Aug 31, 2021 22:17 UTC
  • Jumatano tarehe Mosi Septemba 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 23 Muharram 1443 Hijria sawa na tarehe Mosi Oktoba mwaka 2021.

Miaka 847 iliyopita katika siku kama ya leo, ilianza kazi ya kujenga mnara maarufu wa Pisa huko katika mji wa Pisa nchini Italia. Mnara huo ulijengwa kwa ajili ya kuitundika saa juu yake. Hata hivyo mnara huo uliokuwa na urefu wa mita 55 ulipinda kwa karibu mita tano muda mfupi baada ya kuanza kujengwa. Hitilafu hiyo imeufanya mnara huo ujulikane kwa jina la"Mnara Uliopinda wa Pisa." Hadi kufikia sasa mnara huo umefanyiwa marekebisho ya kiwango fulani kufuatia juhudi za wahandisi na wataalamu wa nchi mbalimbali. 

Mnara wa Pisa

Katika siku kama ya leo miaka 234 iliyopita aliaga dunia Allamah Mulla Muhammad Mahdi Naraqi, mwanazuoni na msomi mkubwa wa Kiislamu. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali nchini Iran, msomi huyo mkubwa alielekea Hauza ya Najaf nchini Iraq kwa lengo la kuzidisha elimu ya kidini na alipata elimu kwa walimu mashuhuri wa zama hizo. Baada ya hapo Allamah Mulla Mahdi Naraqi alianza kufanya utafiti, kufundisha na kuandika vitabu. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya Allamah Naraqi ni "Jamiul Sa'adat" na " Anisul Muwahhidin".

Allamah Mulla Muhammad Mahdi Naraqi

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulioambatana na uharibifu mkubwa na kuua idadi kubwa ya watu, ulitokea nchini Japan. Zilzala hiyo iliyokuwa na ukubwa wa 8.3 kwa kipimo cha Rishta iliua watu zaidi ya laki moja na 40 elfu. Mtetemeko huo uliyakumba hata baadhi ya maeneo ya miji ya Tokyo na Yokohama. Mbali na hasara kubwa zilizosababishwa na mtetemeko huo, idadi kubwa ya Wajapani pia walikosa makazi yao na nyumba nyingi ziliteketea kwa moto.

Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, Vita vya Pili vya Dunia vilianza baada ya jeshi la Ujerumani ya Kinazi kuanzisha mashambulizo dhidi ya Poland. Adolf Hitler alianza kuliandaa jeshi lenye nguvu wakati alipokuwa madarakani huko Ujerumani kwa kutumia vibaya hadhi yake na hisia za ubaguzi na utaifa wa wananchi wa nchi hiyo, ambao walikuwa wamefedheheka sana baada ya kushindwa vibaya katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Katika kipindi kifupi, Hitler alifanikiwa kuikalia kwa mabavu sehemu kubwa ya ardhi za Ulaya na kaskazini mwa Afrika. 

Kuanza Vita vya Pili vya Dunia

Siku kama leo miaka 52 iliyopita, yaani sawa na tarehe Mosi Septemba  mwaka 1961, ulifanyika mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya Isiyofungamana na Upande Wowote NAM huko Belgrade mji mkuu wa Yugoslavia ya zamani kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 25 duniani. Jumuiya ya NAM iliasisiwa lengo kuu likiwa ni kuziunga mkono nchi za ulimwengu wa tatu mkabala na kambi za Mashariki na Magharibi. Masharti makuu ya kujiunga na jumuiya hiyo, ni kutokuwa mwanachama rasmi katika muungano unaofungamana na madola makubwa ya Mashariki na Magharibi.

Na miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo, kulifanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Libya yaliyomfikisha madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Kabla ya mapinduzi hayo, Libya ilikuwa ikiongozwa na utawala wa Mfalme Idris wa Kwanza. Wakati mfalme Idris alipoelekea nchini Uturuki kwa ajili ya matibabu, kundi moja la wanajeshi ambalo liliongozwa na Kanali Muammar Gaddafi lilifanya mapinduzi na kumvua madaraka mfalme huyo sambamba na kutangaza utawala wa kisoshalisti nchini Libya. Baada ya hapo Libya ilifuata siasa za Urusi ya zamani na kutaifisha sekta ya mafuta na benki. Baada ya kusambaratika Urusi ya zamani, Muammar Gaddafi alianza kufuata siasa za Wamagharibi na kuwakabidhi viwanda vya mafuta vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, hali inayodaiwa kuchangia hasira za wananchi. Muammar Gaddafi aliondolewa madarakani na kuuawa kufuatia mapinduzi ya tarehe 21 mwezi Agosti 2011.

Muammar Gaddafi

Na siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, sawa na tarehe 23 Muharram 1427 Hijria Haram mbili takatifu za Maimamu al Hadi na Hassan al-Askari katika mji wa Samarra nchini Iraq, ziliharibiwa vibaya kwenye mashambulizi kadhaa ya miripuko ya mabomu yaliyofanywa na magaidi wa kundi la al Qaida na kusababisha hasara kubwa za mali na watu. Maimamu hao ni wajukuu wa  Mtume Muhammad SAW, na walikuwa na nafasi kubwa ya kielimu na uchamungu katika zama zao. Kitendo cha kuharibiwa eneo hilo kiliwakasirisha mno Waislamu duniani hususan wafuasi wa Ahlul Bait wa Mtume (saw). Kabla ya mashambulizi hayo, ulinzi wa haramu hizo ulikuwa mikononi mwa majeshi vamizi ya Marekani. Shambulio hilo lilifanyika kwa lengo la kuzusha ufa na hitilafu kati ya safu za Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni nchini Iraq.

Haram mbili takatifu za Maimamu al Hadi na Hassan al-Askari