Jumanne tarehe 19 Oktoba 2021
Leo ni Jumanne tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na Oktoba 19 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 1496 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Masoudi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW. Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani. Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa ulimwengu wa Kiislamu.

Tarehe 12 Rabiul Awwal mwaka wa kwanza Hijria, Mtume Muhammad (saw) aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa msikiti wa kwanza kabisa katika Uislamu katika kijiji cha Quba kilichoko pambizoni mwa Madina. Mtume (saw) aliweka jiwe la msingi la msikiti huo wa kihistoria wakati aliposimama kwa siku chache katika eneo la Quba akiwa njiani kutoka Makka na kuelekea Madina. Mtukufu huyo alisimama kwa muda katika kijiji cha Quba akimsubiri Ali bin Abi Twalib na jamaa wa familia ya Mtume.

Katika siku kama ya leo tarehe 12 Rabiul Awwal miaka 1202 iliyopita, alifariki dunia Imam Ahmad bin Hanbal mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Baghdad, Iraq ya leo. Ahmad bin Hanbal alizaliwa mwaka 124 Hijria, katika mji wa Baghdad na kupata elimu ya kidini katika mji huo kutoka kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Shafii. Imam Hanbal alifanya safari katika miji kadhaa kama vile Kufa, Basra, Makka, Madina, Sham na Yemen kwa minajili ya kukusanya hadithi za Bwana Mtume SAW. Ahmad bin Hanbal ndiye mwasisi wa madhehebu ya Kisuni ya Hanbal na mwandishi wa kitabu mashuhuri cha hadithi cha al Musnad.

Miaka 240 iliyopita katika siku inayofanana na ya leo, Charles Cornwallis, kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Uingereza nchini Marekani alisalimu amri mbele ya George Washington, kamanda wa kikosi cha wanajeshi wa Marekani na kwa msingi huo vita vya kuikomboa Marekani vikamalizika rasmi. Vita hivyo vilianza mwaka 1775 kati ya wahajiri wa Kimarekani na wakoloni wa Kiingereza. Miaka miwili baada ya ushindi wa mwisho wa wahajiri, pande mbili hizo zilisaini makubaliano mwaka 1783 ambapo kwa mujibu wake Uingereza ilitambua rasmi uhuru wa Marekani.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, Ali Hassan Salameh mmoja kati ya viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliuawa shahidi nchini Lebanon kupitia njama za vibaraka wa shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD. Salameh alikuwa afisa wa usalama wa PLO na aliuawa shahidi baada ya kuripuka bomu lililotegwa katika gari lake mjini Beirut. Jinai hiyo ya utawala haramu wa Israel ndani ya Lebanon kwa mara nyingine iliweka wazi ugaidi na uvamizi wa Israel dhidi ya ardhi ya nchi nyingine.

Katika siku kama ya leo miaka 34 iliyopita manowari za jeshi la Marekani zilishambulia visiwa vya mafuta vya Jamhuri ya Kiislamu katika Ghuba ya Uajemi wakati wa vita vya Iraq dhidi ya Iran.

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, alifariki dunia Ali Ezzat Begovic, mwanasiasa na mwandishi wa Bosnia Herzegovina. Ali Begovic alizaliwa mwaka 1925 na kupata taaluma ya sheria katika Chuo Kikuu cha Sarajevo katikati mwa Bosnia. Alianza kupambana na utawala wa kikomunisti wa Yugoslavia ya zamani akiwa kijana mdogo na kufungwa jela mara kadhaa. Mwaka 1989 Ali Begovic aliasisi chama kipya cha siasa kwa jina la Democratic Action kilichokuwa na nafasi kubwa katika uhuru wa Bosnia mwaka 1991. Mwanasiasa huyo wa Kiislamu ambaye baada ya uhuru wa taifa hilo alichaguliwa kuwa rais, alikuwa na nafasi kubwa katika kuwatetea raia wa Bosnia katika mashambulizi ya askari wa Serbia dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.
