Apr 08, 2022 21:48 UTC
  • Jumamosi, Aprili 9, 2022

Leo ni Jumamosi, tarehe 7 Ramadhani 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 9 Aprili mwaka 2022 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1433 iliyopita yaani tarehe 7 Ramadhan mwaka wa 10 tangu kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad (saw), kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, aliaga dunia Abu Talib, ami na mtetezi mkubwa wa Mtume (saw) katika mji wa Makka. Baada ya kufariki dunia Abdul Muttalib, babu mtukufu wa Nabii Muhammad (saw), Abu Talib ndiye aliyebeba jukumu la kumlea Mtume na akawa bega kwa bega na mwana huyo wa nduguye katika hali zote. Baada ya kupewa Utume Nabii Muhammad (saw), Abu Talib hakumwacha mkono mtukufu huyo na alisimama imara kukabiliana na washirikina wa Kikureishi. Lakini baada ya kufariki dunia Abu Talib washirikina walishadidisha maudhi na manyanyaso yao dhidi ya Bwana Mtume (saw), kiasi kwamba kutokana na hali ngumu mno iliyomkabili, hatimaye kwa amri ya Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo alilazimika kuhama Makka na kwenda kuhamia Madina ambako aliasisi utawala wa kwanza wa Kiislamu.

 

Siku kama ya leo miaka 1240 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Ma'mun, khalifa wa utawala wa Bani Abbas alimlazimisha Imam Ridha (as) kukubali matakwa yake ya kuwa mrithi wa kiti cha ufalme baada yake. Ni vyema kuashiria kuwa uadui wa watawala wa kizazi cha Bani Umayyah na Bani Abbas dhidi ya Ahlul Bait wa Mutume (saw) ni wa muda mrefu. Vizazi hivyo viwili ni maarufu kwa dhulma, ukandamizaji na utesaji dhidi ya Ahlul Bait wa Mtume, ambapo havikusita hata kuwaua maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume wa Allah. Baada ya Ma'mun kutwaa madaraka ya ukhalifa alihofia sana taathira chanya ya Imam Ridha (as) kwa watu na kwa kuwa alikusudia kumuweka mtukufu huyo chini ya uangalizi wake mkali, huku akijionyesha kuwa ni mwenye mapenzi kwa Watu wa Nyumba ya Mtume, hivyo alitoa amri ya kumuondoa Imam Ridha kutoka mjini Madina na kumpeleka Khorasan (Mash'had ya leo) na kisha akamlazimisha kukubali kuwa mrithi wa kiti cha ufalme. Siku kama ya leo, yaani tarehe 7 Ramadhan mwaka 201 Hijiria, khalifa huyo aliwasilisha mbele ya mtukufu huyo suala hilo ambapo hata hivyo alilipinga. Baada ya kulipinga, mtawala huyo dhalimu alitumia vitisho dhidi ya Imam Ridha (as) ambapo baadaye alikubali tu kwa kutikisa kichwa huku mtukufu huyo akisisitiza kuwa jambo hilo halitofikiwa. Baada ya hapo mtukufu huyo alitumia fursa hiyo kueneza mafundisho sahihi ya dini ya Uislamu suala ambalo baadaye lilimfanya Ma'mun kuchukizwa na hatua yake ya kumtoa mjini Madina na ni baada ya hapo pia ndipo alipopanga njama ya kumuua, njama ambayo ilitekelezwa siku ya tarehe 30 Safar mwaka 203 Hijiria.

Haram ya Imam Ridha AS mjini Mash'had, Iran

 

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Milaadia, utawala ghasibu wa Israel ulifanya mauaji ya kinyama katika kijiji cha Deir Yassin huko magharibi mwa Baitul Muqaddas. Mauaji hayo yalifanyika wakati wa vita vya kwanza vya Waarabu na Israel na yalitekelezwa na Wazayuni wa kundi la Irgun lililokuwa likiongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Israel Menachem Begin. Eneo la Dier Yassin lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Wazayuni kutokana na kuwa katika njia ya Baitul Muqaddas na karibu na pwani. Baada ya kukivamia kijiji cha Deir Yassin, Wazayuni hao waliwaua kinyama wakazi 270 ambao hawakuwa na hatia yoyote wa kijiji hicho. Mauaji hayo yaliwalazimisha Wapalestina wengi wa eneo hilo kukimbia makazi yao kwa kuhofia kukaririwa mauaji kama hayo ya kinyama.

Mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Wazayuni makatili huko Deir Yasin, Palestina

 

Tarehe 9 Aprili miaka 30 iliyopita Waserbia wa Bosnia waliokuwa wakiungwa mkono na kusaidiwa na dikteta wa zamani wa Yugoslavia Slobodan Milosevic, walianza mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo katika mji wa Belgrade. Mauaji hayo yalianza baada ya kutangazwa matokeo ya kura ya maoni hapo tarehe Mosi Machi 1992 ambayo kwa mujibu wake asilimia 99 ya washiriki walipiga kura ya kujitenga Bosnia Herzegovina na Yugoslavia ya zamani. Hata hivyo Waserbia wachache wa Bosnia walipinga suala hilo la kuanzisha uasi kisha baadaye wakajitangazia mamlaka ya Seribia katika maeneo yao. Milosevic aliwaunga mkono Waserbia na kuanzisha vita vikubwa zaidi vya mauaji ya kimbari barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Hadi vita hivyo vinamalizika mwaka 1995 zaidi ya Waislamu laki moja wa Bosnia walikuwa wameuawa kwa umati. Zaidi ya Waislamu wengine milioni mbili pia walilazimika kuwa wakimbizi.

Slobodan Milosevic

 

Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, iliyosadifiana na tarehe 20 Farvardin 1385 Hijria Shamsia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanikiwa kupata teknolojia ya kurutubisha madini ya urani kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Wasomi na wataalamu wa Iran walifanikiwa kukamilisha mfumo wa kuzalisha nishati ya nyuklia licha ya mbinyo na vikwazo vya nchi za kibeberu. Kwa utaratibu huo Iran iliingia katika kundi la nchi zenye teknolojia ya nyuklia duniani. Mwaka mmoja baadaye Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kuzalisha nishati hiyo viwandani. Mafanikio hayo makubwa ya Iran yalipatikana chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata hivyo baadhi ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinapinga vikali miradi ya nishati ya nyuklia ya Iran kutokana na sera zao za kindumakuwili na za kibaguzi.

Mchakato wa kurutubisha urani nchini Iran