Mar 26, 2022 03:07 UTC
  • Jumamosi, 26 Machi, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 23 Shaaban 1443 Hijria, sawa na tarehe 26 Machi 2022 Miladia.

Siku kama ya leo Miaka 1139 iliyopita, Abu Muhammad Hassan bin Ali Utrush aliyepewa lakabu ya Nassir Kabir na ambaye alikuwa mwanazuoni na mwanapambano mashuhuri katika wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw) aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 230 Hijiria mjini Madina na kubaidishiwa mjini Samarra huko kaskazini mwa mji wa Baghdad nchini Iraq na wafalme wa Bani Abbas akiwa na idadi kadhaa ya watu wa ukoo wa Mtukufu Mtume akiwemo Imam Hassan Askari (as) na baba yake Hassan Utrush. Alijifunza elimu za kidini mjini Baghdad na Kufa na kutokea kuwa mwanazuoni mashuhuri katika elimu hizo. Alijishughulisha na masuala ya kisiasa pia ambapo alikuwa na nafasi muhimu katika kipindi cha mapambano na kusimamishwa dola la Maalawi huko Tabarestan kaskazini mwa Iran. Alifanya juhudi kubwa za kueneza dini ya babu yake, Mtume Mtukufu (saw) ambapo aliwaingiza makumi ya maelfu ya watu katika dini tukufu ya Uislamu. Aliandika pia vitabu vingi katika uwanja huo vikiwemo vya al-Basit, Tafsir al-Utrush na al-Imamatul Kabir. ***

Abu Muhammad Hassan bin Ali Utrush aliyepewa lakabu ya Nassir Kabir

Katika siku kama hii ya leo miaka 111 iliyopita alizaliwa mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Marekani, Tennessee Williams. Alivutiwa sana na fasihi na mvuto huo ulikolea na kuimarika zaidi wakati alipokuwa masomoni katika chuo kikuu na hatimaye alifanikiwa kuwa mwandishi mkubwa. Tennessee Williams alitumia uhodari wake kueleza fikra zake kwa lugha ya michezo ya kuigiza. Kazi zake nyingi zilieleza hali ya watu wa tabaka la chini na wanaosumbuliwa na ukata katika jamii ya Marekani. Miongoni mwa kazi za mwandishi huyo mashuhuri ni Cat on a Hot Tin Roof, Sweet Bird of Youth na The Glass Menagerie. ***

Tennessee Williams

Miaka 70 iliyopita katika siku kama ya leo, yalianza mapambano ya Mau-Mau yakiongozwa na Mzee Jomo Kenyatta, mwasisi wa nchi huru ya Kenya, dhidi ya wakoloni wa Kiingereza. Katika kipindi cha vita viwili vikubwa vya dunia, Kenya ilikumbwa na machafuko na vurugu nyingi. Hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wananchi wa nchi hiyo waliamua kupambana kufa na kupona ili kuikomboa nchi yao kutoka mikononi mwa wakoloni wa Ulaya. Wakoloni wa Kiingereza waliweka sheria kali katika maeneo tofauti ya Kenya hasa katika maeneo ya Wakikuyu lakini hilo halikuzuia kuasisiwa harakati ya Mau-Mau. Kaulimbiu kuu ya wapiganaji wa Mau-Mau ilikuwa ni kuweko usawa na uadilifu katika masuala ya kijamii na kisiasa baina ya wenyeji wa Kenya na Wazungu. Hatimaye harakati hiyo ya Mau-Mau kwa uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta ilifanikiwa kuikomboa Kenya kutoka mikononi mwa wakoloni wa Kiingereza mwanzoni mwa muongo wa 60. 

Mzee Jomo Kenyatta, mwasisi wa nchi huru ya Kenya, dhidi ya wakoloni wa Kiingereza

Tarehe 26 Machi mwaka 1971 katika siku kama hii ya leo, Pakistan Mashariki ambayo hivi sasa inajulikana kwa jina la Bangladesh iliamua kujitenga na Pakistan baada ya kuzuka mivutano mikubwa ya kisiasa na uasi nchini humo. Pakistan Mashariki na ile ya Magharibi ilikuwa nchi moja, iliyoamua kujitenga na India mwaka 1947. Wabangladeshi waliokuwa wakiishi Pakistan Mashariki na kuunda jumla ya asilimia 98 ya watu wa eneo hilo, hawakuridhishwa na vitendo vya kibaguzi vilivyokuwa vikifanywa na serikali kuu huko Pakistan Magharibi na kwa msingi huo awali walitaka kupewa mamlaka ya kujiendeshea mambo yao wenyewe. Baadaye walianzisha mapambano ya silaha na kufanikiwa kulifukuza jeshi la Pakistan Magharibi wakisaidiwa na jeshi la India. Pakistani Mashariki ilipewa jina la Bangladesh. 

Bendera ya Bangladesh

Na miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ahmad Sekou Toure kiongozi mkubwa wa nchi ya Kiafrika ya Guinea. Sekou Toure alizaliwa Januari 9 mwaka 1922 katika moja ya miji ya katikati mwa Guinea. Aliingia katika harakati za kisiasa akiwa katika rika la ujana na alikuwa akitaka uhuru wa  chi yake kutoka kwa wakoloni wa Kifaransa. Hatimaye mwaka 1958 nchi hiyo ilipata uhuru na mwaka mmoja baadaye Touré akateuliwa kuwa rais na kusalia madarakani hadi mwaka 1984 alipofariki dunia. 

Ahmed Sékou Touré

 

Tags