Ijumaa tarehe 27 Agosti 2021
Leo ni Ijumaa tarehe 18 Muharram 1443 Hijria sawa na Agosti 27 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 386 iliyopita, alifariki dunia Lope de Vega, mwandishi mkubwa wa Uhispania. Vega alizaliwa mwaka 1562 Miladia na akiwa kijana mdogo alionekana kuwa mwenye harakati nyingi na mwenye kipawa kikubwa cha akili huku akianza pia kusoma mashairi. Akiwa na umri wa miaka 14 alijiunga na shule ya msingi na sekondari ya kidini ambapo baada ya kuhitimu masomo yake katika chuo kikuu, alijiunga na jeshi la kujitolea. Taratibu akaanza kuonyesha kipawa chake katika michezo ya kuigiza na masuala mengine na hivyo kuwavutia watu wengi. Lope de Vega anajulikana kuwa mwanzilishi wa michezo ya kuigiza kitaifa nchini Uhispani.
Siku kama ya leo miaka 251 iliyopita, alizaliwa Georg Wilhelm Friedrich Hegel mwanafalsafa mkubwa wa Ujerumani. Licha ya msomi huyo kufundisha katika vyuo mbalimbali na kuandika vitabu tofauti, lakini bado alikuwa masikini. Kufuatia uvamizi wa jeshi la Napoleon dhidi ya Ujerumani mwaka 1806, Hegel alivutiwa na shakhsia ya kamanda huyo Kifaransa. Alibainisha hatua za historia na kuamiani kuwa, muelekeo wa harakati ya kihistoria huainishwa na Mwenyezi Mungu na kwamba hata malengo ya historia ni hivyo. Katika kubainisha itikadi yake, Georg Wilhelm Friedrich Hegel aliandika vitabu kadhaa katika uwanja huo. Hegel alifariki dunia mwaka 1831 Miladia.
Siku kama ya leo, miaka 150 iliyopita alizaliwa Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli, alimu mkubwa na mtaalamu wa fiqhi mjini Kabul, Afghanistan. Akiwa kijana mdogo Allamah Sardor Kabuli alipata kusoma kwa wasomi wakubwa wa enzi hizo kama vile, Mirza Hussein Nuri na Sayyid Swafiyyud-Din Hassan bin Hadi Kadhimi, sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwa maulama na maraajii watajika kama vile, Sayyid Hassan Sadr naHaji Sheikh Abbas Qumi, ambapo pia alipata ijaza (idhini) ya kunakili na kuandika riwaya na hadithi. Mwaka 1310 Hijiria, Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli alielekea mjini Kermanshah, Iran na kujishughulisha na ufundishaji kwa wakazi wa mji huo sanjari na kuandika vitabu kadhaa. Aidha msomi huyo alipata kusomea lugha kadhaa za dunia, kama vile Kiarabu, Kingereza, Kiebrania na Urdu. Kitabu cha ‘Tarjama ya Injili ya Barnaba’ na ‘Hadithi 40 katika fadhila za Amirul-Muuminin’ ni miongoni mwa athari za msomi huyo. Allamah Haidar Qali Sardor Kabuli alifariki dunia mwaka 1372 Hijiria, akiwa na umri wa miaka 79 na kuzikwa mjini Najaf, Iraq.
Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Hadi mwisho wa uhai wake msomi huyo alisalia mjini Tehran na baada ya kufariki dunia akazikwa mjini Qum.
Siku kama ya leo tarehe 5 Shahrivar nchini Iran ni siku ya kumkumbuka Muhammad bin Zakaria Razi, msomi mtajika wa Kiislamu. Muhammad bin Zakaria Razi alizaliwa mwaka 251 hijria katika mji wa Rei nchini Iran na alianza kujifunza kemia na fizikia akiwa bado kijana. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadaye Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia. Msomi huyo wa Kiislamu Muirani alikuwa shakhsia wa kwanza kuvumbua alkoholi.
