Sep 04, 2021 22:22 UTC
  • Jumapili tarehe 5 Septemba 2021

Leo ni Tarehe 27 Muharram 1443 Hijria sawa na Septemba 5 mwaka 2021.

Siku kama hii ya leo miaka 164 iliyopita Auguste Comte mwanafalsafa na mwanahisabati wa Kifaransa alifariki dunia. Comte alizaliwa mwaka 1798. Alishirikiana kwa muda fulani huko Paris na Henri de Saint Simon, mwanafalsafa mashuhuri wa zama hizo na baadaye Comte alianza kufundisha. Auguste Comte alikuwa mwasisi wa mfumo wa elimu jamii. Comte ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha The Positive Philosophy of Auguste Comte.

Auguste Comte

Miaka 134 iliyopita mwafaka na tarehe 5 mwezi Septemba mwaka 1887, mto mkubwa wa Huang He huko China ulianza kufurika maji. Mafuriko hayo makubwa yalisababishwa na kujaa maji katika mto huo kwa zaidi ya mwezi mmoja. Zaidi ya watu laki tisa walipoteza maisha katika mafuriko hayo na taathira zake mbaya. Aidha miji kadhaa, mamia ya vijiji na mashamba mengi yaliharibiwa baada ya kukumbwa na mafuriko ya mto Huang He huko China.

Miaka 116 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 5 Septemba mwaka 1905, Mkataba wa Portsmouth ulitiwa saini na hivyo kuhitimisha vita kati ya Russia na Japan. Februari 8 mwaka 1904, vikosi vya majeshi ya Japan vilifanya mashambulio ya kushtukiza dhidi ya meli za kivita za Russia na kuyadhibiti maeneo ya Manchuria ambayo yalikuwa chini ya mamlaka ya Russia. Russia ilipata vipigo mfululizo katika vita hivyo. Hatimaye kwa upatanishi wa Marekani, katika siku kama ya leo pande mbili zilitia saini mkataba wa Portsmouth na huo ukawa mwisho wa vita kati ya Japan na Russia.

Mkataba wa Portsmouth

Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita Ayatullah Ali Quddusi Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mapinduzi ya Kislamu nchini Iran aliuawa shahidi katika mlipuko wa bomu uliotekelezwa na kundi la kigaidi la MKO. Shahidi Quddusi alipata elimu kwa wasomi kama Ayatullah Burujerdi, Allama Tabatabai na Imam Ruhullah Khomeini MA na kufikia daraja ya Ijtihad. Shahidi Quddusi alishiriki vilivyo katika masuala ya kidini na mfano wa wazi wa mchango wake ni kuasisi shule ya mafunzo ya kidini ya Haqqani. Mwaka 1341 Hijria Shamsia alisimama kupambana na utawala dhalimu wa Shah na akatiwa jela kwa kipindi fulani. Ayatullah Quddusi alisabilia miaka ya mwishoni mwa umri wake katika juhudi za kuimarisha mfumo mchanga wakati huo wa Kiislamu hapa nchini na hatimaye aliuawa shahidi na magaidi wa kundi la MKO katika siku kama hii ya leo.

Ayatullah Ali Quddusi

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita inayosadifiana na tarehe 5 Septemba 1993, moja kati ya misikiti mikubwa katika ulimwengu wa Kiislamu ulifunguliwa rasmi huko Casablanca nchini Morocco. Msikiti huo umejengwa kwa mtindo wa kisasa na una minara inayoakisi usanifu majengo wa hali ya juu wa Kiislamu. Eneo la uwanja wa msikiti huo lina uwezo wa kuchukua waumini 75,000. Eneo la ndani la msikiti huo limepambwa kiufundi. Pembeni ya msikiti huo kumejengwa maktaba moja kubwa na Chuo Kikuu cha Kidini. Msikiti huo unahesabiwa kuwa moja kati ya misikiti mikubwa na maridadi sana katika ulimwengu wa Kiislamu.

Msikiti wa Casablanca