Jumatatu, Machi 28, 2022
Leo ni Jumatatu tarehe 25 Shaaban 1443 Hijria sawa na 28 Machi 2022 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1306 iliyopita, aliuawa kamanda wa Kiiran, Abu Muslim Khorasani, kwa amri ya Mansur, aliyekuwa mtawala wa wakati huo wa Bani Abbasi. Abu Muslim Khorasani alikuwa kiongozi wa harakati liyopewa jina la 'Siah Jamegan' huko Khorasan ambayo ilianzisha uasi dhidi ya mtawala dhalimu wa Bani Umayyah. Katika kipindi kifupi watu wengi wa vijiji na miji mingi ya Khorasani walijiunga na kundi hilo. Baada ya vita vingi Abu Muslim na wafuasi wake walifanikiwa kuwashinda watawala hao wa Bani Umayyah. Kwa utaratibu huo kuliandaliwa uwanja wa kuhitimisha kabisa utawala wa Bani Umayyah na kuingia madarakani watawala wa Bani Abbas. Katika kipindi hicho Abu Muslim Khorasani alikuwa na nafasi kubwa kiasi cha kumfanya Mansur, mtawala wa ukoo wa Bani Abbas kujawa na hofu kubwa. Kwa sababu hiyo alipanga njama ya kumuua. Baada ya mauaji hayo wafuasi wa Abu Muslim Khurasani walianzisha mapambano na kulipiza kisasi cha damu yake na mapimbano hayo yaliendelea kwa muda mrefu.
Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita, alizaliwa mwandishi mashuhuri wa Russia Alexei Maximovich Peshkov aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Maksim Gorky. Gorky alilazimika kusoma na wakati huo huo akifanya kazi ili kuweza kukidhi mahitaji yake ya maisha kutokana na umaskini mkubwa uliokuwa ukimkabili. Alianza kuandika riwaya haraka sana na kufanikiwa kuchapisha riwaya yake ya kwanza katika gazeti la Tbilisi wakati alipokuwa akifanya kazi katika sekta ya reli. Miaka miwili baadaye mwandishi Gorky alipata mafanikio makubwa ambapo alichapisha riwaya yake katika kitabu na taratibu akaanza kuingia katika safu ya waandishi wakubwa na mashuhuri duniani.
Katika siku kama leo miaka 83 iliyopita, baada ya kupita karibu miaka miwili na nusu ya vita vya ndani huko Uhispania, wapigania usultani chini ya uongozi wa Jenerali Francisco Franco waliwashinda wapigania jamhuri na kudhibiti Madrid, mji mkuu wa nchi hiyo. Machafuko yalianza huko Uhispania wakati Alphonso wa 13 mfalme dikteta wa nchi hiyo alipolazimika kujiuzulu kufuatia mashinikizo ya wapigania jamhuri na baadaye mfumo wa jamhuri ukaasisiwa huko Uhispania.
Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita mwandishi wa Kiingereza, Bi Virginia Woolf aliaga dunia kwa kujiua. Woolf alizaliwa mwaka 1882 na alianza kufaidika na maktaba binafsi ya baba yake ambaye alikuwa mwandishi na mkosoaji wa fasihi, akiwa bado mtoto. Virginia Woolf alianza kuandika vitabu mapema na miongoni mwa vitabu hivyo ni Mrs. Dalloway, The Waves na To the Lighthouse. Hata hivyo maradhi ya kiakili na kinafsi yaliyompata akiwa bado kijana yaliendelea kumuandama na hatimaye mwandishi huyo wa Uingereza aliamua kujiua katika siku kama hii ya leo.