Oct 13, 2016 12:25 UTC
  • Ufufuo na Marejeo ya Mja kwa Allah (17)

Katika makala ya wiki iliyopita tulizungumzia taathira ya amali na matendo mema na mabaya ya mja katika hatima yake. Makala yetu ya leo itazungumzia ulimwengu wa Barzakhi ambao ndio nyumba ya kwanza ya mwanadamu baada kifo na kufariki dunia.

Barzakh ina maana ya kitu kinachozuia na kutenganisha baina ya viti viliwi. Neno hilo limekaririwa mara kadhaa katika ya za Qur'ani Tukufu kama katika aya ya 100 ya Suratul Muuminun, aya ya 53 ya Suratul Furqan na aya ya 20 ya Suratul Rahman. Tunapochunguza aya zote zinazohusiana na Barzakh tunaona kuwa, mbali ya Siku ya Kiyama ambako amali na matendo ya waja yatashughulikiwa, kuna ulimwengu mwingine baina ya dunia hii ya kimaada na Siku ya Kiyama ambao kiistilahi unaitwa ulimwengu wa Barzakh. Ulimwengu huu wa Barzakh pia unaitwa "A'lamul Mithal", kwa maana ya ulimwengu wa mfano, kwa sababu ni mfano na picha ndogo ya ulimwengu wa Akhera na Siku ya Kiyama. Hata hivyo inatupasa kuelewa kwamba, ni muhali kuweza kupata maarifa na taswira kamili ya ulimwengu wa Barzakhi kabla ya kuingia kwenye ulimwengu huo. Kwa hakika ulimwengu wa Barzakhi ukilinganishwa na dunia hii ni mithili ya dunia yetu hii ikilinganishwa na fuko la uzazi la mama. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, iwapo mtoto aliyeko katika fuko la uzazi ataambiwa kuwa, mbali na dunia yako hii kuna ulimwengu mwingine mpana na mkubwa zaidi, basi hataweza kuelewa vyema na kupata taswira na picha kamili ya dunia hii. Pamoja na hayo inawezekana kupata taswira nakisi na isiyokamili ya ulimwengu wa Barzakhi. Ulimwengu huo unashabihiana kwa njia moja au nyingine ya ulimwengu anaoingia ndani yake mwanadamu anapokuwa katika usingizi. Mwenyezi Mungu SW anaashiria suala hilo katika aya ya 42 ya Suratu Zumar akisema:

اللَّهُ یَتَوَفَّى الأَنفُسَ حِینَ مَوْتِهَا وَالَّتِی لَمْ تَمُتْ فِی مَنَامِهَا فَیُمْسِکُ الَّتِی قَضَى عَلَیْهَا الْمَوْتَ وَیُرْسِلُ الأُخْرَى إِلَى أَجَلٍ مُسَمًّى إِنَّ فِی ذَلِکَ لَآیَاتٍ لِّقَوْمٍ یَتَفَکَّرُونَ

Mwenyezi Mungu huzichukua roho zinapokufa. Na zile zisiokufa wakati wa kulala kwake, huzishika zilizohukumiwa kufa, na huzirudisha nyengine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri.

Aya hii inaonesha wazi kuwa, kifo kinashabihiana na usingizi na kwamba katika hali zote mbili za usingizi na kifo, Mwenyezi Mungu huchukua roho za wanadamu, kwa tofauti kwamba, mtu ambaye wakati wa kifo chake umewadia, Mwenyezi Mungu Muweza huchukua kikamilifu roho yake, na yule ambaye wakati uliopangwa wa kifo chake haujafika hurejeshewa roho yake wakati wa kuamka.

