Jul 18, 2021 05:39 UTC

Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.

ipindi chetu kilichopita kilizungumzia  na kutupia jicho kwa mukhtasari historia na maisha ya msomi mwingine wa Kishia ambaye si mwingine bali ni Ali bin Hassan Karaki mashuhuri zaidi kwa lakabu ya Muhaqqiq Thani au Muhaqqiq Karaki. Tulisema katika kipindi kilichopita kwamba, Ali bin Hassan Karaki alizaliwa mwaka 865 katika kijiji cha Karak moja ya vijiji na viunga vya Jabal Amil nchini Lebanon. Muhaqqiq Karaki au Muhaqqiq Thani alikipitisha kipindi cha utoto na kukua kwake katika familia ya kielimu. Kadhalika tulieleza kwamba, Mwanazuoni huyu ana vitabu 71 ambapo maarufu zaidi na ambacho kinahesabiwa kuwa dafina na Johari kubwa ni Sherh Kitab Qawaid Allamah Hilli ambacho kimeondokea kuwa mashuhuri zaidi kwa jina la Jamiul Maqasid fi Sherh al-Qawaid.  Sehemu ya 25 ya mfululizo huu juma hili itaendelea kumzungumzia msomi huyu. Endeleeni kunitegea sikio.

 

Baada ya Khaje Nassirddin Tusi, Muhaqqiq Karaki anahesabiwa kuwa mtu aliyefanya juhudi kubwa mno kwa ajili ya kuinua jina la madhehebu ya Shia na maktaba ya Ahlul-Baiti (as) nchini Iran.

Moja ya nukta muhimu za kuweko Muhaqqiq Karaki nchini Iran ni hatua ya alimu huyo mkubwa ya kuingia katika masuala ya kisiasa na kijamii. Alikuwa akiamini kwamba, uongozi na usimamizi wa nchi na masuala ya watu yanapaswa kuwa kwa mujibu dini na uongozi wa Fakihi Mtawala aliyetimiza masharti. Mtazamo huu ndio ile nadharia ya Wilayatul-Faqih (Utawala wa Fakihi) ambao unaaminiwa na wanazuoni wengi wa Kishia. Kama ambavyo Muhaqqiq Karaki katika athari na vitabu vyake alibainisha nadharia ya kisiasa ya Uislamu kuhusiana na kusimamisha utawala, katika uga wa kivitendo pia aliitekeleza nadharia hiyo kadiri alivyoweza. Mtawala wa wakati huo wa Iran, Shah Tahmasebi alivutiwa mno na haiba na shakhsia ya kielimu ya mwanazuoni huyo kiasi cha kufikia kusema: Wewe unastahiki zaidi kuongoza na kusimamia masuala ya nchi kuliko mimi; kwani wewe ni naibu wa Imam Mahdi (atfs) na mimi ni mmoja wa watawala wako.

Mfalme Tahmasebi alimpatia Muhaqqiq Karaki hadhi na daraja ya Sheikhul Islami ambayo katika zama hizo ilikuwa ikihesabiwa kuwa daraja na cheo cha juu kabisa cha kiongozi wa dini na akamkabidhi masuala ya usimamizi wa nchi. Alimu huyu alitumia fursa hii kufanya marekebisho na mageuzi katika jamii ya Waislamu kadiri ya uwezo wake na kutumia jukumu alilokuwa amepatiwa kwa njia bora kabisa.

 

 

Muhaqqiq Karaki alianza mjadala wa Wilayatul-Faqi sambamba na kadhia ya Uimamu. Mwanazuoni huyo analihesabu suala la Uimamu kwamba, lina adhama kama adhama ya Utume na anauhesabu Uimamu kuwa ni katika Usul Din yaani misingi ya dini.

Anasema: Sababu na hoja ile ile inayowafanya watu kumhitajia Mtume ndio ileile inayowafanya pia  wamhitajie Imam; kwani daima watu ni wenye kuhitajia kiongozi mwenye nguvu na awe ndio dira yao. Hii ni kutokana na kuwa, msukumo wa kuleta shari daima upo.

