Sep 27, 2016 08:28 UTC
  • Ufufuo na Marejeo ya Wanadamu kwa Mwenyezi Mungu (15)

Katika makala iliyopita tulizungumzia Malaika wa Mauti na wanadamu anavyotolewa roho kwa njia tofauti. Tulisema kuwa, kila mtu anayefariki dunia humuona malaika huyo wakati wa kutokwa na roho kulingana na matendo na amali zake hapa duniani. Leo tutatupia jicho hali za waumini na makafiri wakati wa mauati na kutokwa roho.

Dakika na kipindi cha kutokwa na roho na kupatwa na mauti huwa kigumu sana kwa watu wote. Ugumu na mashaka hayo ya kuanza kuingia katika ulimwengu wa Barzakhi ni wanadamu wote wa watu wote wa kawaida watakumbana nayo. Hata hivyo tofauti za daraja za imani za watu zina taathira katika ugumu au wepesi wa kipindi cha mauti na kutokwa roho. Ni wazi kuwa, kadiri mwanadamu anavyoanisika na kuipenda zaidi dunia ndivyo anavyopatwa na mashaka na machungu makubwa zaidi wakati anapokuwa anaachana na kutengana nayo. Kinyume chake, kadiri thamani za Akhera na ulimwengu mwingine zinavyokuwa muhimu zaidi kwa mwanadamu na mapenzi yake kwa dunia na vilivyomo yakawa madogo ndivyo anavyopatwa na mashaka na machungu madogo zaidi anapokuwa anafarikiana na kuachana nayo. Mashinikizo na machungu anayopata mtu huyu wakati wa kutokwa roho na kufariki dunia hii ya kimaada huwa machache sana yakilinganishwa na ladha na raha anazopata wakati anaingia katika ulimwengu wa Barzakhi. Bali kwa hakika huwa anajiona kuwa ametoka katika jela ya kimaada ya mwili na kupaa katika malakuti na dunia pana na kubwa zaidi.

Katika aya mbalimbali za Qur'ani tukufu Mwenyezi Mungu SW ameeleza kifo na hali zake tofauti kwa waumini na makafiri. Baadhi ya aya hizo zinawapa bishara njema waumini na nyingine zinawatahadharisha na kuwaonya makafiri. Kwa mfano tu aya ya 62 ya Suratu Yunus inawapa bishara njema mawalii wa Mwenyezi Mungu kwamba hawatapatwa na huzuni wala woga katika maisha ya dunia na Akhera. Biashara hii njema inahusu vipindi vyote vya maisha ya dunia na Akhera ya mawalii wa Mwenyezi Mungu kwa maana ya watu wasiotenda au kufanya dhambi. Hawa ni watu ambao daima huzichunga na kuzihesabu nafsi zao. Daima huchunguza daftari la matendo yao na kujipinda katika kutakasa nafsi. Tunapaswa kuelewa kuwa, adhabu na mashaka ya mwanadamu katika kipindi cha kutoka roho au anapokuwa kaburini katika ulimwengu wa Barzakhi na hata Akhera hutokana na matendo maovu yaliyotendwa na mwanadamu huyo hapa duniani. Kimsingi huzuni na maumivu humpata mtu kutokana na kuachana au kupoteza kitu alichokuwa akikipenda sana na kushikamana nacho barabara. Hivyo hupatwa na maumivu na machungu kwa sababu ya kukipoteza au kuachana nacho. Vivyo hivyo woga na hofu hutokana na wasiwasi wa kuachana au kupoteza kitu alichokuwa akikipenda na kukiashiki. Wanadamu wote wanaoipenda sana na kuiashiki dunia na kutengeneza maisha yao kwa mujibu wa njozi zisizo na mashiko daima huwa katika wasiwasi, wahka na hofu. Kinyume chake, mawalii wa Mwenyezi Mungu husafisha roho zao kwa kujiepusha au kutoipenda kupita kiasi dunia hii ya kimaada na kuzijaza roho zao kwa mahaba na kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hawa huwepeseshewa mashaka ya sakaratul mauti na kipindi cha kutokwa na roho, bali huwa na hamu kubwa ya kuelekea kwenye neema na ulimwengu mpana na mkubwa zaidi.

 

Hapa yumkini baadhi ya watu wakafungamanisha suala la kutokuwa na hofu wakati wa kufariki dunia mawalii wa Mwenyezi Mungu na jinsi ya vifo vyao vilivyotokea. Kwa mfano wanasema baadhi ya waumini na mawalii wa Mwenyezi Mungu walikumbwa na vifo ambavyo kidhahiri vilikuwa vyenye machungu na mashaka makubwa kama kuchinjwa, kusulubiwa au kukatwa mapanga na kuchomwa moto, na kinyume chake, baadhi ya makafiri walifariki dunia kwa utulivu.

