Jul 09, 2021 21:58 UTC
  • Jumamosi, Julai 10, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 29 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1442 Hijria sawa na tarehe 10 Julai 2021 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1147 iliyopita, kisiwa cha Iceland kilichoko kaskazini mwa Ulaya na jirani na nchi ya kaskazini kiligunduliwa na wavuvi wa Kinorway. Kisiwa hicho mwaka 1261 kilidhibitiwa na Norway. Katika kipindi cha zaidi ya karne moja iliyofuata, Denmark ilizidhibiti nchi zote mbili za Iceland na Norway. Hatimaye mwaka 1944 Iceland ilijipatia uhuru wake kamili kutoka kwa Denmark. ***

Bendera ya Iceland

 

Miaka 280 iliyopita ardhi ya Alaska iligunduliwa na mvumbuzi wa Kidenmark kwa jina la Vitus Bering. Mvumbuzi huyo aligundua ardhi ya Alaska inayopatikana kaskazini magharibi mwa Canada akiwa katika safari yake kuelekea Urusi. Hadi kufikia mwaka 1867 eneo tajiri kwa mafuta la Alaska lilikuwa sehemu ya mamlaka ya Urusi ya Kitezari. Hata hivyo mwaka huo Urusi iliiuzia Marekani ardhi ya Alaska kwa kiasi cha dola milioni saba, eneo ambalo leo hii linahesabiwa kuwa jimbo la 49 la Marekani. ***

Vitus Bering

 

Katika siku kama ya leo miaka 165 iliyopita, alizaliwa Nikola Tesla mwanafizikia mashuhuri wa Yugoslavia. Wakati wa kipindi chake cha masomo Tesla alikuwa na mapenzi makubwa na elimu ya fizikia. Kutokana na ufahamu na maarifa ya hali ya juu aliyokuwa nayo alipewa lakabu ya mtu mwenye kipaji. Baada ya kumaliza masomo yake Nikola Tesla alianza kufanya uhakiki katika uga wa umeme. Msomi huyo wa Kiyugoslavia alifanya tafiti na uvumbuzi wake mwingi katika uwanja wa nishati ya umeme na kupata mafanikio makubwa. Umeme mbadala au altenative electricity unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafikizia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux). Hatimaye msomi huyo aliaga dunia tarehe 10 Mei mwaka 1943 akiwa na umri wa miaka 87. ***

Nikola Tesla

 

Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, Italia iliingia rasmi katika Vita vya Pili vya Dunia ikiwa muitifaki wa Ujerumani ya Kinazi. Katika zama hizo, Benito Mussolini kiongozi wa chama cha Kifashti ndiye aliyekuwa Waziri Mkuu wa Italia. Kuingia jeshi la Italia katika Vita vya Pili vya Dunia licha ya kuwa kuliongeza uharibifu, lakini Musolini hakuweza kutoa msaada muhimu kwa kiongozi wa wakati huo wa Ujerumani ya Kinazi Adolph Hitler. ***

Benito Mussolini

 

Miaka 81 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na 10 Julai 1940 Jemadari Henri Petain Waziri Mkuu wa muda na afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Ufaransa, alichukua uongozi baada ya Ufaransa kushindwa na Wanazi wa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia. Kwa mujibu wa mkataba wa kivita uliosainiwa na nchi mbili hizo tarehe 22 Juni 1940, eneo la kaskazini mwa Ufaransa, ukiwemo mji wa Paris lilibaki chini ya himaya ya jeshi la Ujerumani ya Kinazi. ***

Jemedari Henri Petain 

 

Na miaka 48 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Bahamas huko Amerika ya Kati vilipata uhuru kutoka Uingereza na siku kama ya leo hufahamika visiwani humo kama siku ya taifa. Visiwa vya Bahamas viligunduliwa mwaka 1492 na mvumbuzi wa Ulaya Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania. Visiwa vya Bahamas vilipata uhuru mwaka 1973 na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Visiwa vya Bahamas viko kaskazini mwa Cuba na kusini mashariki mwa Marekani. 

Bendera ya Visiwa vya Bahamas