Aidha akipinga suala la dini kutenganishwa na siasa anasema: Haiwezekani kusema kwamba, watu wanamhitajia kiongozi na mtawala katika masuala yao ya kidunia duni na kwamba, utawala ni jambo linalohusiana na masuala ya kidunia tu. Kwa mtaszamo wa Muhaqqiq Karaki ni kuwa, masuala ya kisheria nayo pia yanahusiana na mfumo wa maisha na ulimwengu wa watu. Kwa mfano, kuteua na kuuzulu licha ya kuwa ni jambo linalohusiana na sheria, lakini lina uhusiano na ulimwengu wa watu.

Alimu huyo anasema, lengo la kutumwa Mitume lilikuwa ni kuwaongoza watu katika masuala ya dunia na akhera na anaamini kwamba, masuala ya ibada yanahusiana na akhera ya watu, lakini kuna sheria nyingi na maamrisho ya Uislamu ambayo yanahusiana na dunia yao. Kwa muktadha huo, watu ambao wanaweza kuchukua jukumu la utekelezaji wa hukumu na sheria za dini ni wale ambao ni wateule kutoka kwa Mtume (saw) na kinyume na wao, kila ambaye atachukua cheo na jukumu hilo atakuwa dhalimu.

Karaki alikuwa akiamini kuwa, fakihi ambaye ana ustahiki wa kuchukua jukumu kwa niaba ya Imam Maasumu katika zama za ghaiba, anapaswa kuwa na sifa na vigezo maalum. Kwa mtazamo wake, moja ya masharti ya fakihi huyo ni imani, kwani fakihi ambaye siyo muumini siyo muadilifu. Uadilifu nao ni katika sifa na masharti mengine ambayo fakihi anapaswa kuwa nayo. Sifa nyingine ni kuwa na elimu na ufahamu na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume saw, kwa kiwango ambacho aweze kutoa na kunyambua hukumu na maagizo ya kidini kutoka katika vynazo vyake yaani Kitabu na Sunna.

Swala ya Ijumaa ni moja ya ibada ya kimaanwi na kisiasa kwa Waislamu

 

 

Kuhusiana na kusimamisha Swala ya Ijumaa, Muhaqqiq Karaki anaamini kuwa, ni lazima hilo lifanyike kwa kuweko Imam au naibu wake. Alimu huyu alinukuu nadharia za wapinzani wa kusimamishwa Swala ya Ijumaa katika zama za Ghaiba ya Imam wa zama yaani Imam Mahdi (atfs) kama Sayyid Murtadha na Ibn Idris Hilli na kupingana na hoja zao. Wapinzani wa hilo walikuwa wakitoa hii kwamba, kwa kuwa moja ya masharti ya kusimamisha Swala ya Ijumaa ni uwepo wa Imam au mtu ambaye yeye mwenyewe amemteua, hivyo Swala ya Ijumaa katika zama za Ghaiba haiwezi kuswaliwa. Hivyo basi wakati Swala ya Ijumaa inaposwaliwa bila ya uwepo wa Imam, Swala ya adhuhuri inabakia katika mabega ya waumini; lakini kama Imam yupo, pakiswaliwa Swala ya Ijumaa basi Swala ya Adhuhuri haipaswi kuswaliwa. Hata hivyo Karaki alikuwa akipinga nadharia hii. Alikuwa akiamini kwamba, fakihi aliyetimiza masharti kiujumla ni ameteuliwa na Imam, hivyo anaweza kusimamisha Swala ya Ijumaa.

Hatimaye mwaka 940 Hijria mwanazuoni huyu alirejea katika mji wa Najaf al Ashraf nchini Iraq. Nukuu za historia zinaonyesha kuwa, wakati anarejea Najaf alikuwa na umri wa miaka 70. Alimu huyu alirejea katika mji huo huku nyuma akiwa ameacha taathira kubwa na muhimu mno za kielimu katika Ulimwengu wa Kishia. Baada ya siku chache tangu kurejea kwake, kuliripotiwa habari ya mbaya na ya kusikitisha ya kufa kwake shahidi. Hii ilikuwa ni habari mbaya mno kwa wafuasi na vipenzi vyake na hata wale ambao ni wapenzi wa elimu na maarifa.

Muhaqqiq Karaki aliuawa kwa kupewa sumu na mmoja wa wapinzani wake na hivcyo akafa shahidi. Mwili wake ulisindikizwa kwa heshima na taadhima zote na kuzikwa jirani na Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika mji wa Najaf nchini Iraq.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, basi hadi tutakapokutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki juma lijalo. Ninakuageni nikikutakieni kila la kheri maishani.

Wassalaamuu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaaatuh

Tags