Jumanne tarehe 22 Juni 2021
Leo ni Jumanne tarehe 11 Dhulqaada 1442 Hijria sawa na tarehe 22 Juni mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1294 iliyopita, sawa na tarehe 11 Dhulqaad mwaka 148 Hijria, alizaliwa Imam Ali bin Mussa Ridha (as), mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (as) katika mji wa Madina. Imam Ridha alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu mara baada ya kufariki dunia baba yake Imam Mussa al-Kadhim (as), mnamo mwaka 183 Hijiria. Shakhsia huyo alikuwa mbora zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu wakati wa zama zake. Kwa minajili hiyo, Ma'amun Khalifa wa Kiabbasi alijaribu kumpatia wadhifa Imam Ridha (as) kwa shabaha ya kuimarisha nafasi yake na wakati huo huo kumdhibiti Imam. Imam Ridha (as) alikubali pendekezo hilo kwa kulazimishwa na kwa mashinikizo ya utawala wa Ma'amun. Mtukufu huyo aliwaeleza Waislamu wote, wakiwemo watu wa eneo la Khorasan, ukweli wa mambo ulivyo, na kuwaathiri mno wananchi kuhusiana na uhakika wa Ahlul-Bayt wa Mtume (as). Redio Tehran inatoa mkono wa heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani hususan wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume (as) kwa mnasaba huu.
Siku kama ya leo miaka 1106 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 11 Dhul Qaad 336 Hijria, ilizaliwa Muhammad bin Muhammad mwenye lakabu ya Sheikh Mufid, msomi na mwanafaqihi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu katika mji wa Baghdad. Sheikh Mufid alilelewa katika familia ya kielimu, kidini na yenye imani na kisha kujipatia elimu kutoka kwa wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Miongoni mwa harakati zake za kifikra na kiutamaduni za Sheikh Mufid ilikuwa ni kufanya midahalo na mafaqihi na wasomi wa Madhehebu mbalimbali. Sheikh Mufid ametuachia vitabu mbalimbali vyenye thamani vikiwemo al Irshaad, al Arkaan na Usulul Fiqh.
Miaka 388 iliyopita mnajimu, mtaalamu wa hisabati na mwanafizikia wa Italia Galileo Galilei alilazimika kukana itikadi zake za kisayansi na kielimu mbele ya viongozi wa Kanisa. Mwaka 1632 Galilei aliandika kitabu akijibu na kukosoa mitazamo ya Betlemosi kuhusu sayari ya jua na kutangaza kuwa dunia inazunguma jua. Mwaka mmoja baadaye Papa wa Kanisa Katoliki alimwita Galileo mjini Roma na kuitaja mitazamo hiyo ya kisayansi kuwa ukafiri. Kwa msingi huo, kanisa lilimlazimisha Galileo akane itikadi zake za kielimu la sivyo akabiliwe na adhabu ya kifo. Japokuwa msomi huyo alikana mitazamo yake hiyo ya kielimu kidhahiri tu lakini wakati alipotoka nje ya mahakama alipiga chini mguu wake na kuiambia ardhi: "Licha ya haya yote lakini wewe unazunguka."
Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, katika Vita vya Pili vya Dunia, jeshi la Ujerumani ya Kinazi lilianza mashambulizi makubwa dhidi ya Urusi ya zamani kwa jina la Operesheni ya Barbarossa. Kwa utaratibu huo Adolph Hitler akaanzisha vita vingine katika upande wa mashariki mwa Ujerumani kwa shabaha ya kutimiza mipango yake ya kutaka kujitanua zaidi. Hadi wakati huo tayari dikteta huyo alikuwa ameteka nchi kadhaa za Ulaya. Katika operesheni hizo, askari wa Ujerumani walisonga mbele na kufika katika viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo, Moscow. Hata hivyo jeshi la Ujerumani lilipata matatizo makubwa kufuatia kuanza kipindi cha baridi kali na hivyo likashindwa kusonga mbele. Wananchi na jeshi la Urusi katika miji mbalimbali ya nchi hiyo hususan Moscow, Leningrad na Stalingrad walipambana vikali na jeshi hilo vamizi na kulilazimisha kurudi nyuma. Mwezi Agosti 1944 jeshi la Urusi lilifika katika mipaka ya Ujerumani.
Miaka 40 iliyopita sawa na tarehe Mosi Tir mwaka 1360 kwa mujibu wa Kalenda ya Kiirani, hayati Imam Ruhullah Khomeini alipasisha uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu wa kutokuwa na imani na rais wa wakati huo Abul Hassan Bani Sadr na kwa utaratibu huo kiongozi huyo akalazimika kung'atuka madarakani. Bani Sadr ni miongoni mwa watu waliojidhihirisha kuwa wapenzi na watetezi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya Imam Khomeini kuhamia Paris, Ufaransa na alifanikiwa kushika madaraka ya nchi na kuwa rais katika uchaguzi wa kwanza wa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini kwa kutumia ujanja wa kipropaganda. Muda mfupi baadaye Imam Khomeini alimkabidhi ukamanda wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo Bani Sadr aliyekuwa mtu mwenye uchu wa madaraka, mwenye kiburi na msaliti alianza mara moja kushirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kuangusha utawala wa Kiislamu nchini Iran.