Sep 20, 2016 04:41 UTC
  • Ufufuo (14)

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Ni wakati mwingine umewadia wapenzi wasikilizaji wa kuwa nanyi katika sehemu ya 14 ya kipindi cha maadi na safari ya mja kurejea kwa Mola Muumba. Katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia dakika na nyakati za mwisho za uhai wa mwanadamu duniani na kipindi cha sakaratul mauti na kukata roho.

Tulisema kuwa, kipindi hicho mwanadamu anayekuwa katika hali ya Ihtidhar huona mambo mengi yasiyo ya kimaada akiwemo Malaika wa Mauti, shetani na pengine Mtume (saw) na Aali zake watoharifu. Leo tutangumzia Malaika wa Mauti. Karibuni….

Kifo ambacho ni kutengana roho na mwili, hutokea kwa amri ya Mwenyezi Mungu Muumba. Wakati wa kifo unapowadia, Mwenyezi Mungu humuamuru Malaika Wake kutoa roho ya kiumbe, naye hutekeleza amri hiyo bila ya kusita. Malaika wa Mauti amepewa wasaidizi ambao hushirikiana kutoa roho ya kiumbe husika. Kwa maana kwamba, kama ambavyo mkuu wa kundi la walinzi - kwa mfano -, huwa na wasaidizi wake ambao huwatumia katika kazi mbalimbali, Malaika wa Mauti pia anao malaika wengine anaowatumia kutoa roho za watu na kuzikabidhi kwake na kishe yeye huzikabidhi kwa ukamilifu kwa Mwenyezi Mungu SW. Aya ya 11 ya Suratul Sajdah inasema: Sema: Atakufisheni Malaika wa Mauti aliyewakilishwa juu yenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi. Sehemu moja ya aya ya 42 ya Suratu Zumar pia inasema: Mwenyezi Mungu huchukua roho zinapokufa... Miongoni mwa maswali yanayoulizwa kuhusu Malaika wa Mauti ni kwamba, inawezekana vipi kwa Malaika mmoja kutoa roho za wanadamu wengi walioko katika maeneo mbalimbali na tofauti ya dunia katika dakika na wakati mmoja? Kwa mfano tu wakati mwingine idadi kubwa ya watu hufariki dunia katika zilzala na mtetemeko wa adhi na wakati huo huo ndege huanguka katika sehemu nyingine ya dunia na kuua mamia ya watu, huku wengine wakifariki dunia wakati huo huo kutokana na ajali, uzee na magonjwa mbalimbali katika sehemu nyingine ya dunia. Inawezekana vipi kwa Malaika wa Mauti kuchukua roho za wanadamu hawa wote wanaokuwa katika maeneo tofauti ya dunia tena katika wakati mmoja?

Imepokewa katika hadithi kwamba, mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Ja'far Swadiq (as) amesema kwamba Malakul Maut aliulizwa swali kwamba, vipi unachukua roho za watu wa mashariki mwa dunia na wa maghaibi wakati mmoja? Malaika wa Mauti alisema: Mimi huziita roho za wanadamu nazo huniitikia. Kisha akasema: Dunia mbele yangu mimi ni mithili ya chombo cha chakula kinachokuwa mbele ya mmoja wenu ambaye hupeleka mkono na kuchukua chakula popote pale anapotaka katika chombo hicho. Dunia nzima kwangu mimi ni sawa na sarafu ya dirhamu inayokuwa mikononi mwa mmoja wenu ambaye huigeuza atavyo na kuangalia pande zake zote mbili. (Manla Yahdhuruhul Faqiih)      <<<<   

 

Wapenzi wasikilizaji namna ya kuchukuliwa roho za wanadamu kunatofautiana kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine. Wanadamu wote watamuona Malaika wa Mauti wakati wa kufariki dunia lakini kila mmoja wao atamuona katika sura inayonasibiana na kulingana na amali na matendo yake hapa duniani. Imepokewa katika hadithi kwamba, Nabii Ibrahim (as) alikutana na Malaika mmoja wa Mwenyezi Mungu. Alimuuliza wewe ni nani? Malaika alisema: Mimi ni Malaika wa Mauti. Nabii Ibrahim alimuuliza: Unaweza kunionesha sura unayokuwa nayo wakati unachukua roho ya muumini? Malaika alisema ndiyo, kisha akamuomba afumbe macho yake. Nabii Ibrahim anasema: Nilifumba macho yangu na nilipoyafumbua niliona kijana mwenye sura nzuri, mavazi maridadi, mwenye kuvutia na mwenye harufu nzuri sana. Kisha Nabii Ibrahim (as) alisema: Iwapo muumini hataona chochote wakati wa kufariki dunia isipokuwa kijana huyu mwenye sura nzuri na mavazi maridadi basi sura hiyo inamtosha kuwa ujira na malipo yake.  Baadaye Nabii Ibrahim alimwambia Mailaka wa Mauti kwamba: Je, unaweza kunionesha sura unayokuwa nayo wakati unachukua roho ya mtu fasiki na mwenye madhambi? Malakul Maut alisema: Hutaweza kustahamili kuona sura hiyo. Nabii Ibrahim alisema: Ninaweza kustahamili. Malaika alimwamuru kufumba macho yake kisha akayafumbua. Nabii Ibrahim anasema: Niliona mtu mweusi kupita kiasi mwenye nywele ndefu, harufu mbaya na mavazi yenye rangi nyeusi tititi. Wakati huu Nabii Ibrahim alizimia na alipozinduka na kumuona tena Malaika wa Mauti katika hali yake ya awali alisema: Kama mtu fasiki hatakutana na yeyote yote isipokuwa mwenye sura hii basi hiyo inamtosha kuwa adhabu na jazaa yake. (Tafsiri ya Thaqalain, juzuu ya 5)  

