Jumapili tarehe 29 Agosti 2021
Leo ni Jumapili tarehe 20 Muharram 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 29 Agosti 2021.
Siku kama ya leo miaka 175 iliyopita, Mirza Taqi Khan Amir Kabir aliuzuliwa cheo cha Kansela. Alikuwa mmoja wa wanasiasa wa Iran katika kipindi cha utawala wa Qajar. Kipindi fulani alikuwa Kansela wa Naser al-Din Shah mfalme wa wakati huo wa Iran. Amir Kabir alikuwa mtu huru, mwenye imani, muenezaji wa elimu na mwenye kupenda utamaduni na anahesabiwa kuwa mmoja wa waasisi wa marekebisho na waenezaji wa fikra bora katika uwanja wa ufundishaji, malezi na utamaduni nchini Iran. Amir Kabir alifanya juhudi kubwa katika njia ya mafanikio ya wananchi wa Iran na katika kipindi alichokuwa Kansela alitoa huduma na kufanya marekebisho mengi. Aidha alifanya juhudi kubwa za kuzuia uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Iran.
Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita Urusi ya zamani ilifanya majaribio ya siri ya bomu lake la kwanza la nyuklia. Kwa utaratibu huo Urusi ikawa nchi ya pili yenye mabomu ya nyuklia baada ya Marekani suala ambalo liliibua mlingano wa nguvu kati ya nchi hizo mbili ambao ulipewa jina la “Mlingano wa Hofu.” Kwani katika hali hiyo kila mmoja wao aliogopa kutumia silaha hizo za nyuklia dhidi ya mwenzake kwa kuogopa kushambuliwa pia na silaha kama hizo. Tangu wakati huo Marekani na Urusi ya zamani ziliingia katika vita vya kipropaganda. Vita hivyo vilipewa jina la "Vita Baridi" au Cold War kwa kimombo. Vita hivyo vya kati ya kambi ya Mashariki na Magharibi viliendelea hadi wakati wa kusambaratika Urusi ya zamani mwaka 1991.
Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo msanii na mchoraji maarufu wa katuni wa Palestina Naji al Ali ambaye alikuwa ameshambuliwa na maajenti wa Shirika la Ujasusi la Israel MOSSAD huko London, Uingereza alifariki dunia baada ya siku 38 za kuwa katika hali ya kupoteza fahamu. Al-Ali alizaliwa mwaka 1937 huko Palestina na alilazimika kukimbia nchi yake akiwa bado mtoto akiwa pamoja na familia yake na kuishi katika kambi ya wakimbizi ya Ain al-Halwa kusini mwa Lebanon kutokana na ukatili na unyama wa Wazayuni. Alishuhudia kwa karibu mashaka na masaibu ya Wapalestina na akaamua kutumia kipawa chake cha usanii kufichua unyama na ukatili wa utawala ghasibu wa Israel kwa kutumia sanaa ya uchoraji vibonzo. Hatimaye magaidi wa Shirika la Ujasusi la Israel MOSSAD walimshambulia na kumuua mwanamapambano huyo akiwa njiani kuelekea ofisini kwake mjini London. Miezi sita baada ya kufariki kwake dunia Jumuiya ya Kimataifa ya Wachapishaji ilimtunuku msanii huyo tuzo ya Kalamu ya Dhahabu ya Uhuru.
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Shahrivar 1369 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar-ashi Najafi mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96. Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, usul fiqihi, Hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhmein na Najaf Iraq. Moja ya athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar-ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko mjini Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake duniani.