Jumanne, tarehe 5 Aprili, 2022
Leo ni Jumanne tarehe 3 Ramadhani 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 2022.
Siku kama ya leo miaka 1030 ilyopita inayosadifiana na tarehe 3 Ramadhani 413 Hijria, alifariki dunia Muhammad bin Nu'uman maarufu kwa lakabu ya Sheikh Mufiid, faqihi, mtaalamu wa elimu ya Hadithi, Qurani Tukufu na historia ya Kiislamu. Sheikh Mufid alikuwa hodari na mwanafikra aliyepevuka, kwani aliweza kujibu masuala ya kifiqihi kwenye midahalo kulingana na madhehebu yoyote aliyotakiwa kufanya hivyo. Kutokana na uhodari wake huo, maulamaa wengi wa Kiislamu katika zama hizo walimpa lakabu ya Mufiid. Sheikh Mufiid ameandika vitabu vingi miongoni mwa hivyo, ni al Kalaam Fii Dalaailil Quran', al Arkaan' naKashful Saraair'.

Siku kama ya leo miaka 437 iliyoyopita yaani 5 Aprili 1585, yalifanyika mauaji ya halaiki katika mji wa Harlem nchini Uholanzi, ambacho kilikuwa kitovu cha wapigania uhuru nchini humo. Mauaji hayo yalifanyika kwa amri ya Mfalme wa Uhispania. Jumla ya watu elfu sita wanaaminika kuwa waliuawa kwenye shambulio hilo. Hatimaye Uholanzi ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Uhispania hapo mwaka 1609.

Tarehe 5 Aprili 228 iliyopita, aliuawa Georges Danton mmoja kati ya viongozi wa mapinduzi ya Ufaransa. Danton licha ya kusomea taaluma ya sheria, alikuwa mhamasishaji mzuri katika kipindi cha mapinduzi ya Ufaransa. Danton alikuwa akiamini kuwa, sanjari na kuzuia machafuko na maafa ya kibinadamu, utawala wa kifalme nchini Ufaransa ulipaswa kutokomezwa. Amma Robes Pierre mmoja kati ya vinara wakubwa wa mapinduzi ya Ufaransa ambaye pia alikuwa mshindani wa Danton alichukua uamuzi wa kimtia mbaroni Danton na hatimaye kumuuwa.
Na siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Aprili 1956, yalimalizika mashambulizi ya kinyama ya majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza. Majeshi hayo, tarehe 4 Aprili, yalianza kufanya mashambulio makubwa na kuwauwa watu 56 na kuwajeruhi wengine 30 wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee katika kipindi cha siku mbili. Nchi za Magharibi na jamii ya kimataifa hazikutoa radiamali yoyote kuhusiana na jinai hizo za Wazayuni.