Sep 08, 2021 02:40 UTC
  • Jumatano tarehe 8 Septemba 2021

Leo ni Jumatano tarehe Mosi Safar 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 8 Septemba 2021.

Siku kama ya leo miaka 1406 iliyopita, awamu ya mwisho ya vita kati ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na Muawiya bin Abi Sufiyan ilianza katika eneo la Siffin kandokando ya Mto Furati (Euphrates) nchini Iraq. Baada ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) kushika hatamu za uongozi Muawiya alikataa kumpa mkono wa utiifu na akaamua kuanzisha vita dhidi ya serikali yake.

Tarehe Mosi Safar miaka 1382 iliyopita, msafara wa familia ya Mtume Muhammad (SAW) ambayo ilichukuliwa mateka katika vita vya Karbala, uliwasili katika mji wa Sham ambao ulikuwa makao makuu ya utawala wa Yazid bin Muawiya. Wakiwa Sham, Ahlul Bait wa Mtume (SAW) hususan Bibi Zainab (as) na Imam Sajjad (as) walitoa hutuba tofauti katika msikiti wa Sham wakifichua maovu ya Yazidi, kiongozi dhalimu wa Bani Umayyah. Vilevile Ahlul Bait wa Mtume (SAW) walifikisha kwa watu ujumbe wa harakati ya mashahidi wa Karbala kwa njia nzuri kiasi kwamba watu wa Sham walielewa ukweli kuhusu jinai za jeshi la Yazid na kuzua hasira dhidi ya mtawala huyo. Hali hiyo ilimfanya Yazidi aliyetoa amri ya kuuawa Imam Hussein (as) na wafuasi wake, akane uhakika huo na kumtwisha lawama hizo Ubaidullah bin Ziyad, aliyekuwa gavana wa mji wa Kufa, Iraq.

Tarehe 8 Septemba ilitangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ujinga. Kujua kusoma na kuandika ni miongoni mwa vielelezo cha ustawi katika jamii ya mwanadamu na ujinga husababisha umaskini na kubakia nyuma kimaendeleo. Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa mkakati wa kupambana na kutojua kusoma na kuandika haukuwa wa kuridhisha katika baadhi ya nchi na hadi sasa idadi kubwa ya watu hawajapata neema hiyo.

Nchini Iran baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu kulifanyika jitihada kubwa za kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika kwa kadiri kwamba Disemba mwaka 1979 Imam Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuasisiwa Harakati ya Kupamgana na Ujinga. Taasisi hiyo imechukua hatua kubwa hapa nchini. 

Miaka 258 iliyopita katika siku kama ya leo,  baada ya mapigano ya muda mrefu na kwa mujibu wa makubaliano ya Paris, Canada iliondoka chini ya udhibiti wa Ufaransa na kudhibitiwa rasmi na Uingereza. Hata hivyo mivutano baina ya Wacanada wenye asili ya Ufaransa na Waingereza waliokuwa wakiishi Canada iliendelea kwa muda mrefu. Licha ya Canada kujitangazia uhuru na mamlaka ya kujitawala mwaka 1867 lakini nchi hiyo inafuata Uingereza katika mfumo wake wa kisiasa. 

Katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, wanajeshi wa Ujerumani ya Kinazi waliuzingira mji wa Leningrad, Saint Petersburg ya sasa. Hata hivyo mji huo haukutekwa na jeshi la Kinazi licha ya matarajio ya Adolf Hitler na makamanda wake. Wakazi wa Leningrad waliendeleza mapambano ya ukombozi hadi Januari mwaka 1944 wakati walipofanikiwa kujiondoa katika mzingiro wa wanajeshi wa Ujerumani.

Leningrad

Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, kulitiwa saini mkataba wa ulinzi wa mataifa ya Asia ya kusini mashariki (SEATO) katika mji mkuu wa Ufilipino, Manila. Mkataba huo ulitiwa saini na nchi za Marekani, Uingereza, Australia, Pakistan, Thailand, Ufaransa, New Zealand na Ufilipino. Kwa mujibu wa mkataba huo, nchi mwanachama itakapokabiliwa na mashambulio ya kijeshi kutoka nje, uasi na vitisho vya ndani, basi nchi wanachama zinapaswa kuisaidia nchi hiyo kijeshi au kwa kutumia wenzo wa vikwazo.

Na miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi wa utawala wa kidikteta wa Pahlavi walishambulia maandamano makubwa ya wananchi wa mji wa Tehran na kuua raia wengi. Wananchi Waislamu wakazi wa Tehran siku hiyo walianza kuandamana tangu asubuhi, hayo yakiwa maandamano ya siku kadhaa mfululizo kuwahi kufanywa na wakazi wa mji wa Tehran dhidi ya utawala wa kibaraka wa Pahlavi. Wakati huo, utawala wa kijeshi ulikuwa umetangazwa katika mji wa Tehran, lakini wananchi Waislamu walipuuza hali hiyo na wakamiminika mitaani wakipiga nara dhidi ya utawala wa Shah. Wakati huo huo, walinzi maalumu wa Shah walifanya mashambulizi na katika muda mfupi wakawaua shahidi wananchi zaidi ya elfu nne wa Tehran waliokuwa wakipigania haki zao.

Tarehe 17 Shahrivar