Ukweli ni kuwa, hali na jinsi mtu anavyofariki dunia si kigezo cha kutokuwa na huzuni na hofu wakati wa kutokwa na roho. Kwa mfano tu Firauni alimsulubu mke wake Asia aliyekuwa na imani kubwa kwa kumpiga misumari minne na kumuweka kwenye jua kali na kisha kuweka jiwe kubwa kifuani mwake. Hata hivyo mwanamke huyo mwema, kama inavyosimulia aya ya 11 ya Suratu Tahriim, alikuwa akinong'ona na Mola wake katika hali hiyo na kusema: "Mola Wangu Mlezi! Nitayarishie mimi nyumba huko kwako peponi…". Mfano mwingine ni pale mal'uuni Ibn Mujim alipompiga panga utosini Imam Ali bin Abi Twalib alipokuwa akiswali asubuhi msikitini. Mtukufu huyo alisikika akisema kwa sauti kubwa: "Hakika nimefuzu kwa jila la Mola wa al Kaaba". Hivyo basi aina ya kidhahiri ya mauti na kifo cha mtu si kipimo na mizani ya imani yake. Kwa ujumla kuna aina nne za kifo kwa mujibu wa aya za Qur'ani tukufu na hadithi za Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu. Baadhi ya watu hufariki dunia na kutokwa roho kwa wepesi. Aina hii ya mauti na kutokwa roho huwa ni ya waumini wa kweli ambao katika maisha yao yote walitii amri za Mola wao na kufuata mafundisho ya Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu. Khalifa na wasii wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Ali bin Abi Twalib amesema: Wakati watu wema wanapofariki dunia hupewa bishara njema na kupenda mauti na hatimaye hutokwa roho na kufariki dunia kwa wepesi. (Biharul Anwar 6:153)

Kundi la pili ni la waumini ambao waliteleza na kutenda baadhi ya dhambi hapa duniani. Kundi hili linahitaji kufutiwa dhambi hizo na kusafishwa, na mashaka ya kipindi cha kufariki dunia na kutokwa roho huwa kafara na fidia ya madhambi hayo. Mtume Muhammad (saw) anasema: «الموتُ کفّارة لذُنوبِ المؤمنین» "Mauti na mashaka yake ni fidia ya madhambi ya waumini". (Biharul Anwar 6:151)

 

Kundi la tatu ni la baadhi ya makafiri na madhalimu ambao yumkini wakawa na kifo na mauti mepesi. Suala hili hutokana na uadilifu wa Mwenyezi Mungu SW ambaye hapotezi ujira wa kila mtu hata akiwa kafiri na dhalimu. Hata hivyo katika upande mwingine, Mwenyezi Mungu SW ameapa kwamba, hatawafanyia hisani makafiri na madhalimu. Hivyo basi watu wa aina hii hupewa malipo yao hapa hapa dunia kwa kupata mauati mepesi. Katika uwanja huu Imam Ja'far Swadiq (as) aliulizwa kwamba, kwa nini baadhi ya wanadamu waumini, wasafi na wema hufariki dunia kwa mashaka na maumivu, wakati baadhi ya watu wasioshikamana na dini na watenda dhambi hufariki dunia na kutokwa roho kwa wepesi mno. Imam alisema: Mashaka yanayompata muumini wakati wa kufariki dunia ni kwa ajili ya kumuosha na kumtakasa na dhambi ili awasili katika Siku ya Kiyama akiwa safi na kupata malipo na thawabu za milele. Na wepesi wa mauati na kifo cha kafiri ni kwa ajili ya kumpa malipo ya amali zake njema hapa hapa duniani na hivyo aingie katika ulimwengu wa Akhera akiwa hana chochote isipokuwa madhambi yatakayomsababishia adhabu ya milele. (Biharul Anwar 6:153) Vilevile Imam Muhammad Baqir (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) amesimulia kisa kinachosema: Mmoja kati ya Mitume wa Banii Israil alikuwa akipita eneo moja ambako aliona mtu muumini akiwa katika hali ya kutokwa na roho. Nusu ya mwili wa bwana huyo ilikuwa chini ya ukuta uliomwangukia na nusu nyingine mwili wake ikiwa nje. Wakati huo huo wanyama walikuwa akinyofoa na kurarua mwili wa bwana huyo muumini. Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu aliona taswira hiyo na kupatwa na masikitiko makubwa. Akiwa njiani alifika katika mji mmoja na kuona kwamba, mtawala wake fasiki na dhalimu alikuwa amefariki dunia. Jeneza la mtawala huo muovu liliwekwa juu ya kitanda na kandokando yake kuliwekwa vyetezo vilivyokuwa vikifukiza hewani ubani na udi wenye harufu nzuri. Baada ya kuona mandhari hiyo, Mtume wa Banii Israil alimwambia Mwenyezi Mungu kwamba: Mola wangu! Nashuhudia kwamba wewe ni mtawala mwadilifu na humdhulumu yeyote. Bwana yule muumini ambaye hakukushirikisha na chochote hata mara moja umemkadiria mauati na hali ile ya kusikitisha, lakini mtawala huyu ambaye hakukuamini hata dakika moja amempa izza na utukufu namna hii. Nini sababu yake? Mwenyezi Mungu SW aliteremsha wahyi na ufunuo akisema: Ewe mja wangu! Kama ulivyosema, Mimi ni mtawala mwadilifu na simdhulumu yeyote. Bwana yule wa kwanza alikuwa na baadhi ya madhambi kwangu mimi na kwa sababu hiyo nimeyafanya mauti na kifo chake kwa namna hiyo ili yawe malipo na jazaa ya madhambi hayo; hivyo wakati atakapokuja kukutana na Mimi hatakuwa na dhambi yoyote. Na huyo bwana dhalimu alitenda baadhi ya mambo mema. Hivyo nimempa izza na heshima hii wakati wa kufariki dunia ili iwe malipo na jazaa yake kwa mema hayo na wakati atakapokuja kwangu hataomba malipo kwa jema lolote. Kundi la nne ni watenda dhambi ambao hutokwa roho na kufariki dunia kwa mashaka makubwa. Mashaka na maumivu haya huwa adhabu ya awali kwa watu wa aina hii ambayo huwapa ishara mbaya ya kuanza maisha ya adhabu na mashaka ya milele huko Akhera.