'Tiba ya Kiajemi' yaingia katika kamusi ya kimataifa ya tiba
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia matukio mbali mbali ya sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa utanufaika.
Kamusi ya kitiba ya Medical Subject Headings (MeSH) imeongeza 'Tiba ya Kiajemi' kama moja ya misamiati yake ya wale wanaotafuta makala, vitabu au taarifa zingine zote za kitiba.
Kujumuishwa 'Tiba ya Kiajemi' au Tiba ya Kiirani katika kamusi hiyo ya kitiba ya kimataifa ni hatua muhimu katika kutambua tiba ya jadi na asili ya Iran, amesema Armna Zargaran wa Wizara ya Afya ya Iran.
Ameongeza kuwa, miaka miwili iliyopita Idara ya Tiba ya Kisasa na Tiba ya Jadi ya Kiajemi katika Wizara ya Afya ilianza jitihada za kuhakikisha Tiba ya Kiajemi inawekwa katika kamusi hiyo ya kimataifa.
Ameitaja hatua hiyo kuwa ni muhimu katika kuhakikisha kuwa tiba ya jadi ya Kiirani inatambuliwa kama sehemu rasmi ya sayansi ya tiba kimataifa.
Ameashiria pia ushirikiano wa karibu baina ya Iran na Shirika la Afya Duniani katika elimu na utafiti huku akisisitiza haja ya kutumiwa uwezo uliopo katika tiba ya jadi ya Kiirani katika kutoa huduma bora za kitiba na kiafya.
Tiba ya jadi ya Kiirani ni moja ya tiba za kale zaidi duniani na msingi wake ni ule uliowekwa na wanasayansi maarufu wa Kiislamu ambao ni Muḥammad ibn Zakariyyāʾ al-Rāzī ambaye Wamagharibi wanamuita Rhazes na Abu Ali Sina ambaye katika ulimwengu wa Magharibi anajulikana kama Avicenna.
Tiba ya jadi ya Kiirani husisitiza zaidi kudumishwa afya njama na kuzuia magonjwa ili mwanadamu asihitajie matibabu.
Hivi sasa kote duniani kuna mimea karibu 30,000 ya tiba za jadi ambapo nchini Iran pekee kuna mimea 8000 ya kitiba na hivyo kuifanya nchi hii kuwa na anuai kubwa ya mimea ya kitiba kuliko bara lote la Ulaya.
Wataalamu wanasema kujumuishwa dawa za jadi katika mifumo ya afya sambamba na kuhakikisha zinaendana na ubora wa dawa za kisasa ni jambo linaloweza kupelekea watu wote wapate huduma za afya.
@@@@
Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii, ECOSOC, Collen Vixen Kelapile ameiteua nchi ya Tanzania kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Jukwaa la Saba la Wadau Mbalimbali wa Masuala ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi katika kutekeleza Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, SDGs.
Rais wa ECOSOC pia amemteua Balozi Profesa Kennedy Gastorn ambaye ni Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, na Balozi Sergiy Kyslytsya, Mwakilishi wa Kudumu wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa kuwa wenyeviti wa jukwaa hilo.
Akizungumza na waandishi habari wa Umoja wa Mataifa baada ya uteuzi huo, Balozi Gastorn amesema ni heshima kubwa sana kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweza kupata nafasi hii kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Jukwaa hili.
Ameongeza kuwa, “pamoja na mambo mengine hii ni ishara ya jinsi ambavyo Tanzania na diplomasia yake inazidi kukubalika katika macho ya kimataifa chini ya uongozi wa mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."
Amesema Tanzania kama mwanachama mwingine katika Umoja wa Mataifa, itaitumia nafasi hiyo kubadilishana uzoefu na kuonesha mipango yake, mafanikio na changamoto katika sekta hiyo na kuweza kukuza uhusiano na kubadilishana uzoefu na wadau wengine kimataifa.
Hali kadhalika Balozi Gastorn amebaini kuwa, kama mwenyekiti mweza, Tanzania itatumia nafasi hiyo kuwaunganisha wadau wa masuala ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi katika kutekeleza ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 ya Umoja wa Mataifa.
