Jul 19, 2021 21:55 UTC
  • Jumanne tarehe 20 Julai mwaka 2021

Leo ni Jumanne tarehe 9 Dhulhija mwaka 1442 Hijria sawa Julai 20 mwaka 2021.

Leo ni siku ya Arafa tarehe 9 Dhil-Hija. Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na mlima wa Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya siku hii mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, husimama katika uwanja wa Arafa na Hadithi nyingine za Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho. Hadithi zinasema kuwa Mwenyezi Mungu SW ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahala pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hija na ameweka meza na karamu yake pembeni ya mlima wa Jabalur Rahma. Ni vyema kukumbusha kuwa magharibi ya siku hii ya leo mahujaji wanaondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hija.

Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita, Muslim bin Aqil, binamu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS aliuawa shahidi mjini Kufa Iraq. Alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa na wacha Mungu katika zama zake. Alielekea Kufa, Iraq akiwa na lengo la kwenda kutathmini ni kwa kiwango gani watu wa mji huo walikuwa wakimtii Imam Hussen, baada ya watu wa mji huo kumwandikia maelfu ya barua Imam huyo wakimuomba aende mjini humo na kwamba wako tayari kumuunga mkono katika harakati yake dhidi utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya. Watu wa Kufa walimsaliti Muslim bin Aqil baada ya kuhadaika kwa hila na uongo wa Ubeidullah bin Ziyad, mtawala wa wakati huo wa Kufa na wakamuacha Muslim bin Aqiil peke yake.

Mahali liliko kaburi la Muslim bin Aqil, Kufa nchini Iraq

Miaka 894 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alifariki dunia Fadhlu bin Hassan Tabarsi mashuhuri kwa lakabu ya Aminul Islam, alimu, mfasiri na mpokezi mkubwa wa hadithi katika ulimwengu wa Kiislamu. Alikuwa mwanachuoni mkubwa na aliyeheshimiwa na akthari ya madhehebu ya Kiislamu katika zama hizo. Athari na kumbukumbu muhimu kabisa ya alimu huyo ni tafsiri ya Qur'ani iitwayo Maj'maul Bayan. Sheikh Tabarsi alitokea kuwa mashuhuri baada ya kuandika tafsiri nyingine ya Qur'ani aliyoiita Jawamiul Jam'i. Tafsiri hiyo imekuwa na itibari kwa wanazuoni wengi kutokana na umakini katika kubainisha sababu za kushushwa aya pamoja na tarjumi yake. Msomi huyo ameandika vitabu vingine vingi kama "Haqaiqul Umur", "Al Shawahid" na "Tajul Mawaliid".

Tafsiri ya Majmau'l Bayan

Miaka 211 iliyopita katika siku kama ya leo, uhuru wa Colombia ulitangazwa rasmi. Colombia iligunduliwa mwishoni mwa karne ya 15 Miladia na Wahispania na kuanza kukoloniwa. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 18 Miladia, harakati za kupigania uhuru za wananchi wa nchi hiyo ziliongezeka na hatimaye harakati hizo kuzaa matunda katika siku kama ya leo. Hatua ya Napoleon Bonaparte ya kuikalia kwa mabavu Uhispania, ilizipatia fursa nzuri nchi makoloni ya Uhispania ikiwemo Colombia kuzidisha mapambano ya ukombozi.

Bendera ya Colombia

Katika siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, Georg Friedrich Bernhard Riemann, mwanahisabati wa Kijerumani aliaga dunia baada ya kuugua maradhi ya kifua kikuu. Georg Friedrich alizaliwa mwaka 1826 katika mji wa Hanover nchini Ujerumani na baada ya kumaliza masomo yake ya awali aliendelea na masomo ya hisabati. Alipofikisha umri wa miaka 28 Bernard Riemann alikuwa tayari ni mhadhiri wa Chuo Kikuu katika uwanja huo wa hisabati. 

Georg Friedrich Bernhard Riemann

Miaka 84 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Guglielmo Marconi mvumbuzi wa radio wa Kiitalia akiwa na umri wa miaka 63. Guglielmo alizaliwa mwaka 1874 huku akiwa mtoto wa mfanyabiashara mmoja wa Kiitalia. Marconi alipenda sana kujifunza masuala ya ufundi na sanaa tangu akiwa kijana  mdogo ambapo alianza utafiti wa mawimbi ya sauti. Marconi hatimaye alifanikiwa kuvumbua radio baada ya utafiti wake huo na baadaye akaikamilisha bila ya kutumia waya.

Guglielmo Marconi

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika mwezini. Katika siku hiyo wanaanga wa Kimarekani Neil Armstrong na Edwin Aldrin walitumia chombo cha kusafiria katika anga za mbali kwa jina la Apolo- 11 na kufika mwezini na baadaye wakarejea duniani huku wakiwa na sampuli za mawe na udongo walizokuja nazo katika safari hiyo. Kwa utaratibu huo juhudi kubwa za mwanadamu zilizokuwa zikifanywa kwa muda mrefu kwa lengo la kufikia mwezini zikawa zimezaa matunda.

Neil Armstrong

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, wanajeshi wa Uturuki walivamia na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Cyprus, mashariki mwa kisiwa hicho. Tangu kale Waturuki na Wagiriki wa Cyprus walikuwa wakizozana juu ya namna gani pande mbili hizo zigawane mamlaka ya nchi hiyo.

Bendera ya Cyprus