Ufufuo na Safari ya Kurejea kwa Allah (4)
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu ya tatu ya kipindi hiki Ufufuo na Safari ya Kurejea kwa Allah, kizungumzia athari chanya za imani ya ufufuo katika maisha ya mwanadamu. Ni matarajio yetu kwamba mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki.
Mpenzi msikilizaji, katika baadhi ya jamii ya mwanadamu, dini na itikadi za kidini huelezwa kuwa ni mambo mtu binafsi. Pamoja na hayo kumwamini Mwenyezi Mungu na ulimwengu wa Akhera ni masuala yenye nafasi na mchango mkubwa katika maisha ya mwanadamu. Kimsingi, katika fremu ya itikadi hiyo, maisha ya mwanadamu huwa na maana na malengo maalumu. Mitazamo, amali, nyendo na matendo ya mtu anayeamini ufufuo na Siku ya Mwisho yanatofautiana sana na ya mtu asiyeamini ufufuo na marejeo ya mwisho ya kiumbe huyo. Kadhalika mtu anayeamini ufufuo na Siku ya Kiyama huyafanya maisha yake ya duniani utangulizi wa kuelekea Akhera na hufanya juhudi kubwa kuhakikisha kwamba anapanda mbegu kwenye shamba hili la dunia ili apate mafanikio na mavuno bora katika maisha yasiyo na ukomo ya huko Akhera. Kwa mtazamo huo kila kitu hapa duniani huwa wenzo na chombo cha kuelekea kwenye ukamilifu, na maisha mwanadamu kama huyo huwa na nishati na kujenga matumaini.
Kuikumbatia dunia na kung'ang'ania maisha ya kimaada ni miongoni mwa mambo yanayosababisha kuwepo wasiwasi na kukosa utulivu kwa watu walio wengi. Kujishughulisha kupita kiasi na masuala ya kidunia, kwenyewe huwa sababu ya wasiwasi na misukosuko na ukosefu wa utulivu. Mtume Mtukufu Muhammad SAW anasema: 'Kuikumbatia sana dunia huzidisha huzuni na majonzi'. Imam Ali bin Abi Twalib (as) amesema: 'Mtu anayeiashiki dunia moyo wake hugubikwa na mambo matatu: Huzuni isiyoisha, tamaa ya kudumu na matarajio ya mambo asiyoweka kuyapata".
Wakati huo huo kuwa na imani ya ufufuo humpa mwanadamu utulivu wa moyo na matumaini ya kufika kwenye bara ya amani na uokovu. Mwanadamu anayeamini ufufuo hatopumbazika na ulimwengu huu wa kimaada, bali atakuwa na matumaini makubwa ya kuishi maisha mengine baada ya kufikwa na umauti.
Mpenzi msikilizaji, kuamini ufufuo na maisha ya Akhera licha ya kutoa dira na mwelekeo wa maisha, huwa na taathira kubwa katika malenzi ya mwanadamu. Imani na itikadi hiyo humpa mwanadamu ushujaa na ujasiri mkubwa kwa namna ambayo kamwe hayuko tayari kusalimu amri katika mazingira magumu na mashaka makubwa. Kuamini ufufuo na marejeo ya mja kwa Mwenyezi Mungu husababisha mabadiliko makubwa katika nyoyo na fikra za wanadamu kwa namna ambayo hawatetereshwi na mashinikizo wanayokumbana katika utekelezaji wa majukumu yao na huwa tayari kuyakaribisha kwa mikono miwili. Shakhsia na mtu kama huyo kamwe hawezi kusalimu amri mbele ya madhalimu, kwa sababu anaamini kwamba, amali yoyote ile nzuri au mbaya ina malipo na jazaa yake huko katika ulimwengu wa Akhera.
