Sayansi na Teknolojia
Metaverse ya Kiislamu kuanza kutumika
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknoljia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Kati ya tuliyonayo leo ni ustawi wa Iran katika anga za mbali, metaverse ya Kiislamu na ugonjwa wa monkeypox
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Issa Zarepour amesema, Iran ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazotengeneza na kurusha satelaiti katika anga za mbali na kusisitiza kuwa sekta hiyo inailetea Iran nguvu na teknolojia mpya.
Zarehpour amesema: Iran imepata maarifa na teknolojia ya hali ya juu zaidi katika uga wa anga za mbali katika kilele cha vikwazo na matatizo, kwa kadiri kwamba imefanikiwa kutengeneza satelaiti na makombora ya kurushia satelaiti ambayo yanazifikisha satelaiti hizo katika maeneo yaliyokusudiwa angani kwa usahihi na umakinifu mkubwa.
Huku akibainisha kuwa nchi kama Uingereza kwa hivi sasa bado zinaitegemea Russia kuzirushia satelaiti, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran amesema ni fahari kubwa kwamba hii leo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajivunia kuwa moja ya nchi zilizo na uwezo mkubwa na teknolojia ya kisasa kabisa katika uwanja huo.
Katika kilele cha vikwazo na matatizo, Iran imepata maarifa na teknolojia ya hali ya juu zaidi katika uwanja wa anga za juu ambayo inaiwezesha kujitengenezea satelaiti na makombora ya kurushia satelaiti na kuziweka kwa usahihi na ustadi mkubwa katika maeneo yanayolengwa angani.
Katika miongo minne iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua kubwa za maendeleo katika uga wa kujipatia teknolojia ya makombora yanayofika katika anga za mbali. Hata kama maadui wamejaribu kukwamisha maendeleo ya kiuchumi na kisayansi ya Iran, ikiwemo sekta ya anga za mbali, kupitia vikwazo mbalimbali, lakini licha ya vikwazo na mashinikizo hayo yote, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa pakubwa kupata teknolojia mbalimbali za masuala ya anga za mbali, jambo ambalo linapaswa kuchukuliwa kuwa ni maendeleo makubwa kwa Iran ya Kiislamu.

Wakati huo huo, Maonyesho ya Pili ya Kimataifa ya Tekneoljia ya Habari na Mawasiliano ya Kish (KITEX) yamefanyika kuanzia Mei 9-12 katika Kisiwa cha Kish kusini mwa Iran. Maonyesho ya mwaka huu yalijikita zaidi katika akili za kubuni au Artificial Intelligence, Intaneti katika Vitu (IoT), miji erevu, teknolojia ya fedha za kidijitali au blockchain na vyombo vya habari vya kidijitali. Makampuni zaidi ya 190 katika sekta za sayansi na teknolojia yalishiriki na kuonyesh abidhaa na huduma mpya. Maonyesho hayo yanalenga kuwasilisha bidhaa za sayansi na teknolojia nchini Iran katika soko la dunia na hivyo kuipa nchi hii pato la fedha za kigeni.
Wageni kutoka nchi mbali mbali duniani wamealikwa katika Maonyesho ya Pili ya Kimataifa ya Tekneoljia ya Habari na Mawasiliano ya Kish. Kati ya nchi jirani zilizoshirki katika maonyesho hayo ni Qatar, Oman na Syria.
Shirika moja la masuala ya uchumi wa Kiislamu limetangaza kuzindua Metaverse ya kwanza ya Kiislamu ambayo inaenda sambamba na mafundisho ya Kiislamu.
Shirika la IBF.NET limesema litapanua shughuli zake za kiuchumi mitandaoni kwa kuzindua metaverse aina mbili, moja ya masomo na nyingine itakuwa ni soko.
Wazo la metaverse ya Kiislamu liliwasilishwa kwa mara ya kwanza katika makala iliyotumwa katika blogu ya IBF NET na baadaye mchakato wa utekelezaji wake ukaanza.
Je, metaverse ni nini? Kwa kifupi ni kuwa, metaverse ni ulimwengu mpya wa kidijitali ambapo watu wanaweza kuishi pamoja kwa njia ya intaneti. Maana yake ni kuwa, ni ulimwengu wa kidijitali na kwa msingi huo haupo katika mazingira ya kweli, upo katika mtandao.
Weledi wa masuala ya teknolojia wanasema metaverse ni hatua inayofata ya ustawi wa intaneti na teknolojia hii inajumuisha teknolojia inayojulikana kama uhalisia ulioigwa (Virtual Reality au VR).
Badala ya kutumia kompyuta, watu katika metaverse watatumia headset kuingia ulimwengu usio halisi na kuunganishwa katika mazingira yote ya kidijitali.
Inatumainiwa kwamba ulimwengu usio halisi wa VR huenda ukatumika kwa chochote kuanzia kufanya kazi, kucheza michezo pamoja na kujiunga na matamasha hadi kuwasiliana na marafiki na familia. Hata shirika la Facebook limeshabadilisha jina lake la kampuni na kujiita Meta ikiwa ni mpango wake wa kujiimarisha kuelekea katika ulimwengu mpya wa kidijitali.