Akifafanua madhumuni ya jukwaa hilo la wadau wa masuala ya Sayansi, Teknolojia na Uvumbuzi, Balozi Gastorn amesema, “madhumuni ya jukwaa hili ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wa masuala ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi ili kujadili na kubadilishana uzoefu kwa namna masuala hayo yanavyoweza kurahisisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, SDGs ya mwaka 2030.”
\\\\\\\\
Serikali ya Tanzania imezindua mradi wa maabara ya akili bandia au akili ya kubuni (artificial intelligence) utakaosaidia kurahisisha shughuli za maendeleo nchini.
Hayo yalisemwa Jumatatu Januari 24, 2022 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis akizindua mradi huo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
“Kama hivi wengi tunavyoangalia dunia za sasa hivi wenzetu wameshakwenda mbele zaidi. Sometimes (wakati mwingine) unakuta watu wanavyokwenda makazini wanajibiwa na robot, unapopanda lifti, mwendo kazi,” amesema.
Naibu Waziri huyo amesema teknolojia hiyo inatumika hata mashambani ambapo badala ya kwenda mtu linatumika robot na maofisini.
Amesema kwa nchini ni maabara ya pili kuanzishwa ambapo hivi sasa wapo katika utafiti wa kuangalia ni jinsi gani teknolojia hiyo mpya inavyoweza kutumika.
Abdullah amesema ni vyuo viwili ambavyo vimeingia katika mradi huo ambavyo ni Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha jijini Arusha na Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Makamu Mkuu wa Chuo cha Nelson Mandela, Profesa Emmanuel Luoga amesema mradi huo mkubwa wa kisayansi utakasaidia maendeleo.
“Tunajua katika nchi yetu tunaelekea katika uchumi wa kidigitali, mapinduzi ya nne ya viwanda haya yote hayawezi kutekelezeka bila matumizi ya Tehama. Akili Bandia ni moja ya akili za juu katika kuleta mapinduzi katika viwanda,”amesema.
Kiongozi wa mradi huo katika chuo cha Udom, Dk Ally Nyamawe amesema mradi huo una nguzo tatu ambazo ni kufanya tafiti, mafunzo na ubunifu.
“Mradi unatarajia kutoa mafunzo kwa wanafunzi wawili wa PHD (shahada ya udaktari) na wawili wa masters (shahada ya uzamivu),” amesema.
@@@
Na utafiti mpya umebaini kuwa MWANAUME anayeishi maisha ya ukapera baada ya kutalikiana na mkewe yuko katika hatari kubwa ya kusumbuliwa na magonjwa hatari kama vile maradhi ya moyo.
Wataalamu wanasema kuwa wanaume huathirika zaidi kiafya ndoa inapofikia tamati ikilinganishwa na wanawake.
Afya hudorora zaidi iwapo ataachwa na wanawake zaidi ya wawili, kwa mujibu wa watafiti.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Copenhagen nchini Denmark, na ripoti yake kuchapishwa katika jarida la Journal of Epidemiology and Community Health hivi majuzi, ulibaini kuwa wanaume wanaokaa kwa muda mrefu bila kuoa kufuatia kuvunjika kwa ndoa ya awali, pia wanakuwa katika hatari ya kupatwa na msongo wa akili, kusahau mambo kwa urahisi (dementia) na kudorora kwa kingamwili (immunity).
Utafiti huo ulifanywa miongoni mwa watu 4,835 ndani ya miaka 26.
Wataalamu wanasema kuwa ndoa, haswa miongoni mwa vijana zimekuwa zikivunjika baada ya muda mfupi kwa sababu wahusika wanakimbilia kuoana bila kupata ushauri nasaha.
Baadhi ya wanandoa kwa mujibu wa wataalamu, wanapendelea kunyamaziana wanapokosana badala ya kuzungumzia tatizo lililopo na kuelewana.
Mitandao ya kijamii pia imelaumiwa kwa kuchochea wanandoa kuwa na ‘mipango ya kando’ hivyo kutia ndoa au uhusiano wa kimapenzi hatarini.
@@@
Naam wapenzi wasikilizaji na hadi hapo ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya sayansi na teknolojia.