Aug 21, 2021 02:30 UTC
  • Jumamosi, 21 Agosti, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 12 Mfunguo Nne Muharram 1443 Hijria mwafaka na tarehe 21 Agosti 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Muharram mwaka 61 Hijria msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na wanawake na watoto wa mashahidi wa Karbala, uliwasili katika mji wa Kufa, nchini Iraq. Kiongozi wa msafara huo alikuwa Bibi Zainab (as) dada wa Imam Hussein bin Ali (as) pamoja na Imam Ali bin Hussein Sajjad (as), mtoto wa Imam Hussein (as). Imam Sajjad na Bibi Zaynab (as) walitekeleza majukumu yao kwa kufikisha ujumbe wa Imam Hussein kwa jamii ya Waislamu. ***

Msafara wa mateka wa Karbala

 

Katika siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita sawa na tarehe 12 Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Hijria, miili ya mashahidi wa Karbala ukiwemo mwili mtukufu wa mjukuu wa Mtume (saw) Imam Hussein AS ilizikwa ikiwa ni siku mbili baada ya kuuawa shahidi na kuachwa jangwani. Mashahidi wa Karbala walizikwa na watu wa kabila la Bani Asad. Mwili wa Imam Hussein na mashahidi wote wa Karbala ilibakia kwa siku mbili bila ya kuzikwa kwani hakuna mtu aliyekuwa na ujasiri wa kuzika miili hiyo kutokana na hofu ya utawala dhalimu wa Bani Umayyah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo wanawake wa kabila la Bani Asad waliwahamasisha wanaume wao kuzika miili hiyo mitakatifu ya wajukuu wa Mtume na masahaba wa Imam Hussein (as). ***

Mahala walipozikwa mashahidi wa Karbala

 

Siku kama ya leo miaka 1348 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Imam Ali Zainul Abidin maarufu kwa lakabu ya Sajjad mwana wa Imam Hussein (as) na mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu S.A.W, aliuawa shahidi. Imam Zainul Abidin alizaliwa mwaka 38 Hijria huko katika mji wa Madina. Mtukufu huyo aliishi katika zama ambapo watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu walikuwa wakikabiliwa na masaibu mengi. Imam Sajjad A.S ambaye alikuwa mgonjwa wakati wa tukio la Karbala, baada ya harakati adhimu ya Imam Hussein, alibeba jukumu kubwa la kueneza ujumbe wa mapambano hayo na kuendeleza njia ya baba yake. ***

Kumbukumbu ya kuuawashahidi Imam Zeinul-Abidina (as)

 

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, iliasisiwa The Central Treaty Organization ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Cento na kuchukua nafasi ya mkataba wa Baghdad. Taasisi hiyo iliundwa na Iran, Uturuki, Pakistan na Uingereza mjini Ankara Uturuki. Pamoja na kuwa Marekani haikuwa mwanachama rasmi wa Taasisi ya Cento na ilishiriki kwenye vikao vya jumuiya hiyo kama mtazamaji tu, lakini ilikuwa na nafasi kuu katika maamuzi yote ya taasisi hiyo. The Central Treaty Organization ilivunjika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kujiondoa nchi hiyo katika mkataba huo mwaka 1979. ***

Mkataba wa Cento

 

Tarehe 21 Agosti mwaka 1965 yaani katika siku kama hii ya leo miaka 56 iliyopita Wamarekani wenye asili ya Afrika katika mji wa Alabama walifanya maandamano wakitaka kutekelezwa sheria ya haki ya kupiga kura. Maandamano hayo yalizidisha harakati ya vuguvugu la kupigania haki za kijamii za Wamarekani weusi. Harakati hiyo ilianza mwaka 1955 kwa lengo la kupigania usawa kati ya Wamarekani weusi na wazungu na ilimalizika mwaka 1968 baada ya kupasishwa sheria ya haki za kiraia. ***

 

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, inayosadifiana na 21 Agosti 1969 Miladia, Masjidul Aqsa Kibla cha Kwanza cha Waislamu, kilichomwa moto na Wazayuni. Katika tukio hilo, eneo hilo takatifu na la kihistoria liliharibika vibaya sana. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa, kitendo hicho kilifanywa na mtalii wa Kiaustralia. Utawala huo wa Kizayuni ulitayarisha mahakama ya kimaonyesho tu mjini Tel Aviv na kuchukua uamuzi wa kumuachilia huru mhalifu huyo kwa madai kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili. Baada ya kutokea kitendo hicho, nchi za Kiislamu zilikutana na kuamua kuunda Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC). ***

Kuchomwa na Wazayuni msikiti waal-Aqswa

 

Tarehe 21 Agosti inatambuliwa kama siku ya kimataifa ya msikiti. Upasishwaji wa siku hii ulijiri mwaka 1382 Hijiria Shamsia, sawa na tarehe 22 Agosti mwaka 2003 Miladia katika mkutano uliofanyika mjini hapa Tehran na kwa pendekezo la Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu la nchini Iran sanjari na kupitishwa na Wizara za Mashauri ya Kigeni za nchi za Kiislamu. Kikao hicho kilifanyika kwa mnasaba wa wiki ya kumbukumbu ya kuchomwa moto msikiti wa Al-Aqsa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel tarehe 21 Agosti mwaka 1969. Aidha katika kikao hicho nchi za Kiislamu zilitakiwa kutoa himaya kwa misikiti kama mahala patakatifu sanjari na kuienzi sehemu hiyo. ***

Siku ya Kimataifa ya Msikiti

 

Na miaka 30 iliyopita katika siku kama hii ya leo Latvia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani ilijitangazia uhuru. Latvia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 Miladia kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Latvia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii. ***

Latvia