Sep 06, 2021 03:50 UTC
  • Jumatatu tarehe 6 Septemba 2021

Leo ni Jumatatu tarehe 28 Muharram 1443 Hijria sawa na na tarehe 6 Septemba 2021.

Katika siku kama ya leo miaka 787 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, mji wa Baghdad uliokuwa makao makuu ya watawala wa Kiabbasi ulitekwa na Hulagu Khan Mongol baada ya kuuawa Mustaasim aliyekuwa mtawala wa mwisho wa utawala wa Bani Abbas. Mauaji ya mtawala huyo yalihitimisha utawala wa kizazi hicho uliotawala sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kislamu kwa kipindi cha miaka 500. Hulagu Khan Mongol hakusita kufanya mauaji na jinai katika uvamizi wake dhidi ya nchi mbalimbali, na baada ya kuteka baadhi ya maeneo ya Iran na kuua watu kwa umati katika maeneo ya mijini na vijijini, aliushambulia mji wa Baghdad na kufanya mauaji ya kinyama ya maelfu ya wakazi wake. Vilevile aliharibu na kuvunja nyumba na majengo muhimu ya mji wa Baghdad. 

Miaka 56 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo jeshi la India lilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Pakistan kufuatia machafuko ya zaidi ya mwezi mmoja katika mipaka ya nchi mbili hizo. Hivyo vilikuwa vita vya pili vikubwa kuwahi kutokea kati ya nchi mbili hizo jirani kuhusiana na eneo la Kashmir. Pakistan na India zilikubaliana kusimamisha mapigano kufuatia upatanishi wa Urusi ya zamani. Viongozi wa nchi mbili hizo hatimaye waliafikiana kuanza mazungumzo tarehe 10 mwezi Juni mwaka 1966 huko Tashkend mji mkuu wa Uzbekistan nchini ya upatanishi wa Waziri Mkuu wa Urusi ya zamani. Japokuwa azimio la Tashkend lilibainisha njia za kumaliza mgogoro wa eneo la Kashmir na namna ya kuboresha uhusiano kati ya New Delhi na Islamabad na pia kupokelewa na nchi mbalimbali duniani, lakini lilishindwa kumaliza hitilafu kati ya India na Pakistan kuhusu umiliki wa eneo la Kashmir. 

Vita vya Kashmir

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita Swaziland ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na kila inapowadia siku kama hii husherekewa kama siku ya taifa. Kuimarika ukoloni wa Ulaya huko kusini mwa Afrika kulisababisha pia Swaziland kukaliwa kwa mabavu. Hatimaye nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika ilipata uhuru mwaka 1968. Hata hivyo utawala wa nchi hiyo umeendelea kuwa wa kifalme kama ilivyokuwa huko nyuma.

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, baada ya kupamba moto harakati za mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah, kulifanyika maandamano makubwa katika maeneo mbalimbali kote nchini. Kwa sababu hiyo utawala wa Shah uliokuwa umepatwa na wasiwasi mkubwa kutokana na harakati hizo za mapinduzi, uliamua kupiga marufuku maandamano ya aina yoyote ile. Wakati huo huo Imam Ruhullah Khomeini MA aliyekuwa uhamishoni huko Najaf nchini Iraq alitoa taarifa akiwataka wananchi wa Iran kudumisha harakati za mapambano. Katika sehemu moja ya taarifa yake kwa wananchi, Imam Khomeini aliyataja maandamano yanayofanywa kwa ajili ya kufikia malengo ya Kiislamu kuwa ni ibada.

Maandamano ya wananchi dhidi ya Shah

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 15 Shahrivari 1361 Hijria Shamsia, kulitokea mlipuko mkubwa katika moja ya barabara zenye msongamano mkubwa wa watu katika mji wa Tehran, Iran. Makumi ya watu waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika tukio hilo. Jinai hiyo ilifanywa na vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqin la MKO. Mlipuko huo ulikuwa mkubwa mno kiasi kwamba, ulisikika katika mji wote wa Tehran. Mlipuko huo ulitekelezwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa dikteta wa wakati huo wa Iraq, Saddam Hussein ambaye jeshi lake lilikuwa limeshindwa vibaya na wanamapambano shupavu wa Iran katika medani ya vita.

Tehran

 

Tags