Mfano wa wazi wa taathira ya itikadi hiyo tunaweza kuuona kwa wachawi waliokusanywa na Firauni kwa ajili ya kukabiliana na Nabii Mussa (as). Wachawi hao walipouona muujiza wa Nabii Mussa (as) walitangaza waziwazi imani yao kwa Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume wake (as) bila ya kusita, licha ya kwamba Firauni alikuwa amewaahidi kuwafanya watu wa karibu yake zaidi kama wangemshinda Nabii Mussa (as). Hivyo, tunaona kwamba itikadi na imani waliyokuwa nayo wachawi ilitoa pigo kubwa kwa Firauni, kwa msingi huo alitoa vitisho vikali dhidi yao lakini hawakutetereka wala kuyumba katika Imani yao. Mwenyezi Mungu anaeleza misimamo na imani thabiti ya wachawi hao katika aya za 71 hadi 73 za Suratu Twaha akisema: (Firauni) akasema: Oh! Mnamwamini (Mussa) kabla sijakupeni ruhusa? Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliyekufundisheni uchawi. Basi kwa yakini nitakukateni mikono yenu na miguu yenu kwa kutafautisha. Na nitakutundikeni misalabani katika vigogo vya mitende, na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika sisi aliyemkali wa kuadhibu na kuiendeleza adhabu yake. Wakasema (wachawi): Hatutokukhitari wewe kuliko ishara waziwazi zilizotujia, na kuliko yule aliyetuumba. Basi hukumu utavyohukumu; kwani wewe unahukumu haya ya maisha ya duniani tu. Hakika sisi tumemwamini Mola wetu Mlezi ili atusamehe makosa yetu na uchawi uliotulazimisha kuufanya. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora na Mwenye kudumu zaidi.
Mpenzi msikilizaji, mwanadamu ana ghariza na matamanio mengi kama matamanio ya kijinsia, kupenda madaraka na cheo, utajiri na mengineyo ambayo iwapo hayatadhibitiwa huwenda yakasababisha ghasia na machafuko, kuvuruga misingi ya maisha na kuvunja utulivu na amani. Kumwamini Mwenyezi Mungu, Siku ya Mwisho na hesabu za amali na matendo yake Siku ya Kiyama ni miongoni mwa mambo muhimu yanayoweza kudhibiti matakwa na matamanio ya mwanadamu na hatimaye kumuongoza kwenye njia ya uongofu.
Mwandamu anayeamini ufufuo na maisha mengine baada ya kufariki dunia na akawa na yakini kwamba amali, nyendo na hata nia zake vinachunguzwa na kuhesabiwa, hawezi kufanya maovu, dhulma na ufisadi, kwa sababu anaelewa kwamba amali na matendo yake yote yanasajiliwa na kuandikwa na yana taathira katika maisha yake ya baada ya dunia hii.
Mwenyezi Mungu SW anatoa mifano mingi ndani ya Kitabu chake kitakatifu inayoonesha taathira za kimalezi za imani ya maadi na ufufuo katika kumwokoa wa mwanadamu kwenye vipindi vigumu na migogoro mikubwa. Qurani Tukufu inaelezea kisa cha Nabii Yussuf (as) na yaliyojiri kati ya Mtume huyo wa Allah na Zuleikha, na jinsi mwanamke huyo alivyomtaka Nabii Yusuf atekeleze matakwa yake. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 23 ya Suratu Yusuf akinukuu maneno ya Mtume wake huyo kwamba: "Najikinga na Mwenyezi Mungu. Huyu bwana wangu kaniweka maskani nzuri, na hakika wenye kudhulumu hawatengenekewi (yaani huko Akhera)". Katika maelezo haya ya Nabii Yusuf tunaona mambo mawili muhimu yaliyomkinga na Nabii huyo kutumbukia kwenye maasi. Mosi ni imani yake kwa Mwenyezi Mungu, na pili kuamini ufufuo na marejeo kwa Mola Muumba. Iwapo Yusuf (as) asingeamini mambo hayo mawili, kusingekuwepo sababu nyingine yoyote ya kumzuia asimkaribie Zuleikha na kutumbukia kwenye maasi.
Faida nyingine inayopatikana katika kuamini ufufuo na maisha ya baada ya umauti, ni kuirekebisha na kuilea jamii kimaadili. Itikadi ya kuwepo ulimwengu mwingine baada ya kifo na kubakia athari za matendo na amali zake ni sababu nyingine inayomfanya mwanadamu aweze kujizuia na kutenda dhambi na maovu. Taathira za kuamini kuwepo ulimwengu mwingine baada ya kifo katika kuwarekebisha mafisadi na watu waovu na kuwashajiisha watenda mema na wanaojitolea ni kubwa zaidi ya taathira za vyombo vya mahakama za kidunia. Kwa sababu miongoni mwa sifa za mahakama ya Siku ya Malipo ni kwamba katika mahakama hiyo hakuna kukata rufaa, hakuna upendeleo, hakuna hadaa wala hongo na mambo mengine mengi yanayoshuhudiwa katika mahakama za kidunia. Kwa msingi huo kuamini siku ya ufufuo kuna umuhimu na nafasi kubwa katika kurekebisha akhlaki na maadili ya jamii.
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabakatuh