May 02, 2021 00:47 UTC
  • Jumapili, Mei Pili, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 19 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1442 Hijria mwafaka na tarehe Pili Mei 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1402 iliyopita mwaka 40 Hijria Qamaria, Imam Ali bin Abi Talib AS ambaye ni mkwe, binamu na shakhsia wa karibu kwa Mtume Mtukufu SAW, alipigwa upanga wa sumu na kujeruhiwa vibaya akiwa anaswali swala ya alfajiri katika msikiti wa mji wa Kufa na mtu aliyeitwa Abdur Rahman bin Muljim Muradi. Imam Ali A.S alikufa shahidi baada ya siku 3. Ali bin Abi Talib ni shakhsia wa pili baada ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW ambaye anaelezwa na historia ya Uislamu kuwa shujaa, mwenye imani, akhlaki njema, elimu na uadilifu. Alipata elimu na mafunzo kutoka kwa Mtume Mtukufu mwenyewe SAW, na alikuwa mwanamume wa kwanza baada ya Mtume SAW kuukubali Uislamu. Katika vipindi tofauti daima Imam Ali AS alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume SAW katika hali zote za shida na matatizo na hata kuhatarisha maisha yake ili kumlinda Mtume Mtukufu na dini ya Uislamu huku akionyesha ushujaa mkubwa katika vita mbalimbali vya haki dhidi ya batili. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji mashuhuri, Imam Ali AS alikuwa mpole na mwenye upendo. Kiasi kwamba moyo wake ulikuwa ni wenye kuathirika sana na kujawa na huruma alipoona machozi ya mtoto yatima. Imam Ali AS alipenda haki na uadilifu na kupambana vilivyo na dhulma katika kila njanya. Katika sehemu ya matamshi yake yenye hekima Imam Ali AS anasema: 'Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hata kama watanilaza bila ya nguo juu ya miiba ya jangwani, au kunifunga pingu na kamba na kuniburuza juu ya ardhi, kwangu mimi jambo hilo ni bora kuliko kukutana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake siku ya Kiama hali ya kuwa nimewadhulumu waja wake.' ***

 

Siku kama ya leo miaka 610 iliyopita alifariki dunia Ghiyathud-Din Jamshid Kashani, mwanahisabati na mtaalamu mashuhuri wa nyota wa Iran. Jamshid Kashani alikuwa mtaalamu mkubwa wa hesabati na mnajimu kama ambavyo alihusika katika kuvumbua vifaa vingi na zana muhimu za kufuatilia nyota. Aidha Ghiyathud-Din Jamshid Kashani alihusika katika ujenzi wa kituo cha kufuatilia harakati za nyota cha Samarqand. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu ameacha athari zenye thamani katika uga wa hisabati na nyota vikiwemo vitabu vya ‘Miftaahul-Hisaab’ na ‘Risaalatu Aalaat Rasad.’ ***

Ghiyathud-Din Jamshid Kashani,

 

Katika siku kama ya leo miaka 502 iliyopita, alifariki dunia mchoraji na msanifu majengo maarufu wa Italia Leonardo da Vinci. Alizaliwa mwaka 1452 na umahiri wake ulidhihiri haraka katika nyanja mbalimbali za sanaa. Baada ya kufanya safari katika miji kadhaa ya Italia, mwaka 1506 Da Vinci alielekea Ufaransa na kuwa mchoraji wa Mfalme Louis xii. Aliishi katika kipindi cha mchoraji mwingine mashuhuri wa Italia Michelangelo na wasanii hao wawili mashuhuri walitoa mchango mkubwa katika sanaa na kipindi cha mwamko wa Ulaya (Renaissance). Miongoni mwa michoro maarufu ya Leonardo Da Vinci ni The "Last Supper" na "Mona Lisa".  Mbali na uchoraji, Leonardo Da Vinci alikuwa amebobea pia katika taaluma nyingine kama hisabati. ***

Leonardo da Vinci

 

Miaka 408 iliyopita katika siku kama ya leo, kipindi cha utawala wa Kitsar wa ukoo wa Romanov kilianza huko nchini Russia. Miaka mitatu baada ya mashambulio ya Poland dhidi ya Russia, mmoja wa makamanda wa Kirusi aliibuka mshindi na kuukomboa mji wa Moscow kutoka katika uvamizi wa jeshi la Poland na Mikhail Romanov akachaguliwa kuwa mtawala mpya wa Kitsar. Kwa hatua hiyo, kipindi cha miaka 304 cha utawala wa familia ya Romanov kikawa kimeanza huko Russia. Katika zama za utawala wa ukoo wa Romanov,  nchi ya Russia ilipanuka mno, lakini kwa upande wa kiuchumi haikupiga hatua ya kuzingatiwa na udiketa na ukandamizaji wa Waromanov ulizuia wananchi wa Russia kushiriki katika kuainisha mustakabali wao.***

Mikhail Romanov

 

Na miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 12 Ordibehesht 1358 Hijria Shamsia, mwanachuoni na mwanafikra mashuhuri wa Kiislamu Ayatullah Murtadha Mutahhari, aliuawa shahidi na kundi lililo dhidi ya mapinduzi la Furqan hapa nchini. Tukio hilo lilitokea katika kipindi cha chini ya miezi mitatu tangu kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hapa Iran. Shahidi Mutahhari alijistawisha kielimu kutoka kwa maulamaa wakubwa wakiwemo Ayatullahil Udhma Burujerdi, Allamah Tabatabai na Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Murtadha Mutahhari ameandika makumi ya vitabu nyanja mbalimbali. ***

Murtadha Mutahhari