Muhammad bin Zakaria Razi ameandika vitabu 56 vya tiba, 33 vya sayansi ya asili, 17 vya falsafa, 14 vya teolojia, 22 vya kemia na makumi ya vita katika nyanja mbalimbali. Msomi huyo wa Kiislamu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 60 na alizikwa katika mji wa Rei ambao hii leo uko kusini mwa Tehran.
Tarehe 27 Agosti mwaka 1896, kulitokea vita vya muda mfupi zaidi duniani visiwani Zanzibar. Jengo la Kihistoria mjini Unguja linalojulikana kwa jina la Beit al-Ajaib lililojengwa na Sultan Barghash bin Said huko Forodhani kisiwani Unguja, lilishambuliwa kwa mizinga ya manowari za Uingereza. Hatua hiyo ilikuja kufuatia ugomvi uliozuka baina ya wana wawili wa Sultani wa Zanzibar. Watoto hao walijulikana kwa majina ya Said Barghash Khalid na Said Hamud bin Muhammed na ugomvi wao ulihusiana na utawala na nani anapaswa kurithi kiti cha ufalme. Vita hivyo vilidumu kwa dakika 45 tu na kuwa vita vifupi zaidi duniani.
Tarehe tano Shahrivar miaka 43 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, mwanzo wa kalenda ya Iran ulirejeshwa tena katika mwaka wa Hijria Shamsia kutoka mwanzo wa tarehe wa Kifalme. Katika miaka ya kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu utawala wa kidikteta wa Pahlavi ambao ulitambua mafundisho ya Uislamu kuwa ni kinyume na maslahi yake, ulikuwa ukifanya njama za kukabiliana na Uislamu kwa kutumia utajiri na turathi ya kihistoria ya Iran. Katika mkondo huo bunge la kimaonyesho la utawala wa Kipahlavi lilipasisha sheria iliyobadilisha mwanzo wa kalenda ya Iran kutoka mwaka wa Hijra ya Mtume (saw) na kuifanya kuwa tarehe ya kuvikwa taji la Mfalme Kurosh wa silsila ya Khahamaneshi. Hatua hiyo ilikabiliwa na hasira na malalamiko makubwa ya Imam Ruhullah Khomeini na wananchi Waislamu wa Iran. Kubadilishwa huko kwa mwaka wa Hijria na kufuata mwaka wa Kifalme nchini hakukudumu kwa zaidi ya kipindi cha miaka miwili na nusu na utawala wa Shah uliokuwa ukikabiliwa na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ulilazimika kutambua tena mwaka wa Hijra ya Mtume (saw) kutoka Makka kwenda Madina kuwa ndiyo mwanzo wa kalenda nchini Iran.

Miaka 31 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo alifariki dunia Ali Akbar Kaveh, mwalimu mkubwa wa sanaa ya kaligrafia ya hati za Kifarsi. Mtaalamu huyu alizaliwa mwaka 1271 Hijria mjini Shiraz, moja ya miji ya kusini mwa Iran na kuanza kujihusisha na masuala ya karigrafia. Baada ya hapo Ali Akbar Kaveh alipata kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo kama vile Mirza Twahir Katib, Homayun Hamedani na Imad Al Katib Seifi Qazwini na hatimaye akawa hodari mkubwa katika sanaa ya kaligrafia.
Na katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, yaani tarehe 27 Agosti mwaka 1991, nchi ya Moldova iliyoko mashariki mwa Ulaya ilipata uhuru. Kwa mujibu wa kumbukumbu za historia nchi hiyo ilikaliwa kwa mabavu na tawala, kaumu na nchi mbalimbali zikiwemo, Ukraine, Russia, Romania na utawala wa Othmania. Baada ya mapinduzi ya kikomunisti nchini Russia, Moldova iliungana na Romania. Mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Moldova ilikaliwa kwa mabavu na Urusi. Hata hivyo baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti, nchi hiyo ikajikomboa na kupata uhuru.
