Jumatatu tarehe 20 Septemba 2021
Leo ni Jumatatu tarehe 13 Safar 1443 Hijria sawa na Septemba 20 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1140 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu Abu Abdulrahman Ahmad bin Shuaib Nasai, maarufu kwa jina la Sheikhul Islam. Nasai alizaliwa mwaka 220 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Khorasan huko kaskazini mwa Iran na akaelea nchini Misri akiwa kijana. Huko alipata elimu ya fiqhi na hadithi na akaanza kufunza taaluma hizo. Baadaye Sheikhul Islam Nasai aliekele Damascus, Syria ambako alibainisha sifa na maadili ya watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake) na kupigwa mara kadhaa na wapinzani wa Ahlul Bait. Hatimaye alielekea Hijaz na kuishi mjini Makka. Nasai ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Khasaisu Amirul Muuminina Ali" na kile cha "Sunanun Nasai" ambacho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vya hadithi vya Kiislamu.
Nasaii ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Khasaisu Amirul Muuminina Ali" na kile cha "Sunanun Nasai" ambacho ni miongoni mwa vitabu mashuhuri vya hadithi vya Kiislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 1073 iliyopita alifariki dunia mtaalamu wa fasihi, fiqhi na tafsiri ya Qurani Muhammad Azhari Harawi. Alizaliwa mwaka 282 Hijria katika eneo la Harat nchini Afghanistan.Harawi alitekwa nyara na Waarabu wa jangwani akiwa safarini kuelekea Makka kwa ajili ya ibada ya hija na huko alijifunza lahaja asilia ya lugha ya Kiarabu ambayo aliitumia katika vitabu vyake. Mtaalamu huyo wa lugha ameandika vitabu vingi vya tafsiri na hadithi. Kitabu chake muhimu zaidi ni kile cha "Tahdhibul Lugha."

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, lilitengenezwa basi la kwanza lililokuwa likitumia nishati ya mvuke. Basi hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 30 na kwenda kwa kasi ndogo na lilitengenezwa na Gordon Branz, raia wa Uingereza. Hii leo mabasi bora na ya kisasa ni miongoni mwa vyombo muhimu vya usafiri kote duniani.

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, nchi ya Hungary iliungana na ardhi ya Austria na Francois Joseph akawa mtawala wa kifalme wa nchini mbili hizo. Hungary ambayo kwa mara kadhaa katika historia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na nchi zenye nguvu za Ulaya kama vile Austria na utawala wa Othmania, baadaye ilijipatia uhuru wake mnamo mwaka 1918 mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, Jean-Bedel Bokasa, dikteta wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. Bokasa alizaliwa mwaka 1922 na kusomea nchini Ufaransa. Alikuwa shabiki mkubwa wa Napoleon Bonaparte na Charles de Gaulle, viongozi wawili wa zamani wa Ufaransa. Alichukua madaraka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 1966 baada ya kufanya mapinduzi dhidi ya binamu yake, David Dacko, wakati Bokasa alipokuwa mkuu wa majeshi ya nchi hiyo. Jean-Bedel Bokasa alitawala nchi hiyo kwa mfumo wa kiimla na kwa kipindi cha miaka 13 na kusimamia moja kwa moja wizara 14 kati ya wizara 16 za nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.
Na siku kama ya leo, miaka 10 iliyopita, aliuawa , Mkuu wa Baraza Kuu la Usalama nchini Afghanistan. Burhanuddin Rabbani alizaliwa tarehe 20 Septemba mwaka 1940. Alikuwa kiongozi wa chama cha Jumuiya ya Kiislamu nchini humo na rais rasmi wa kwanza wa utawala wa Mujahidina huko Afghanistan. Hadi mwisho wa maisha yake, Burhanuddin Rabbani, alikuwa mkuu wa Baraza Kuu la Usalama lililoundwa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Hamid Karzay. Baraza hilo lilikuwa na wadhifa wa kufanya mazungumzo na kundi la Taleban kwa lengo la kufikiwa suluhu na kumaliza mgogoro wa taifa hilo kwa njia ya amani. Rabani aliuawa katika siku kama ya leo na gaidi aliyekuwa ameficha bomu katika kilemba chake, wakati alipoingia ofisini kwa mwanasiasa huyo kwa madai ya kufanya mazungumzo.