Jumapili, Mei 9, 2021
Leo ni Jumapili tarehe 26 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1442 Hijria mwafaka na tarehe 9 Mei 2021 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 368 iliyopita, kazi ya ujenzi wa jengo la Taj Mahal linalohesabiwa kuwa miongoni mwa majengo ya kuvutia zaidi duniani na moja kati ya mifano bora zaidi ya usanifu majengo wa Kiislamu huko India ilimalizika baada ya miaka 22. Ujenzi wa jengo la Taj Mahal ulianza baada ya kufariki dunia mke wa Shah Jahan, mfalme wa India huko katika jimbo la Agra. Jengo hilo lilijengwa kwa kutegemea ramani iliyochorwa na msanifu majengo mashuhuri wa Iran, Issa Isfahani. Kwa upande wa nje, jengo la Taj Mahal limenakshiwa kwa ustadi kwa rangi mbalimbali huku kuta zake zikiwa zimeandikwa maandishi ya Kiarabu yenye aya za Qur'ani Tukufu. Ndani ya jengo hilo kuna makaburi mawili ya mfalme Shah Jahan na mkewe, Nur Jahan. ***
Miaka 317 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 26 Mwezi wa Ramadhani mwaka 1125 Hijria Qamaria, aliaga dunia Mohammad Khonsari aliyekuwa na lakabu ya Jamaluddin, alim na mwanazuoni mkubwa Muirani wa zama zake. Alizaliwa katika familia yenye kufungamana kikamilifu na mafundisho ya Kiislamu katika mji wa Isfahan, moja kati ya miji ya kati mwa Iran. Alisomea taaluma mbali mbali za Kiislamu kama vile itikadi, mantiki, falsafa, fiqhi na tafsiri. Jamaluddin Khonsari aliandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na ufafanuzi kuhusu kitabu cha Shifaa cha Abu Ali Sina, msomi maarufu Muirani.***
Tarehe 9 Mei miaka 216 iliyopita aliaga dunia mwandishi, malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kijerumani kwa jina la Johann Christoph Friedrich von Schiller akiwa na umri wa miaka 46. Von Schiller alipenda sana masuala ya uandishi tangu utotoni mwake. Friedrich Von Schiller alikuwa hodari katika fasihi ya Kijerumani na anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waandishi mahiri wa Kijerumani katika uga wa fasihi. ***
Na miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 9 Mei, mkataba wa kihistoria wa Sykes-Picot ulitiwa saini na wawakilishi wa Uingereza, Ufaransa na Urusi ya zamani. Hata hivyo Umoja wa Kisovieti baadaye ulijitoa kwenye makubaliano hayo baada ya mapinduzi ya Bolshevik. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, tawala za Uingereza na Ufaransa ziligawana nchi za Kiarabu zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Kiothmania. Kwa msingi huo Iraq na Jordan zikawa chini ya udhibiti wa Uingereza huku Syria na Lebanon zikitawaliwa na Ufaransa. ***