Jul 08, 2021 04:17 UTC
  • Alkhamisi tarehe 8 Julai 2021

Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Dhulqaada 1442 Hijria sawa na 8 Julai mwaka 2021.

Miaka 65 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mtaalamu, mwanafikra na mwandishi wa Kitaliano, Giovanni Papini. Alizaliwa mwaka 1881 katika mji wa Florence nchini Italia. Giovanni alipitia kipindi kigumu cha utoto na ujana wake. Hata hivyo hamu kubwa ya masomo ilimpelekea kwenda katika maktaba za kijamii na kuzidisha elimu na taratibu alidhihirisha uwezo wake mkubwa katika taaluma ya fasihi. Msomi huyu ameandika vitabu vingi kama "A Man--Finished," "The Failure," na "Life of Christ".

Katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Muhammad Mahdi Rabbani Amlashi aalimu na mujahidi wa Kiirani. Ayatullah Amlashi alizaliwa mwaka 1313 Hijria Shamsiya katika familia ya kidini katika mji mtukufu wa Qum na kuanza masomo ya kidini katika mji huo. Mwanazuoni huyo alipambana vilivyo kwa miaka mingi katika njia ya kuutetea Uislamu na kulinda thamani zake. Kama walivyokuwa viongozi na wafuasi wengine wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Rabbani Amlashi katika uhai wake hakuacha kufanya juhudi za kupambana dhidi ya utawala wa Shah licha ya kufungwa na kubaidishwa.

Ayatullah Muhammad Mahdi Rabbani Amlashi

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, alifariki dunia Kim Il-sung aliyekuwa Kiongozi na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti wa Korea Kaskazini. Kim Il-sung alizaliwa mwaka 1912. Akiwa na cheo cha ukapteni jeshini alirejea kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 1945 akiandamana na jeshi. Alipanda ngazi ya uongozi haraka na akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha wakomunisti wa nchi hiyo. Mwaka 1948 wakati nchi hiyo ilipoasisiwa na kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, Kim Il-sung alifikia cheo cha uwaziri mkuu. Katika vita vya Korea, Kim Il-sung aliteuliwa kuwa kamanda mkuu wa majeshi ya nchi hiyo na mwaka 1972 akawa rais wa taifa hilo.

Kim Il-sung

Siku kama ya leo miaka 6 iliyopita yaani tarehe 27 Dhulqaada 1436 Hijria winchi lililokuwa limewekwa katika eneo la mashariki ndani ya Msikiti mtakatifu wa Makka lilianguka na kuua idadi kubwa ya mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Katika tukio hilo lililotokea saa 17.1 kwa wakati wa Makka, mahujaji 107 waliuawa na wengine 238 walijeruhiwa. Mahujaji wengi waliopoteza maisha katika tukio hilo ni kutoka nchi za India, Pakistan, Indonesia na Iran. Serikali ya Saudi Arabia ilitangaza kuwa sababu ya kuanguka winchi hiyo ni upepo na tufani kali iliyovuma mjini Makka.

Tukio hilo lililodhiohirisha uzembe wa serikali ya Saudia na la lile la maafa ya Mina katika siku ya Idi Kubwa mwaka huo huo ni miongoni mwa matukio machungu zaidi katika historia ya ibada ya Hija. Maelfu ya Waislamu walifariki dunia katika maafa ya Mina wakati wa kuelekea kwenye eneo la kumpiga mawe shetani.