Mmimiliki wa Facebook Mark Zuckerberg alitangaza jina hilo jipya wakati alipokua akizindua mipango ya kujenga "metaverse" - ulimwengu wa mtandao ambapo watu wanaweza kushiriki katika michezo, kufanya kazi, kuwasiliana katika mazingira yaliyoigwa na yasio na uhalisi kwa kutumia vitoa sauti vinavyovaliwa kichwani au headset.
Kwa kuzingatia teknolojia hii mpya ibuka, kuna haja ya kuwa na mitandao yenye kutoa huduma kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu. Ni kwa msingi huo ndio shirika la IBF NET likazindua metaverse ya Kiislamu kuwahudumia Waslamu zaidi ya bilioni mbili kote duniani. Inatazamiwa kuwa mashirika mengine ya Kiislamu katika uga wa teknolojia yataiga mfano huo na kutoa huduma hii muhimu hasa kwa vijana ili wasipotoshwe na mitando mingine isiyozingatia maadili na mafundisho ya kidini.
Kwa mujibu wa Mohammad Alim, Mkurugenzi wa IBF NET, mradi wa metaverse wa shirika hilo unalenga kufungua kituo cha masomo ambapo washiriki wataweza kusoma na kubadilishana mawazo ya kieleimu popote pale na wakati wowote ule na pili ni kufungua soko la kuuza na kununua bidhaa na yote hayo yatafanyika kwa kuzingatia maadili ya Kiislamu.
Aidha anasema wanalenga kufafanua namna teknolojia ya metaverse ilivyo na manufaa kwa jamii za Waislamu na ni kwa msingi huo wanasisitiza kuwa lazima maadili ya Kiislamu yazingatiwe.
Na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani limeripoti kuzuka ugonjwa wa Monkeypox au ndui ya nyani katika maeneo mbali mbali duniani.
Kwa kawaida visa vya ugonjwa huu unaoshabihiana na ndui huripotiwa kwa watu wenye uhusiano na eneo la Afrika ya Kati na Magharibi lakini nchi kadhaa za Ulaya na Amerika Kaskazini zimeripoti visa kwa watu ambao hawakusafiri hivi karibuni barani Afrika.
Ugonjwa huo ambao unasababishwa na virusi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kwa nadra hutokea katika jamii zilizopo karibu na misitu huko Afrika ya kati na Magharibi ambapo kuna hifadhi za Wanyama hata hivyo dalili za wagonjwa waliogundulika barani Ulaya zinafanana na zile zilizoripotiwa siku za karibuni katika nchi za Australia, Canada na Marekani.

Akitaja sababu za kuwepo kwa ugonjwa huo, mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Dkt. Hans Henri P. Kluge ameeleza kuwa ingawa idadi ya kesi za wagonjwa barani Ulaya bado ni ndogo na ingawa hakuna uhusiano wa watu kusafiri kutoka kwenye maeneo yanayojulikana kuwepo kwa ugonjwa huo lakini idadi inaweza kuongezeka kwa kuwa matukio mengi ya wagonjwa wa Monkeypox yamegunduliwa katika kliniki maalumu za magonjwa ya zinaa.
WHO imeeleza kwamba inaendelea kufanya kazi na nchi ambazo ugonjwa huo umeibuka ili kuweza kupata taarifa zaidi na kusaidia katika ugunduzi wa kesi na matukio mengine ingawa mpaka sasa haijulikani wazi kuna kiwango gani cha maambukizi katika jamii lakini kuna uwezekano kwamba kesi zaidi zitatambuliwa katika siku zijazo.
Ugonjwa wa Monkeypox huambukizwa kutokana na virusi na unaambukizwa wakati wa kugusana baina ya watu, (mgusano huo hutokea iwapo mtu mmoja atakuwa na vidonda kwenye ngozi, kuvuta hewa yenye matone ya mtu aliye na ugonjwa huo au maji maji ya mwilini) pia ugonjwa huo unaambukizwa kupitia kujamiiana au kwa kugusana na nyenzo zilizoambukizwa.
WHO imetoa wito kwa mtu yeyote ambaye ana wasiwasi kuhusu kuwa na vipele visivyo vya kawaida kwenda hospitali kupata ushauria wa daktari au mtoa huduma wa afya. Watu wanaoshukiwa kuwa na Monkeypox wanapaswa kuchunguzwa na kutengwa baada ya kudhihiri dalili za kwanza.