Aug 05, 2021 02:30 UTC
  • Alkhamisi tarehe 5 Agosti 2021

Leo ni tarehe 25 Dhulhija 1442 Hijria sawa na tarehe 5 Agosti Agosti mwka 2021.

Tarehe 25 Dhulhija inasadifiana na siku ya kuteremshwa Suratu Dahr ambayo inawahusu Imam Ali bin Abi Twalib, mkewe Bibi Fatimatu Zahra na watoto wao Hassan na Hussein (as). Baada ya watukufu hao kuweka nadhiri ya kufunga swaumu siku tatu kwa ajili ya kukidhiwa haja zao na kuanza kutekeleza nadhiri hiyo, katika siku zote tatu za swaumu masikini, yatima na fakiri walikwenda nyumbani kwa Imam Ali (as) na kuomba chakula. Watukufu hao walitoa chakula chao kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya futari na kuwapa wahitaji hao kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Hali hiyo iliendelea kwa siku tatu za kutimiza nadhiri ya swaumu na wakati huo ndipo iliporetemshwa Suratu Dahr ikipongeza na kubakisha hai tukio hilo.

Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita alifariki dunia Friedrich Engels mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani. Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani yaani Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomonisti iliyotangazwa na vyama vya kikomonisti katika mkutano wao wa kwanza mnamo mwaka 1848. Baada ya Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kujitokeza nadharia ya ukomonisti.

Friedrich Engels

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Burkina Faso ilipata uhuru. Nchi hiyo ilikoloniwa na Ufaransa kuanzia katikati mwa karne 19. Burkina Faso ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Upper Volta, ilijitangazia mamlaka ya kujiendeshea mambo yake ya ndani mwaka 1958 baada ya kutangazwa mfumo wa jamhuri lakini ilibakia kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ufaransa. Miaka miwili baadaye katika siku kama hii ya leo Burkina Faso ilipata uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Mwaka 1984 jina la Upper Volta lilibadilishwa rasmi na kuwa Burkina Faso.

Bendera ya Burkina Faso

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, kulitiwa saini mkataba wa kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia kati ya Marekani, Urusi ya zamani na Uingereza. Baada ya kuanza kipindi cha Vita Baridi, ulimwengu ulikaribia kutumbukia katika vita vikubwa vya maangamizi kutokana na kuanza majaribio ya nyuklia na utengenezaji wa makombora yanayovuka mabara na yenye vichwa vya silaha za nyuklia. Suala la Cuba na kupelekwa huko makombora ya Urusi liliufanya mgogoro huo ufikie katika kilele. Baada ya kusainiwa mkataba huo anga ya kimataifa ilitulia kidogo na kukaanza mazungumzo kwa ajili ya kusimamisha majaribio ya silaha za nyuklia. Kuanzia Oktoba mwaka 1958 Marekani, Urusi na Uingereza zilitilia maanani suala la kusitisha majaribio ya silaha hizo japokuwa ziliendelea kufanya majaribio hayo. Hatimaye na baada ya mazungumzo mapana, nchi hizo tatu zilifikia makubaliano ya kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia ambayo yalitiwa saini tarehe 5 Agosti mwaka 1963.

Majaribio ya silaha za nyuklia

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Mordad 1367 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Allamah Sayyid A'ref Hussein Husseini, mwanachuo mashuhuri na mwanamapambano wa Pakistan katika mji wa Peshawar, kaskazini mwa nchi hiyo. Sayyid A'ref Husseini baada ya kupata elimu ya kidini nchini Pakistan, alifunga safari na kuelekea katika nchi za Iraq na Iran kwa shabaha ya kuongeza maarifa ya kidini. Wakati  wa kutokea  harakati za mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Shah, Allamah A'ref Husseini alikuwa hapa nchini na kuwa bega kwa bega na wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, jambo ambalo liliukasirisha utawala wa Shah na kuamua kumfukuza nchini.

Allamah Sayyid A'ref Hussein Husseini

Na siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC walipasisha Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu katika mkutano  wa 19 wa mawaziri hao uliofanyika Cairo, mji mkuu wa Misri. Kwa mnasaba huo siku hiyo imepewa jina la 'Siku ya Haki za Binadamu za Kiislamu na Utukufu wa Mwanadamu.' Tangazo hilo lina utangulizi na vipengee 25. Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu lilipasishwa baada ya nchi za Kiislamu kukosoa Tangazo la Haki za Binadamu lililopasishwa mwaka 1948 katika Umoja wa Mataifa ambalo lilibuniwa kwa misingi ya fikra za kiliberali za nchi za Magharibi na baadhi ya vipengee vyake vinapingana na mafundisho ya Kiislamu. Sifa kuu inayotofautisha Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu na lile la Umoja wa Mataifa ni kutilia maanani haki za kiroho na kimaanawi za maisha ya mwanadamu kwa mujibu wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu.

Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu

 

Tags