Sep 28, 2016 09:18 UTC
  • Ufufuo na Marejeo ya Wanadamu kwa Mola (16)

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya makala hii ambayo hukujieni kila wiki.  

Katika makala ya wiki iliyopita tulizungumzia hali zinazotofautiana za waumini na makafiri wakati wa mauti na kutoka roho. Hata hivyo kama tulivyoashiria katika makala hiyo, kuna watu wengi wema na wanaoshikamana na dini lakini wakati fulani wanateleza na kufanya madhambi, kama ambavyo pia kuna makafiri na watu waovu ambao licha ya ukafiri na uovu wao, wametenda mambo mema katika baadhi ya nyakati za maisha yao. Au baadhi ya watu ambao batini na dhatu zao ni mbaya na ni waovu lakini dhahirina muonekano wao unaonekana kuwa nzuri. Hapa linakuja swali kwamba, hatima ya watu wa aina hii wakati wa mauti na mwanzoni mwa kuingia katika ulimwengu wa Akhera itakuwa vipi?

Katika dunia tunamoishi mambo mema na mazuri yamechanganyika na mabaya na maovu. Mazuri na mabaya ya wanadamu pia yamechanganyika. Tunajua pia kwamba, ufanisi na maangamizi ya wanadamu vinafungamana na amali na waliyoyafanya katika maisha yao ya hapa duniani, na amali na matendo hayo ndivyo vitakavyoainisha hatima yao katika ulimwengu wa Akhera. Maadamu mwanadamu angali hapa duniani ambao ndio ulimwengu wa taklifu na matendo, huwa kuna uwezekano wa kuwa mtu mwenye saada na ufanisi au mtu wa motoni na adhabu ya milele huko Akhera. Lakini baada tu ya kupatwa na mauti na kutokwa roho, mwanadamu huwa hana tena hiari na irada ya jambo lolote.

Batini na hakika ya baadhi ya watu katika dunia hii inatofautiana na dhahiri yao, na wako baadhi ya watu ambao dhahiri na batini zao zinaoana na kufanana. Ulimwengu wa Akhera ni ulimwengu wa kudhihirishwa na kuwekwa wazi batini na dhati za wanadamu. Katika ulimwengu huo kila amali njema au mbaya itawekwa wazi na kudhihirishwa.  Aya za 6 na 7 za Suratu Tariq zinasema:

یَوْمَ تُبْلَى السَّرَائِرُ.  فَمَا لَهُ مِن قُوَّةٍ وَلا نَاصِرٍ

"Siku zitakapodhihirishwa siri. Basi (mwanadamu) hatakuwa na nguvu wala msaidizi wa kumnusuru".

Hapa inatupasa kuangalia, Mwenyezi Mungu SW atahesabu vipi amali na matendo mema yanayofanywa na watu wasio wema na waovu? Au kwa mfano huchukua hatua gani mkabala wa amali na matendo maovu yanayofanywa baadhi ya wakati na watu wema kutokana na kuteleza au kughafilika?

Mtu muumini lakini aliyeteleza na kutenda dhambi ni kama mtu maridadi mbaye dhahiri na mavazi yake yamechafuka; kwa msingi huo anahitaji kusafishwa ili uchafu na madoa hayo yaondoke na hatimaye sura na dhati yake halisi viweze kuonekana. Vivyo hivyo batini na roho za wanadamu. Mtu mwenye batini na roho safi lakini dhahiri yake ina uchafu na madoa, anapaswa kusafishwa ili uchafu wa madhambi uondolewe. Nafasi ya mtu kama huyu ni peponi kwa sababu batini na roho yake ambayo ndiyo asili yake na kituo kikuu cha hisia za kibinadamu na uja wake mbele ya Mwenyezi Mungu, ni kisafi na chema. Hata hivyo kwa kuwa, baadhi ya wakati aliteleza na kufanya dhambi na maasi, anapaswa kusafishwa, kwa sababu muumini anayepelekwa peponi anapaswa kuwa safi na kuondokana na uchafu, kwani ni muhali kuingia peponi mtu mwenye taka na madoa ya madhambi.

