Sep 23, 2021 22:47 UTC
  • Ijumaa tarehe 24 Septemba 2021

Leo ni Ijumaa tarehe 17 Safar 1443 Hijria sawa na Septemba 24 mwaka 2021.

Siku kama ya leo miaka 547 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Muhammad Mustafa Imadi, maarufu kwa jina la  Abus-Su’ud, faqihi na mfasiri wa Qur'ani tukufu katika kijiji cha Mudarris karibu na mji wa Istanbul huko Uturuki. Baada ya kuhitimu masomo, Abus-Su’ud alijishughulisha na ufundishaji na kufanya kazi ya ukadhi mjini Istanbul, kazi aliyoendelea nayo hadi mwisho wa uhai wake. Abus-Su’ud alikuwa hodari katika masuala mbalimbali ya kijamii na aliandaa sheria za kiidara kwa mujibu wa dini ya Kiislamu katika utawala wa Othmania. Mbali na kuzungumza lugha ya Kituruki, alizungumza pia lugha za Kifarsi na Kiarabu. Msomi huyo wa Kiislamu pia ametunga mashairi katika lugha hizo. Miongoni mwa vitabu vya Abus-Su’ud ni ‘Irshadul-Aqlis-Saliim’ ‘Dua Nameh’ ‘Qanun Nameh’ na ‘Mafrudhaat'.

Katika siku kama ya leo miaka 188 iliyopita, kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Sheikh Abdul Rahim Sultanul-Qurrai Tabrizi, qaari mkubwa wa Qur’ani tukufu na mmoja wa walimu mashuhuri wa taaluma ya qiraa, huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kujifunza taaluma hiyo kutoka kwa baba yake, Sultanul-Qurrai Tabrizi alifahamiana na Sheikh Shamil Dagestani na kushirikiana naye. Wakati Sheikh Shamil Dagestani alipoandaa jeshi kwa ajili ya kupambana na Warusi, Sultanul-Qurrai alifanya safari kuelekea Dagestan ili kushiriki katika harakati hiyo. Baadaye alirejea Tabriz na kuanzisha chuo cha Qur’ani na ni wakati huo ndipo alipopewa lakabu ya Sultanul-Qurrai. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na ‘Risala katika Elimu ya Tajwidi’. Sultanul-Qurrai alifariki dunia mwaka 1336 Hijria huko Tabriz.

Katika siku kama ya leo miaka 82 iliyopita, ndege za kijeshi za Ujerumani zilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya mji mkuu wa Poland, Warsaw. Mashambulio hayo yalifanyika sambamba na kuanza Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na yaliendelea kwa muda wa siku tatu. Hatimaye wananchi wa mji huo walisalimu amri mbele ya majeshi ya Ujerumani baada ya mapambano na siku kumi na moja. Mashambulio hayo ya kinyama yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 15,000.

Picha ya sehemu moja ya mji mkuu wa Poland, Warsaw

Katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, Guinea Bissau ilitangaza uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mreno. Guinea Bissau iligunduliwa mwaka 1446 na Mwana Mfalme Henry aliyekuwa akitawala Ureno pamoja na wenzake na kuwa koloni la nchi hiyo. Guinea Bissau ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Guinea Ureno, ilikuwa miongoni mwa vituo vya biashara ya utumwa ya wazungu katika karne za 17 na 18. Na hatimaye ilipofika mwaka 1974, Ureno ikakubali kuwa huru nchi ya Guinea Bissau. Guinea Bissau iko kaskazini magharibi mwa Afrika na katika pwani ya Bahari ya Atlantic.

Bendera ya Guinea Bissau

Miaka 43 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vikosi vya usalama vya utawala wa Baath nchini Iraq vikishirikiana na utawala wa Shah viliizingira nyumba ya Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu huko Najaf. Kwa kuzingatia uhusiano wake mzuri na utawala wa Shah, utawala wa zamani wa Iraq ulimtaka Imam Khomeini asifanye mahojiano na waandishi wa habari, kutoa taarifa, kuhutubia wala kuzungumzia hali ya mambo ya Iran dhidi ya utawala wa Shah. Imam Khomeini aliwajibu kwa kusema kuwa: "Nitatekeleza wajibu wangu wa kisheria popote pale nitakapokuwa." Baada ya hapo, serikali ya wakati huo ya Iraq, ilimlazimisha Imam Khomeini kuondoka Iraq na hatua hiyo ikaandaa uwanja wa hijra ya kihistoria ya Imam Khomeini ya kuelekea Paris, Ufaransa na kupamba moto harakati za Mapinduzi ya Kiislamu.

Imam Khomeini akiondoka Iraq kuelekea Paris