na Kiingereza, Bi Schimmel alijifunza pia lugha za Kiarabu, Kifarsi, Kiurdu, Kibengali na Kituruki kwa ajili ya kupata maarifa zaidi kuhusu masuala ya Kiislamu.
Prf. Annemmarie Schimmel ameandika vitabu kadhaa kuhusu masuala ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kile cha "Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu" na "Mwanamke katika Irfani ya Kiislamu".
Miaka 74 iliyopita muafaka na lsiku hii ya leo aliaga dunia msomi na mvumbuzi maarufu wa Kimarekani, Henry Ford akiwa na umri wa miaka 84. Ford alizaliwa mwaka 1863 katika familia ya kimasikini katika kijiji cha Greenfield nchini Marekani. Akiwa bado barobaro Henry Ford alijishughulisha na utengenezaji wa saa na alipokuwa kijana alifanya kazi ya umakanika. Henry Ford anatambuliwa kuwa mmoja wa wavumbuzi wa magari.
Miaka 73 iliyopita katika siku kama ya leo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifanya baraza la kwanza la dunia la afya na kuandika hati ya kwanza ya mkutano wa kimataifa wa afya. Baraza hilo pia lilichukua uamuzi kwamba tangu mwaka 1950 tarehe 7 Aprili itakuwa Siku ya Kimataifa ya Afya. Tangu mwaka huo tarehe 7 Aprili kila mwaka imekuwa ikiadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Afya.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita, Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliachiliwa huru kutoka jela kufuatia kujiri upinzani na mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran. Imam Khomeini alitiwa mbaroni na maafisa wa usalama wa utawala wa Shah, baada ya hotuba yake iliyofichua njama za utawala huo. Hata hivyo baada ya kutiwa mbaroni Imam Khomeini, kulishuhudiwa maandamano na upinzani mkubwa huku wananchi hao wa Iran wakitaka kuachiliwa huru kiongozi wao. Upinzani huo uliulazimisha utawala wa Mfalme Shah kumuachia huru Imam Khomeini.