May 23, 2016 09:58 UTC
  • Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain (123)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi kingine cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Katika kipindi kilichopita tulizungumzia aya za 59 na 83 za Surat an-Nisaa katika kujibu swali lililohusiana na udharura wa kuwepo Imam maasumu anayewaongoza Waislamu katika zama zote hadi Siku ya Kiama na hiyo ni baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw).

Katika kipindi hicho tulijadili moja ya sababu muhimu zaidi za udharura wa kuwepo Imam aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe kwa ajili ya kuwaongoza waja wake kwenye njia nyoofu. Aya hizi mbili zinabainisha wazi kwamba ni katika rehema zake Allah kwa waja wake kuwachagulia katika kila zama, Imam miongoni watukufu wenye madaraka kuwa marejeo yao muhimu katika kuwafafanulia sheria zake kutokana na kuwa ni watu maasumu yaani waliopewa kinga dhidi ya kufanya makosa ya aina yoyote ile. Kwa kufanya hivyo Imam huyo maasumu huwa amewaepusha kushawishika na kudhibitiwa na shetani ambaye daima hufanya hila na njama za kuzua na kueneza fitina, migawanyiko chuki na ugomvi miongoni mwao ili kuwazuia kufuata njia sahihi ya Mwenyezi Mungu. Hili ndilo jambo ambalo hadithi nyingi tukufu zinatubainishia na katika kipindi cha leo tutapa fursa ya kuzungumzia baadhi ya hadithi hizo, karibuni. 

************

Katika kitabu chake cha Maani al-Akhbar Sheikh Swaduq anamnukuu Imam Ali (as) kwamba alisema: ‘Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema: Mola wangu Mtukufu amenipasha habari kwamba amenijibu kupitia kwako (ewe Ali!) na washirika wako ambao watakuja baada yako.’ Ali (as) akasema: Nikasema, ewe Mtume wa Allah! Na hao washirika baada yangu ni akina nani?’ Mtume (saw) akasema: (Wao) ni wasii kutoka kwa Aali zangu. Watanikujia kwenye Hodhi, nao wote ni waongozaji walioongozwa na wala hawadhuriwi na wanaowadhalilisha. Wako pamoja na Qur’ani nayo Qur’ani iko pamoja nao. Hawatengani na Qur’ani wala Qur’ani kutengana nao. Umma wangu utanusuriwa kwa sababu yao na kubarikiwa mvua kwa ajili yao. Wataepushwa balaa na kujibiwa dua zao kwa baraka zao.’

Ni wazi kuwa kufungamana kwao na Qur’ani na Qur’ani kufungamana nao kuna maana kuwa kila wanalosema na kulitoa kwenye Qur’ani Tukufu huwa ni neno la Mwenyezi Mungu mwenyewe, ambalo hulitumia kwa ajili ya kutatua na kuondoa hitilafu na msuguano katika jamii ya Waislamu. Kwa njia hiyo Umma wa Muhammad (saw) huwa umeepushwa na hatari ya mabalaa na ushawishi wa shetani mlaaniwa na aliyefukuzwa na Mwenyezi Mungu.

********

Imenukuliwa katika kitabu cha Nahjul Balagha kinachobeba barua, hutuba na semi za hekima za Imam Ali (as) kwamba alisema katika kupinga hoja za Khawarij waliokuwa wakipinga hukumu ya watu (wanadamu): ‘Sisi hatukuwafanya watu kuwa mahakimu (wasuluhishi), bali tumeifanya Qur’ani kuwa hakimu. Na hii Qur’ani ni maandishi yaliyositiriwa kati ya jalada mbili, haitamki kwa ulimi, kwa hivyo hapana budi iwe na wafasiri. Wanaotamka kwa niaba yake ni watu tu. Na hawa jamaa walipotuita ili hukumu kati yetu iwe ni Qur’ani, hatujakuwa ni kundi linaloenda kinyume na Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume (4:59).’

Kisha Imam (as) akasema: ‘Hivyo kurejea kwa Mwenyezi Mungu ni kuhukumu kwa mujibu wa Kitabu chake, na kurejea kwa Mtume ni kutenda kwa mujibu wa Sunna zake. Endapo itahukumiwa kwa ukweli katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi sisi ni wenye haki zaidi katika watu, na endapo itahukumiwa kwa Sunna za Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) basi sisi ni wenye haki zaidi katika watu na tuko bora kuliko wao kwayo.’

