Alkhamisi tarehe 6 Mei 2021
Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Ramadhani 1442 Hijria sawa na tarehe 6 mwezi Mei mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 188 iliyopita sawa na tarehe 23 Ramadhani mwaka 1254 Hijria, ilikamilika kazi ya uandishi wa kitabu cha ‘Jawaahirul-Kalaam’ ambacho kimejumuisha masuala muhimu ya sheria za Mwenyezi Mungu juu ya halali na haramu na kadhalika sheria mbalimbali za dini ya Kiislamu. Ni vyema kuashiria kuwa, kitabu cha Jawaahirul-Kalaam kimebainisha kwa undani masuala mengi ya sheria kiasi kwamba hadi sasa hakuna msomi aliyeweza kuandika kitabu kama hicho. Kunukuu kauli za wasomi wakubwa wa sheria za Kiislamu na kuzitolea ushahidi kwa umakini wa hali ya juu, ni kati ya nukta muhimu za kitabu hicho. Ayatullah Muhammad Hassan Najafi, mtunzi wa kitabu hicho, alianza kazi ya uandishi wa kitabu cha Jawaahirul-Kalaam akiwa na umri wa miaka 25 huku akitumia karibu miaka 30 kukiandika. Katika kipindi cha maisha yake kulitawala hujuma za fikra potofu za genge la Uwahabi na watu wa kundi la Ikhbariyyun suala ambalo lilimfanya Ayatullah Muhammad Hassan Najafi kuelezea umuhimu wa kuwa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu. Ni baada ya hapo ndipo alipotoa nadharia kuwepo Waliyyu Faqihi ‘walii kiongozi' anayesimamia masuala ya sheria za Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa masuala ya kimaumbile na msomi mkubwa wa Kijerumani, Alexander Humboldt. Alizaliwa mwaka 1769 huko Berlin, Ujerumani. Alifanya safari ndefu katika mabara ya Asia na Amerika kwa ajili ya kufanya utafiti. Tafiti nyingi za msomi huyo zilihusu namna dunia ilivyoumbwa.
Tarehe 6 Mei miaka 1882 iliyopita mtaalamu wa Ujerumani, Robert Heinrich Koch ilitangaza habari ya kugunduliwa vijidudu maradhi vya ugonjwa wa kifua kikuu (TB). Mtaalamu huyo wa masuala ya baiolojia alikuwa amegundua vijidudu maradhi hivyo ambavyo vimefupisha umri wa zaidi ya watu bilioni moja wiki mbili kabla. Baadaye Prf Robert Koch aligundua njia ya kufubaza na kutenga vijidudu maradhi hivyo ambavyo vilikuwa sugu mkabala wa dawa na vilikuwa na uwezo wa kujificha mwilini kwa miaka mingi na kujitokeza wakati mwafaka.
Mbali na kugundua vijidudu maradhi vya kifua kikuu, Prf Robert Koch pia aligundua vijidudu maradhi vya kipindupindu katika safari zake katika nchi za Misri na India na mwaka 1906 alitengeneza dawa ya Atoxy inayoshabihiana na Quinine. Prf Robert Koch anatambuliwa kuwa mtaalamu mkubwa zaidi wa vijidudu maradhi duniani baada ya Luis Pastore na alitoa huduma kubwa sana kwa elimu na sayansi ambayo kamwe haitasahaulika
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita yaani tarehe 23 Ramadhani mwaka 1392 Hijria Qamaria, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai mwanafalsafa, arifu na faqihi mkubwa wa Kiirani alikamilisha kazi ya uandishi wa tafsiri kubwa na ya aina yake ya Qur’ani ya al Mizan. Tafsiri hiyo ya Qur’ani ni moja kati ya tafsiri kubwa na makini zaidi za Qur’ani Tukufu na iliandikwa katika kipindi cha karibu miaka 20. Sifa kubwa zaidi ya tafsiri hiyo ni kwamba imefasiri aya za Qur’ani kwa msaada wa aya nyingine za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Tafsiri hiyo kubwa na adhimu iliandikwa na Allamah Tabatabai kwa lugha ya Kiarabu na hadi sasa imetarjumiwa katika lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiingereza na Kihispania.