 

Katika upande wa pili kuna watu ambao hapa duniani wamechafua batini na dhati zao kwa madhambi, maasia na ukafiri. Matendo maovu na machafu, kuwadhulumu wanadamu na kuchupa mipaka ya Mwenyezi Mungu kumeharibu dhati na batini zao. Hata hivyo baadhi ya nyakati huzipamba dhahiri na muonekano wao kwa matendo mazuri na mema japokuwa amali na matendo hayo mema hayakuathiri batini na dhati zao na kuwafanya watu wema na wasafi. Wakati wa sakaratul mauti na kutokwa roho, hijabu na pazia la dhahiri huondoka na batini chafu na iliyojaa dhambi na giza huonekana waziwazi; wakati huo mwanadamu huyo huunganishwa na wenzi wake. Sehemu ya aya za 36 na ya 37 za Suratul Anfal inasema:

وَالَّذِینَ کَفَرُواْ إِلَى جَهَنَّمَ یُحْشَرُونَ

لِیَمِیزَ اللَّهُ الْخَبِیثَ مِنَ الطَّیِّبِ وَیَجْعَلَ الْخَبِیثَ بَعْضَهُ عَلَىَ بَعْضٍ فَیَرْکُمَهُ جَمِیعًا فَیَجْعَلَهُ فِی جَهَنَّمَ أُوْلَئِکَ هُمُ الْخَاسِرُونَ

Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahannam. Ili Mwenyezi Mungu apate kuwapambanua walio waovu na walio wema, na kuwaweka waovu juu ya waovu wengine, na kuwarundika wote pamoja, na kuwatupa katika Jahannam. Hao ndio waliohasirika.      

Katika upande mwingine watu wema na waumini watakusanywa pamoja na kuingizwa peponi. Muumini si mtu wa ria na kujionesha, hakani haki popote pale anapokuwa na hujitahidi kufanya mema popote na wakati wote. Na kama ataghafilika baadhi ya wakati au kuteleza na kufanya dhambi na maasi, basi Mwenyezi Mungu SW hushughulikia amali zake hapa hapa duniani na kusafisha madhambi na dosari hizo kwa mashaka kama maradhi, umaskini, misukosuko, mitihani ya aina mblimbali na kadhalika. Hii ndiyo falsafa ya baadhi ya mashaka yanayowapata waumini na watu wema. Mashaka na misukosuko hiyo huwazindua na kuwaamsha na hatimaye kuwarejesha katika njia sahihi na iliyonyooka. Madhambi mengine ya waumini walioteleza na kufanya maasi pia huondolewa kwa mashaka ya kipindi cha sakaratul maut na kufariki dunia. Katika baadhi ya hadithi imepokewa kuwa, homa iliyompata muumini wa kweli huwa kafara na fidia na madhambi yake. Mkabala wake, raha na hali bora za baadhi ya makafiri na watenda maasia huwa malipo yao kutokana na baadhi ya amali njema walizotenda hapa dunia licha ya kuwa na batini na dhati mbaya na chafu. Hii ni kwa sababu kafiri huwa hafanyi jema kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, hivyo Mola Muumba humlipa hapa hapa duniani kutokana na nia yake.

