Ijumaa ,13 Agosti, 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 4 Mfunguo Nne Muharram 1443 Hijria sawa na Agosti 13 mwaka 2021.
Siku kama ya leo, miaka 1382 iliyopita, Ubaidullah bin Ziyad, mtawala dhalimu na fasiki wa mji wa Kufa, Iraq alitoa hotuba katika msikiti wa mji huo. Katika hotuba hiyo, Ibn Ziyad alitoa vitisho vikali dhidi ya wafuasi wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw) akiwataka wasimsaidie mtukufu huyo katika ardhi ya Karbala na kwamba atamuua mtu yeyote ambaye ataasi amri hiyo. Kwa kutumia fatwa ya hila iliyotolewa na Shuraihul-Qadhi ya kuhalalisha damu ya Imam Hussein (as), Ibn Ziyad akafunga njia zote za kuingia na kutoka mji wa Kufa huku akitoa fedha kwa wakazi wa mji huo kwa ajili ya kwenda kupambana na mjukuu huyo wa Mtume huko Karbala tukio lililomalizika kwa kuuawa Imam Hussein na watu wa familia ya Mtume (saw).

Siku kama ya leo miaka 958 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim Muhammad Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Naqiya, malenga, mwandishi na fasihi mkubwa wa mjini Baghdad, Iraq. Umahiri aliokuwa nao Ibn Naqiya, ndio uliofanya kuwa mashuhuri ambapo hata wataalamu wa mashairi waliyatumia mashairi yake. Kitabu cha ‘Maqaamaat’ ni moja ya athari zinazonasibishwa kwa malenga huyo. Katika kitabu hicho Ibn Naqiya, alizungumzia maovu ya kijamii kupitia hekaya na tenzi. Athari nyingine inayonasibishwa kwa msomi huyo wa Kiislamu, ni kitabu kinachoitwa ‘Al-Jamaan fi Tashbiihaatil-Qur’an’ ambayo ni tafsiri nyepesi ya Qur’an Tukufu. Katika tafsiri hiyo Ibn Naqiya amefafanua aya 226.

Siku kama ya leo miaka 158 iliyopita aliaga dunia Frederick Eugene Delacroix, mchoraji maarufu wa Ufaransa. Eugene Delacroix alirithi kipaji cha sanaa ya uchoraji kutoka kwa mama yake. Baada ya kupoteza wazazi wake wawili akiwa kijana mdogo na kujikuta akiishi maisha magumu sana ya umasikini, aliamua kufanya juhudi kubwa katika kujiendeleza na fani yake uchoraji. Baadaye alianza kufanya maonyesho ya sanaa hiyo katika ukumbi wa jiji la Paris. Katika kipindi hicho baadhi ya watu walikuwa wakimfanyia maskhara na kumkebehi, hata hivyo hakuvunjika moyo na hatimaye kazi zake zilikuwa na taathira. Alipata umashuhuri katika kipindi kifupi na kazi zake zikapokewa sana katika jamii.

Siku kama ya leo miaka 122, yaani tarehe 13 Agosti miaka 115 iliyopita, alizaliwa Alfred Hitchcock mtengeneza filamu mashuhuri wa Kiingereza. Alionesha kazi yake ya kwanza mwaka 1920 na baadaye akaanza kujihusisha na uongozaji filamu. Filamu zake za kuogopesha na za kusisimua zilikuwa mashuhuri mno katika zama hizo. Filamu hizo zilimfanya awe mashuhuri kwa jina la the Master of Suspense. Miongoni mwa filamu zake ni The Man Who Knew Too Much na Young and Innocent. Alfred Hitchcock aliaga dunia tarehe 28 Aprili 1980.

Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, aliaga dunia Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko nchini Italia, akiwa na umri wa miaka 90. Nightingale alizaliwa tarehe 12 Mei 1820 nchini Italia. Aliishi kipindi kirefu cha ujana wake nchini Uingereza. Akiwa kijana alifanya juhudi kubwa katika kuwasaidia watu, suala ambalo alilipa umuhimu mkubwa kuliko kitu kingine chochote na hatimaye alisabilia maisha yake kwa amjili ya kuuguza wagonjwa. Bi, Florence Nightingale alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya ''Mwanamke Mwenye Taa Mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku. Alifanya juhudi kubwa pia kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi nchini Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi bila kuchoka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba alikuwa kipofu mwishoni mwa umri wake na hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910.

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijikomboa na kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Ilikuwa katikati ya karne ya 19 wakati nchi hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo kabla kwa jina la Ubangi-Shari, ilipounganishwa na makoloni ya Ufaransa barani Afrika. Hata hivyo mwaka 1958, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijipatia mamlaka ya ndani na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1960, ikajikomboa na kupata uhuru kamili.