May 23, 2016 09:32 UTC

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu ya tatu ya kipindi hiki cha Ufufuo na Safari ya Kurejea kwa Allah, ambacho leo kitakamilisha maudhui na kipindi kilichopita. Matarajio yetu kwamba mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

Katika kipindi cha wiki iliyopita tulielezea baadhi ya hoja zinazothibitisha kutokea ufufuo na safari ya mja kurejea kwa Mwenyezi Mungu. Tulisema dini zote za mbinguni zinaamini kuwepo suala la ufufuo na marejeo kwa Mola Muweza na zinasisitiza kuwa, suala hilo ni miongoni mwa misingi muhimu ya kiitikadi. Hata hivyo tulisisitiza kwamba wapo baadhi ya watu ambao hawaamini kabisa suala la kuwepo maisha mengine baada ya kifo na kwamba pamoja na hayo hawana hoja na ushahidi madhubuti wa kielimu wa kukanusha ufufuo. Tulisema Mwenyezi Mungu SW ndiye aliyeumba ulimwengu na vilivyomo na kwamba akili ya mwanadamu inahukumu kuwa, kukusanya pamoja maungo na vipande vya kitu kilichosambaratika na kutawanyika ni rahisi zaidi kuliko kukiumba kwa mara ya kwanza. Mwenyezi Mungu SW anaeleza mshangao wa watu hao na kujibu madai yao kuwa hawezi kufufua viumbe waliofariki dunia, miili yao ikasambaratika na kutapakaa kwa kusema katika aya za 66 hadi 68 za Suratu Maryam kwamba: Na mwanaadamu husema: Hivi kweli nitakapokufa, nitafufuliwa niwe hai tena? Je! Hakumbuki mwanadamu ya kwamba tulimuumba kabla, na hali hakuwa chochote? Basi naapa kwa Mola wako Mlezi! Kwa yakini tutawakusanya wao pamoja na mashet'ani; kisha tutawahudhurisha kuizunguka Jahannamu, nao wamepiga magoti!  

Katika kipindi cha wiki iliyopita tugusia ishara za ufufuo katika maisha ya mwanadamu kama vile kufufuka kwa maumbile baada ya kunyauka na kufa katika kipindi cha baridi, suala ambalo ni mfano wa jinsi wanadamu na viumbe vitakavyofufuliwa siku ya Kiyama. Baada ya hapo tiligusia mifano ya kihistoria kuhusiana na ufufuo, kama kufishwa na Uzayr na mnyama wake na kufufuliwa. <<<<<< >>>>>>

Katika mkondo huu wa mifano ya kihistoria ya ufufuo, Qur'ani Tukufu pia imezungumzia kisa cha Nabii Ibrahim al Khalil (as), ambacho kinaweka wazi maudhui ya kuhuishwa na kufufuliwa maungo na vipande vya kiumbe baada ya kusambaratika na kutapakaa sehemu mbalimbali.

Siku moja Nabii Ibrahim (as) alikuwa akipita pambizoni mwa mto, mara akaona mzoga wa mnyama ukiwa pambizoni mwa mto huo. Wanyama mbalimbali wa baharini, nchi kavu na wa angani walikuwa wameuzunguka mzoga ule na kila mmoja wao alikuwa akikata kipande au vipande vya mzoga ule na kuondoka navyo. Nabii Ibrahim (as) alijiuliza ndani ya nafsi yake kwamba, iwapo itatokea siku mwili wa mwanadamu ukawa katika hali kama ile, mifupa, ngozi na viungo vyake vikasambaa kwa wanyama wa baharini, nchi kavu na ndege wa angani, je, Mwenyezi Mungu ataweza kuvikusanya viungo na mifupa ya mwanadamu huyo na kumhuisha tena?

Hapo Nabii Ibrahim (as) alimuomba Mwenyezi Mungu SW amuonyeshe vipi ataweza kuurejesha na kuupa uhai mwili wa mtu aliyefariki dunia katika mazingira kama hayo!

Hakuna shaka kwamba, Nabii Ibrahim (as) alikuwa na yakini na suala la ufufuo kutokana na hoja za kiakili na kimantiki, lakini alimuomba Allah amuoneshe jinsi atakavyowafufua wafu Siku ya Kiyama ili aweze kuongeza na kunyanyua juu kiwango cha yakini yake na kujionea kadhia nzima kwa macho yake mwenyewe. Nabii Ibrahim akaulizwa, je, huamini? Alijibu kwa kusema: Ninaamini, lakini nataka nipate utulivu zaidi na kufikia daraja ya juu ya imani. Nabii Ibrahim (as) aliyekuwa akiamini ufufuo, alitaka kuongeza yakini aliyokuwa nayo, kwa sababu yakini inaweza kuongezeka, na ina daraja na marhala mbalimbali.

Mwenyezi Mungu alilipokea na kulikubali ombi la Nabii Ibrahim al Khalil na akamwamuru achukue ndege wanne na kuwakata vipande vipande. Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa, ndege hao walikuwa tausi, kuku jogoo, njiwa na kunguru ambao kila mmoja wao ni dhihirisho la sifa makhsusi. Tausi anatajwa kuwa ni dhihirisho la urembo, uzuri na ghururi, jogoo ni dhihirisho la matamanio ya kingono, njiwa ni kielelezo cha usanii na kunguru ni dhihirisho la kuwa na matarajio ya mbali.

Mwenyezi Mungu SW alimwamuru Nabii Ibrahim kuchinja ndege hao, awakate vipande vipande na kisha awachanganye pamoja. Baada ya hapo, aliamriwa aweka mafungu tofauti ya mchanganyiko huo juu ya pande mbalimbali za jabali kisha awaite ndege wale. Mtume wa Allah alitekeleza kama alivyoamrishwa na Mola Wake na hatimaye alishangazwa na kustaajabishwa alipowaona ndege wale wakijikusanya na kurejea katika hali na maumbo yao ya awali na kumjia mbio, licha ya kuwa ndege wale walikuwa wamechanganywa ngozi, nyama na mifupa yao. Aya ya 260 ya Suratul Baqarah inasema: "Na aliposema Ibrahim: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe vipi unavyofufua wafu. Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue. Akamwambia: Twaa ndege wanne na uwazoeshe kwako, kisha uweke juu ya kila kilima sehemu, kisha waite, watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, na Mwenye hikima". <<<<< >>>>>

Wapenzi wasikilizaji muda uliotenwga kwa ajili ya kipindi hiki umemalizika. Tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya Makala hii inayozungumzia ufufuo na marejeo ya mwanadamu baada ya kufariki dunia. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

 

 

 

 

Tags