Wapenzi wasikilizaji, sura na maumbile ya Malaika wa Mauti inatofautiana kwa watu mbalimbali. Huwa sura yenye haiba, nzuri na maridadi kwa waumini na watenda mema na sura ya kutisha, mbaya na isiyovumilika kwa watu waliotumia umri wao hapa duniani katika maasia na kutenda maovu. Hivyo hivyo katika namna ya kuchukuliwa roho za wanadamu. Kwa wale waliotenda mema, kujiepusha na maasi na kumtii Mwenyezi Mungu, basi amali na matendo yao yatatoa shufaa na maombezi kwao. Imepokewa katika hadithi kwamba muumini mwenye taqwa na uchamungu, anayewasaidia ndugu zake katika dini, mkarimu na mwema hutokwa na roho kwa wepesi na bila ya mashaka makubwa.

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kuzungumzia jinsi roho ya Mtume wetu kipenzi, Muhammad (saw) ilivyochukuliwa. Imepokewa katika kitabu cha Biharul Anwar na vitabu vingine kadhaa vya Ahlusunna kama Twabaqatul Kubra kwamba: Siku Mtume (saw) alipofariki dunia, Malaika mkuu wa Mwenyezi Mungu, Jibrilu, aliteremka kwa mtukufu huyo kisha akasema: Ewe Ahmad! Kutokana na ubora na utukufu wako, Mwenyezi Mungu SW amenituma kwako akiuliza jambo ambalo Yeye analijua zaidi kuliko wewe. Swali lenyewe ni kwamba: Unajisikiaje? Mtume alisema: Najisikia mwenye masikitiko na majonzi. Malaika Jibrilu ambaye alikuwa ameandamana na malaika mwingine mtukufu wa Mwenyezi Mungu maarufu kwa jila la Malaika wa Mauti pamoja na malaika wengine elfu sabini, alimwambia Mtume wa Allah kwamba: Israiil anaomba idhini ya kuingia ndani, na kabla yako wewe hajawahi kumuomba idhini mtu yeyote na hatafanya tena hivyo kwa yeyote baada yako.

Mtume (saw) alimwambia Jibrilu amruhusu aingie ndani. Malaika Israiil aliingia na kusimama kwa heshima na taadhima mbele ya Mtume kisha akasema: Yaa Rasulallah! Ewe Ahmad! Mwenyezi Mungu mtukufu amenituma kwako na kuniamuru nifanye chochote utakachotaka. Kama utaniamuru nichue roho yako nitafanya hivyo, na kama utaniamuru nikuache nitatii amri yako.

Mtume wa Mwenyezi Mungu alisema: Tekeleza uliyoamrishwa kufanya kuhusiana na mimi. Israaiil alisema: Kazi yangu mimi inategemea amri yako.

Malaika Jibrilu alisema: Ewe Ahmad! Mwenyezi Mungu ana hamu ya kukutana na wewe.

 Mtume wa Allah alisema: Ewe Israaiil! Tekeleza majukumu yako.

Ulipokaribia wakati wa kuchukuliwa roho tukufu na takasifu ya kiumbe bora zaidi wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, Malaika Jibrilu alisema: Sala na salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu yako ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Hizi ni hatua zangu za mwisho hapa adhini na kamwe sitateremka tena ardhini baada ya leo. Nilikuwa nikiteremka ardhini kwa ajili yako na kwa kuwa unaondoka dunia hii na kuelekea katika ulimwengu mwingine hakuna tena haja ya mimi kuja ardhini.

Wakati huu Malaika wa Mauti, Israaiil alichukua roho safi, tukufu na takasifu ya Mtume Muhammad amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake watoharifu.

Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.