Na katika hadithi nyingine ambayo imepokelewa kutoka kwake katika kitabu cha al-Ihtijaj, Imam Ali (as) anaashiria marejeo ya Mwenyezi Mungu ambayo yanatamka kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu ikiwa ni katika kutarjumu na kufasiri Kitabu na Sunna za Mtume wake (saw) ambapo anasema katika sehemu moja ya hadithi ndefu: Hakika Mwenyezi Mungu ameijalia elimu, watu wanaofaa na kuwafaradhishia waja utiifu kwao kwa kusema: Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi, na kwa kauli yake: Na lau wangelipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wangejua wale wanaochunguza katika wao (4:83).

**********

Ni wazi kuwa hatua ya Amir al-Mu’mineen Ali (as) kutumia aya mbili hizi kuthibitisha hoja yake, inaashiria kwamba marejeo ya Mwenyezi Mungu ambayo aliwaamuru wanadamu kuyarejea ni Maimamu maasumu ambao wana uwezo wa kuchambua na kubainisha hukumu ya Mwenyezi Mungu bila ya kuwepo uwezekano wa wao kufanya makosa katika hilo, na hivyo utiifu kwao kuwa ni utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake (saw). Kwa maelezo hayo wao ni watukufu na mawasii wa Mwenyezi Mungu kama alivyoashiria wazi suala hilo Imam Ali (as) mwishoni mwa hadithi yake kwa kusema kuwa wao ni mahujja wa Mwenyezi Mungu na hivyo kuulizwa na mmoja wa watu waliokuwa karibu yake: ‘Je, ni nani hao Mahujja?’

Imam (as) alimjibu kwa kumwambia: Ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na watu waliochukua nafasi yao katika mawasii wa Mwenyezi Mungu, nao wao ni wenye mamlaka ambao Mwenyezi Mungu amewafunganisha naye mwenyewe pamoja na Mtume wake na kuwalazimisha waja kuwatii na kusema kuhusiana nao: Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi, na pia Na lau wangelipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wangejua wale wanaochunguza katika wao.

Na mtu yule alipomuuliza Imam (as) maana ya ‘wenye mamlaka’ kwenye aya ya kwanza Imam alimjibu kwa kumwambia: ‘Ni amri ambayo huteremshwa na Malaika katika usiku ambao hutenganishwa kwayo (usiku huo) kila jambo lenye hekima katika viumbe, riziki, majaaliwa au jaala, matendo, umri, uhai, mauti, elimu ya ghaibu kuhusu mbingu na ardhi na miujiza ambayo haiwezi kufanywa ila na Mwenyezi Mungu, mawasii wake pamoja na Malaika waandishi baina ya Mwenyezi Mungu na viumbe wake.’

Na hatimaye tunanukuu kutoka kitabu cha al-Ihtijaj kauli ya Bwana wa Mashahidi Abi Abdillah al-Hussein (as) ambapo anasema katika hotuba: ‘Sisi ndio kundi la Mwenyezi Mungu lenye kushinda, kizazi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu kilicho karibu, Ahlu Beit wake wema na moja ya Vizito Viwili. Mtume wa Mweyezi Mungu (saw) alitujaalia kuwa kitu cha pili baada ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambacho (Kitabu) kina ufafanuzi wa kila jambo, na ambacho tumekabidhiwa sisi kwa ajili ya kukifasiri. Ufafanuzi wake haupunguzi kasi yetu bali tunafuata hakika zake…..’ Kisha akasema (as): Basi tutiini kwa sababu utiifu kwetu ni faradhi, kwa sababu umefungamanishwa na utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na amesema pia: Na lau wangelipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka katika wao, wangejua wale wanaochunguza katika wao. Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema Yake mngemfuata shetani ila wachache wenu tu.. Kwa hivyo ninakutahadharisheni kusikiliza makelele ya shetani kwa sababu yeye ni adui wenu aliye wazi….’

**********

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipidi hiki cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain mlichokisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa mmenufaika vya kutosha na yale mliyoyasikia. Basi hadi juma lijalo panapo maaliwa tunakuageni nyote ndugu wapendwa kwa kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warhmatullahi Wanarakatuh.