Mtu mmoja alimuuliza Imam Muhammad al Jawad (as) ambaye ni miongoni mwa maimamu watoharifu na wajukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) kwamba: Kifo na mauti ni nini? Mtukufu huyo alisema: Kifo ni usingizi huuhuu unaowajieni kila usiku kwa tofauti kwamba, muda wake ni mrefu zaidi na mwanadamu haamki kutoka mwenye usingizi huo mpaka Siku ya Kiyama. (Tazama: Maanil Akhbar) Kwa msingi huo usingizi ni mfano bora zaidi wa kuweza kuelewa ulimwengu wa Barzakhi.

 

Katika ulimwengu wa Akhera au kwa maneno mengine Siku ya Kiyama, hakuna maada na vitu vya kimaada. Vivyo hivyo hakuna maada katika ulimwengu wa Barzakhi ambao ni ulimwengu unaotenganisha baina ya dunia na Akhera, lakini kuna baadhi ya athari za maada kama umbo, saizi na eneo. Njia bora zaidi ya kujua ulimwengu wa Barzakhi ni ndoto tunazoziona usiku na mchana. Ndoto ni miongoni mwa awamu na daraja za ulimwengu wa Barzakhi. Mambo tunayoyaona katika ndoto huwa na umbo, saizi na kiwango lakini si ya kimaada. Mwili wa kibarzakhi unashabihiana na hali hiyo. Tofauti yake, katika ulimwengu wetu huu wa kimaada kuna mwili wenye kiasi na saizi, umbile.

Katika ulimwengu wa usingizi roho ya mwanadamu husafiri na kufanya harakati kwa wepesi, kutokana na kuwa katika ulimwengu wa Barzakhi viumbe huwa havina mpaka wa eneo mithili ya kufungiwa katika mwili na kiwiliwili cha kimaada. Ni vyema pia kuelewa kwamba, nguvu na uwezo wa kudiriki na kuelewa mambo wa mwanadamu huwa mkubwa na mpana zaidi katika ulimwengu wa Barzakhi kutokana na kutokuwepo maada katika ulimwengu huo. Kwa msingi huo ladha, uchungu, furaha na ghamu, woga na kadhalika huwa vikali na shadidi zaidi katika ulimwengu huo wa Barzakhi kuliko ilivyo katika dunia hii.

Wakati mwanadamu anapofariki dunia na kuingia katika ulimwengu wa Barzakhi hupata uwezo mkubwa na mpana zaidi wa kujua na kuelewa mambo mbalimbali kwa undani. Wakati huo huwa mithili ya mtu aliyeamka kutoka kwenye usingizi mzito. Mtume Muhammad (saw) anasema: "Wanadamu wamelala na wanapofariki dunia huzindukana". (Al Mahajjatul Baidhaa, juzuu ya 7)

Maneno hayo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu yana maana ya kuwa macho na makini baada ya kupatwa na mghafala. Kwani baada ya kufariki dunia hijabu na pazia zote za mghafala zilizomzuia mwanadamu kuona na kufikiria ulimwengu mwingine wa milele, huondolewa. Wakati huo, kama mwanadamu hakuwa miongoni mwa watu wenye imani na wachamungu, hupatwa na simanzi na majuto makubwa na kuomba kurejeshwa duniani kama zinavyosema aya za 99 na 100 za Suratul Muuminun kwamba:

حَتَّى إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ. لَعَلِّی أَعْمَلُ صَالِحًا فِیمَا تَرَکْتُ کَلاَّ إِنَّهَا کَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَى یَوْمِ یُبْعَثُونَ

Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu Mlezi! Nirudishe, ili nitende mema sasa badala ya yale niliyoyaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapofufuliwa.

Wapenzi wasikilizaji, dunia inaelekea kwenye ukamilifu na daima harakati hiyo ya kuelekea kwenye ukamilifu inaendelea abadi na dahari. Kanuni hii inaoana na hekima na matakwa ya Mola Muumba. Ulimwengu wa Barzakhi ni ulimwengu ambao ni kamili zaidi kuliko dunia yetu hii lakini ni duni na wa chini ukilinganishwa na ulimwengu wa Akhera. Kwa maneno mengine ni kuwa, maadamu mwanadamu hajapitia kipindi cha ukamilifu cha ulimwengu wa Barzakhi, huwa hayuko tayari kwa ajili ya kuingia katika ulimwengu wa Akhera na Siku ya Kiyama. Mwanadamu huyu huwa mithili ya janini na mtoto aliyeko katika fuko la uzazi la mama ambako kama hatapata ukamilifu wa kimwili na kiroho unaohitajika, basi hataweza kuingia katika dunia hii tunakoishi. Hivyo hivyo mwanadamu, ili aweze kuingia katika ulimwengu wa milele, anapaswa kupitia kipindi cha Barzakhi ili apate mwili na roho inayonasibiana na kuoana na ulimwengu wa milele.

 

Miongoni mwa sifa za kipindi cha Barzakhi ni kwamba mwanadamu anaweza kufidia baadhi ya amali zake alizotenda duniani akiwa huko. Kwa mfano mtu anayedaiwa na Mwenyezi Mungu au waja wake anaweza kuacha wasia kwa warithi wake walipe deni hilo. Kwa njia hiyo hali yake katika ulimwengu wa Barzakhi hubadilika na kupanda daraja. Imepokewa kwamba Mtume (saw) amesema: Siku moja Nabii Issa Masiih (as) alipita pembeni ya kaburi ambalo mwenye nalo alikuwa akiadhibiwa. Mwaka mmoja baadaye alipita tena kandokando ya kaburi hilo la kupata kwamba, mwenye kaburi hilo hakuwa akiadhibiwa. Alimuuliza Mwenyezi Mungu sababu ya kubadilika hali ya mwenye kaburi hilo na kuambiwa: Mwenye kaburi hili ameacha mtoto mwema duniani ambaye amebaleghe la kutenda mambo mema mawili: Kwanza ametengeneza njia kwa ajili ya kupita watu, na pili amempa makazi mtoto yatima. Hivyo mimi pia nimesamehe madhambi ya baba huyo kwa heshima ya amali za mtoto wake mwema. (Tazama Aamali cha Sheikh Swaduq)

Kuacha sira, ada na mwenendo mzuri na wa kuigwa katika jamii kunaweza kubadili nafasi na hali ya mjaa katika ulimwengu wa Barzakhi. Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) amenukuu kutoka kwa babu yake, Mtume Muhammad (saw) kwamba amesema: Mtu yeyote anayejenga suna na jambo zuri la kuigwa katika jamii hupewa ujira wa jambo hilo na ujira mwingine watu wanaofanya au kutumia sira na jambo hilo hadi Siku ya Kimaya bila kupungua ujira wa watu wanaotumia au kufanya jambo na suna hiyo. (Tuhaful Uquul).

 

Vilevile imenukuliwa kutoka kwa Mtume (saw) kwamba amesema: "Wakati mwana wa Adamu anapofariki dunia amali na matendo yake yote hukatikana na kusimama isipokuwa katika hali tatu. Awache mtoto mwema anayemuombea dua na istighfar, elimu inayowafaidisha watu baada yake au sadaka inayobakia". Mfano wake sadaka inayobakia na kuwanufaisha watu kama kujenga msikiti, madaraja, barabara, hospitali, shule, kujenga visima na kadhalika.

Pamoja na haya inatupasa kuelewa kwamba, kama ambavyo kuacha suna, njia na jambo zuri linalowanufaisha watu kuna taathira katika hali ya mwanadamu katika limwengu wa Barzakhi, kuacha suna, njia na jambo baya katika dunia hii pia kuna taathira mbaya katika ulimwengu huo. Hadithi zinasema kuwa, mtu anayeweka msingi wa suna, ada na jambo baya katika jamii na njia hiyo ikafuatwa na wanadamu wengine, basi dhambi zake humuandama mwanzilishi wake hata huko katika ulimwengu wa Barzakhi.    

Tags