Jumapili, 26 Septemba, 2021
Leo ni Jumapili tarehe 19 Safar 1443 Hijria sawa na Septemba 26 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1272 iliyopita yaani tarehe 19 Safar mwaka 171 Hijria alizaliwa Abu Ma'ashar Balkhi mmoja kati ya wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya nujumu wa Kiirani. Alielekea Baghdad na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Abu Ma'ashar Balkhi alitumia vyanzo vya lugha za Kiarabu, Kihindi, Kigiriki na Kisiriani kwa ajili ya kupata elimu ya nujumu na kuwa miongoni mwa wanajimu wakubwa katika zama zake. Kazi zake katika taaluma hiyo zilitumiwa kwa karne kadhaa katika Ulimwengu wa Kiislamu na Kimagharibi hata baada ya kufariki kwake dunia. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawalidul al Saghirah.

Katika siku kama ya leo miaka 133 iliyopita alizaliwa Thomas Stearns Eliot mshairi na mwanafasihi mashuhuri wa Uingereza. Malenga huyo ambaye ni mashuhuri kwa jina la S. T. Eliot alitoa nudhumu yake ya kwanza ya mashairi mwaka 1922 iliyokuwa na jina la "The Waste Land" na kupata umashuhuri mkubwa. Mwanafasihi huyo wa Kiingereza aliaga dunia mwaka 1965.
Siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, inayosadifiana na 26 Septemba 1907, nchi ya New Zealand iliyoko mashariki mwa Australia ilipata uhuru. Visiwa vya New Zealand vilikoloniwa na Uingereza mwaka 1769 na karne ya 19 Miladia, ilishuhudia ukoloni dhidi ya nchi hiyo ukishadidi sambamba na wimbi kubwa la wahajiri wa Kiingereza waliokuwa wakielekea katika nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, inayosadifiana na 26 Septemba 1960, Makamu wa Rais wa Marekani Richard Nixon na Seneta John F. Kennedy wa Massachusetts walikabiliana katika mdahalo wa kwanza wa televisheni wakati wakiwania tiketi ya kuingia ikulu ya White House. John Kennedy aliibuka na ushindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka huo.
Siku kama hii ya leo miaka 9 iliyopita Maya Nasri mwandishi habari wa Kikristo wa kanali ya televisheni ya Press ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa mjini Damascus nchini Syria wakati alipokuwa akitayarisha ripoti kwa ajili ya kanali hiyo. Maya Nasr alizaliwa tarehe 30 Julai mwaka 1979 nchini Syria na kuhitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Kaplan kilichoko New York huko Marekani. Nasr akiwa pamoja na Mkurugenzi wa kanali ya televisheni ya Press nchini Syria, Hussein Murtadha, alishambuliwa kwa kupigwa risasi mbili kichwani na mlenga shabaha wa wapinzani wa serikali ya Damascus akitayarisha ripoti ya matukio ya Syria. Mwenzake Maya, Hussein Murtadhaa alijeruhiwa katika shambulizi hilo.