Wapenzi wasikiliza wanadamu wote, wema na waovu, huwa na matumaini ya kuwa na mwisho mwema na saada na ufanisi wa milele. Baadhi yao huficha ukafiri wa ndani ya nafsi wakiwa na matumaini kwamba, pepo ni mali yao. Baadhi pia wenye imani duni na dhaifu ambazo hazijafikia kiwango cha yaqini, hudhani kwamba peponi ndio makazi yao. Lakini kama tulivyosema katika baadhi ya makala zilizopita, inatupasa kuelewa kwamba, wakati wa kutokwa roho na kufariki dunia Shetani huwajia watu mbalimbali hususan waumini na kujaribu kuteteresha imani na itikadi zao katika dakika hizi za mwisho. Watu ambao ni waumini halisi na wanaomjua vyema Shetani na vitimbi vyake huwa hawahadaiki kwa ahadi zake katika dakika na nyakati hizo za mwisho baada ya kumuasi Shetani mlaaniwa katika kipindi chote cha maisha yao. Kinyume chake, watu wenye imani dhaifu na za kijuujuu yumkini wakahadaika kwa ahadi za mlaaniwa huyo katika misukosuko na dakika ngumu za kutokwa roho. Hali hii ndiyo inayoelezwa katika aya ya 16 ya Suratul Hashr pale Mwenyezi Mungu SW anaposema:

کَمَثَلِ الشَّیْطَانِ إِذْ قَالَ لِلإِنسَانِ اکْفُرْ فَلَمَّا کَفَرَ قَالَ إِنِّی بَرِیءٌ مِّنکَ إِنِّی أَخَافُ اللَّهَ رَبَّ الْعَالَمِینَ

"Ni kama mfano wa Shetani anapomwambia mtu: Kufuru. Na akikufuru humwambia: Mimi siko pamoja na wewe. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote".

Muumini wa kweli katika kipindi hiki huwa kama jabali na mlima madhubuti mbele ya hadaa za Shetani na vitimbi vyake vya mwisho. Imepokewa katika tafsiri ya Ayyashi kwamba Imam Ja'far Swadiq (as) ambaye ni miongoni mwa maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume wetu Muhammad (saw) amesema: Kila mja mwenye imani anapokaribia kufariki dunia, Shetani humwendea kutoka kulia kwale na kushoto kwake akijaribu kumuondoa katika itikadi na dini yake, lakini Mwenyezi Mungu SW humlinda. Hii ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa waumini pale aliposema katika aya ya 27 ya Suratu Ibrahim kwamba:

یُثَبِّتُ اللَّهُ الَّذِینَ آمَنُواْ بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِی الْحَیَاةِ الدُّنْیَا وَفِی الآخِرَةِ وَیُضِلُّ اللَّهُ الظَّالِمِینَ وَیَفْعَلُ اللَّهُ مَا یَشَاء

"Mwenyezi Mungu huwafanya imara wenye kuamini kwa kauli thabiti katika maisha ya dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwaacha wakapotea hao wenye kudhulumu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo".

Kauli ya Imam Swadiq (as) inayosema "Shetani huwaendea waumini kutoka upande wa kulia" ina maana kwamba, Shetani hujaribu kuwahadaa kupitia pande za kiroho na masuala ya kiimani, na kuwaendea kutoka upande wa kushoto kuna maana ya kuwaendea kupitia masuala ya kimaada na kidunia. Hivyo muumini wa kweli aliyeimarisha imani yake kwa amali na matendo mema hapa duniani, pale anapoghafilika na kuteleza akafanya dhambi na maasi huharakia kutubu na kuomba msamaha kwa Mola. Anapomuudhi na kumkera mwanadamu mwenzake humuomba msamaha na kama amechukua haki ya mtu hufidia na kuziba nakisi na kasoro hiyo na kamwe haruhusu madhambi kurundikana na kuwa mzigo juu ya mabega yake. Huwa kielelezo cha aya ya 201 ya Suratul Aaraf inayosema:

إِنَّ الَّذینَ اتَّقَوا إِذا مَسَّهُم طائِفٌ مِنَ الشَّیطانِ تَذَکَّروا فَإِذا هُم مُبصِرونَ  

Hakika wale wenye taqwa (wachamungu) zinapowagusa pepesi za Shetani huzinduka na kisha huwa macho (na makini). 

Tags