Jumatano, Machi 2, 2022
Leo ni Jumatano tarehe 28 Rajab 1443 Hijria sawa na tarehe Pili Machi 2022 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1383 iliyopita, msafara wa Imam Hussein (as), ulianza safari yake kutoka mjini Madina. Hatua hiyo ilitanguliwa na kuaga dunia Muawiya bin Abi Sufiyan hapo tarehe 15 ya mwezi huo huo wa Rajab na nafasi yake ikachukuliwa na mwanaye, Yazid bin Muawiya. Yazidi alimtaka mtawala wa Madina amlazimishe Imam Hussein ili atoe baia na mkono wa utiifu kwa ajili yake na endapo angekataa, basi amuue. Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa Imam Hussein alikuwa akijua vyema kwamba Yazidi ni mtu muovu na fasiki, alikataa kutoa baia na mkono wa utiifu kwa kiongozi huyo na akaamua kuondoka Madina kuelekea Makka, akiwa na watu wa familia ya Mtume na idadi ndogo ya wafuasi wake.

Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita sawa na tarehe Pili Machi mwaka 1896 mwanafikizia wa Kifaransa Henri Becquerel alivumbua nururishi au Radioactivity baada ya kufanya utafiti katika mada za urani na vitu vinginevyo. Becquerel alikuwa akichunguza urani ndipo alipogundua nururishi. Utafiti wa mwanafikizia huyo wa Kifaransa ulimfanya atunukiwe tuzo ya Nobel mwaka 1903 na miaka mitano baadae aliaga dunia.

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita, sawa na tarehe 28 Rajab mwaka 1337 Hijria, alifariki dunia Ayatullahil Udhma Muhammad Kadhim Tabatabai Yazdi maarufu kwa jina la Allamah Yazdi, msomi mashuhuri wa Kiirani. Allamah Yazdi alipatia elimu ya kidini nchini Iran na huko katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq, kutoka kwa maulamaa kadhaa mashuhuri akiwemo Mirza Shirazi na kufikia daraja ya Ijtihad. Msomi huyo ameandika vitabu vingi, kikiwemo kitabu cha 'al U'rwatul Wuthqaa.

Miaka 66 iliyopita katika siku kama hii, nchi ya Morocco ilipata uhuru. Morocco iko kaskazini mwa Afrika katika Ukingo wa Bahari ya Mediterrania na Bahari ya Antlantic na inapakana na Algeria na Sahara Magharibi. Morocco ilikombolewa na Waislamu mwishoni mwa karne ya Saba Miladia na silsila kadhaa za kifalme zilitawala nchini humo. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Morocco dhidi ya wakoloni wa Uhispania na Ufaransa yalipelekea nchi hiyo kupata uhuru mwaka 1956.

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, mwafaka na tarehe Pili Machi mwaka 2004, mamia ya watu wasio na hatia waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika miripuko kadhaa mikubwa iliyotokea katika shughuli ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) huko katika miji mitukufu ya Karbala na Kadhimein nchini Iraq. Katika mwaka huo wananchi Waislamu wa Iraq walifanya maadhimisho hayo kwa hamasa kubwa baada ya utawala wa Saddam Hussein, dikteta wa zamani wa nchi hiyo aliyeng'olewa madarakani, kupiga marufuku kwa miaka kadhaa shughuli zote za aina hiyo. Miripuko hiyo ya kigaidi ya Karbala na Khadhimein ilitokea ikiwa ni muendelezo wa machafuko yaliyoikumba Iraq tangu nchi hiyo ivamiwe kijeshi na kukaliwa kwa mabavu na Marekani na Uingereza mwaka 2003.
