Jumapili, 12 Septemba, 2021
Leo ni Jumapili tarehe 5 Mfunguo Tano Safar 1443 Hijria sawa na tarehe 12 Septemba 2021 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita Ruqayyah binti mdogo wa Imam Hussein bin Ali (as) alikufa shahidi akiwa huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyya. Ruqayyah ambaye pia anajulikana kwa jina la Fatima binti Hussein (as) alikuwa binti wa mwisho wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kutoka kwa mkewe, Ummu Is’haq binti Twalha. Wanahistoria wanasema mtoto huyo alikuwa na umri wa miaka 3, 4 au 7. Mtoto huyo alikuwa akimpenda sana Imam Hussein na aliandamana naye pamoja na familia yake katika medani ya Karbala. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, ndugu na masahaba wa Imam, Ruqayya alikamatwa mateka na askari wa Yazid akiwa pamoja na watu wengine wa Nyumba ya Mtume na kupelekwa Sham. Huko alikuwa akilia mchana usiku. Wanahistoria wanasema mtawala Yazidi aliamuru kichwa cha Imam Hussein kipelekwe na kutupwa mbele ya binti huyo mdogo ambaye alilia na kuzimia kisha akakata roho. ***

Miaka 124 iliyopita, inayosadifiana na 12 Septemba 1897, Irene Joliot- Curie mtaalamu wa Fizikia na Kemia wa Ufaransa, alizaliwa katika mji wa Paris. Baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu, Irene Joliot- Curie alifanikiwa kuvumbua mada za nunurishi au radioactive. Baadaye akishirikiana na mmoja wa wasaidizi wa mama yake, mwanafizikia huyo alifanya utafiti na uhakiki katika uga huo na kupata mafanikio makubwa. Irene Joliot-Curie aliaga dunia 1957.***
Katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, nchini Ethiopia kulitokea mapinduzi yaliyopelekea kuondolewa madarakani utawala wa Haile Selassie. Haile Selassie alizaliwa mwaka 1892 nchini Ethiopia. Awali alikuwa mkuu wa mikoa kadhaa nchini humo na baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme. Mwaka 1930 alishika hatamu za uongozi wa Ethiopia akiwa mfalme wa nchi hiyo. Awali alifanya jitihada kubwa za kuyaunganisha makabila ya Ethiopia kwa shabaha ya kuyadhibiti. Haile Selassie aliwaajiri wataalamu wa kigeni na kuanza kufanya marekebisho ya kidara hatua kwa hatua. Alikomesha utumwa, akafanya marekebisho ya masuala ya kifedha na kuanzisha mfumo wa mahakama nchini Ethiopia. Hata hivyo mashambulio ya Italia dhidi ya Ethiopia mwaka 1935 yalisitisha mpango wake huo na alibakia nje ya nchi hadi mwaka 1941 aliporejea nchini kwa msaada wa Waingereza na kutwaa tena madaraka. Aliendeleza marekebisho yake ambayo zaidi yalijikita katika mji mkuu Addis Ababa na mambo yasio ya msingi huku sehemu kubwa ya Waethiopia wakikosa suhula za kimsingi za maisha. Selassie alikuwa tegemeza sana kwa nchi za Magharibi. Tarehe 12 Septemba mwaka 1974 Selassie aliondolewa madarakati katika mapinduzi yaliyofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo na mwaka mmoja baadaye utawala wa kifalme ulikomeshwa kabisa nchini Ethiopia. ***
Na siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, nchini Uturuki kulitokea mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Jenerali Kenan Evren na kupelekea kuondolewa madarakani Waziri Mkuu Suleyman Demirel na kisha kuundwa serikali ya kijeshi. Kuibuka kashfa ya ufisadi wa fedha na kuendelea hali ya kulegalega kisiasa na kijamii nchini Uturuki kulipelekea kutokea mgogoro wa kiuchumi ambapo hatimaye katika siku kama ya leo Jenerali Kenan aliyekuwa mkuu wa majeshi alifanya mapinduzi. Baada ya mapinduzi hayo, Jenerali Kenan akiwa pamoja na Baraza la watu sita walishika hatamu za uongozi wa nchi. Mbali na Waziri Mkuu kuondolewa madarakani kulitolewa amri pia ya kuvunjwa Bunge sambamba na kupigwa marufuku shughuli za vyama vya siasa na nchi ikawa inatawaliwa na serikali ya kijeshi. ***