Sibtain (Imam Hassan na Hussein as) katika Qur'ani na Hadithi 2
Hassanain katika Aya inayosema: Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote.
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuriya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, na karibuni kusikiliza sehemu ya pili ya kipindi hiki kipya cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi. Ni wazi kuwa kitabu kitakatifu cha Qur'ani kimezungumzia mambo, visa na matukio mengi sana yakiwemno yale yanayomuhusu moja kwa moja Mtume Mtukufu (saw) na Watu wa Nyumba yake (as), uhusiano wa watu na Mtume, suna na mafundisho yake kwa masahaba zake na matukio yaliyojiri baina ya Mtukufu huyo (saw) na watu wa kawaida.
Mambo haya yote wapenzi wasikilizaji yamezungumziwa na Aya za Qur'ani Tukufu na kusisitizwa na Hadithi pamoja na maandiko ya kihistoria. Hivyo, inawezekanaje baada ya Qur'ani Tukufu kuyazungumzia mambo hayo yote iwe imepuuza na kufumbia macho uhusiano mkubwa wa Mtume (saw) na wapendwa wake wa karibu zaidi, ambao ni miongoni mwa viumbe bora na watukufu zaidi katika jamii ya mwanadamu?! Kwa mfano, itawezekanaje Imam Hassan na Hussein (as) ambao walikuwa wajukuu wake wapendwa zaidi na maua ya macho yake, wawe hawajazungumziwa katika Qur'ani wala uhusiano wake nao pamoja na sifa na nafasi yao katika maisha ya Mtume Mtukufu?!!
Ni wazi kuwa, nyinyi wasikilizaji wapenzi mtaafikiana nasi kwamba hili ni jambo lisilowezekana kabisa kiakili. Kwa mantiki hiyo, wafasiri mashuhuri wa Qur'ani Tukufu wanasisitiza kwamba kuna Aya nyingi sana ambazo ziliteremshwa na Mwenyezi Mungu zikiwakusudia Imam Hassan na Hussein (as) peke yao au wakiwa na Watu wengine wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (saw) ambao ni Amir al-Mu'mineen Ali (as), Fatwimatu az-Zahra (as) wakiongozwa na Mtume mwenyewe, al-Mustafa al-Ameen (saw).
********
Ama kuhusiana na maana ya Aya ya 37 ya Surat al-Baqarah ambayo inasema: Kisha Adam akapokea maneno kutoka kwa Mola wake, na Mola wake akapokea toba yake, wafasiri wa Qur'ani wametoa maoni mengi kuhusiana na makusudio ya maneno hayo aliyoyapokea Nabii Adam (as). Wanasema maneno hayo yalikuwa na umuhimu mkubwa kiasi cha Mwenyezi Mungu kuyafanya kuwa chanzo na sababu ya kuikubali toba ya Mtume wake huyo mwema na mteule (as). Baadhi yao wanasema kuwa maneno hayo yalikuwa dua inayosema:
لا إله إلا أنت ، عملت سوءا وظلمت نفسي ، فارحمني إنک أنت التواب الرحیم
Hakuna Mungu isipokuwa Wewe, nimetenda mabaya (dhambi/maovu) na kuidhulumu nafsi yangu. Hivyo nirehemu, hakika Wewe ni mwingi wa kusamehe Mwenye kurehemu.
Kwa mfano hivi ndivyo alivyosema al-Baihaqi katika kitabu cha Shuab (al-Imaan) na wafasiri wengineo. Ad-Dailami ambaye ni mmoja wa maulama mashuhuri wa Kisuni anasema katika kitabu chake cha Firdaus al-Akhbar kwamba Mwenyezi Mungu alimtuma Malaika Jibrail (as) kwa Nabii Adam (as) aseme maneno yafuatayo ili apate kumsamehe:
اللهم إني أسألک بحق محمد وآل محمد ، سبحانک لا إله إلا أنت ، عملت سوءا ، وظلمت نفسي ، فتب علي إنک أنت التواب الرحیم
Allahumma! Hakika mimi ninakuomba kwa utukufu wa Muhammad na Aali za Muhammad, umetukuka, hakuna Mungu isipokuwa Wewe, nimetenda mabaya (dhambi/maovo) na kuidhulumu nafsi yangu. Hivyo nirehemu, hakika Wewe ni mwingi wa kusamehe Mwenye kurehemu.
Na hili ndilo jambo analosisitiza Ibn al-Maghazili as-Shafi' katika kitabu chake cha Manaqib bin Abi Talib ambapo anasema kuwa Said bin Jubair alisema kwamba Abdallah bin Abbas alisema: 'Mtume Mtukufu (saw) aliulizwa juu ya maneno ambayo Adam aliyapokea kutokwa kwa Mola wake naye akawa amesamehewa makossa aliyofanya, akasema: Alimuomba kwa utukufu na Baraka za Muhammad, Ali, Fatwimah, al-Hassan na al-Hussein amsamehe, naye (Allah) akamsamehe.'
Hadithi hiyo pia imenukuliwa na al-Hafidh as-Suyuti as-Shafi' katika Tafsiri yake ya ad-Durr al-Manthur na al-Qunduzi al-Hanafi katika kitabu chake cha Yanabiul Mawadda Lidhawi al-Qurba na al-Mutaqqi al-Hindiy katika kitabu cha Kanzul Ummal.
Ama katika upande wa maulama wa Kishia, as-Sheikh as-Swaduoq amanukuu hadithi hiyo katika kitabu cha Maani al-Akhbar iliyopokelewa na wapokezi wawili wa Hadithi, yaani Ibn Abbas na Abu Said al-Madaini, ambapo anasema kwamba Baba wa kizazi cha wanadamu, Adam (as) alimuomba toba Mwenyezi Mungu kwa utukufu wa Muhamad, Ali, Fatwimah, al-Hassan na al-Hussein (as). Anasema aliomba toba sahihi inayokubalika naye Mwenyezi Mungu akamsamehe. Ni vipi hangelisamehewa hali ya kuwa aliomba kwa kutumia majina ya viumbe bora na watukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu?!!
**********
Ndugu wasikilizaji, kuna Riwaya na Hadithi nyingi mno zinazozungumzia maneno ambayo aliyapokea Nabii Adam (as) kutoka kwa Mola wake na kupata kusamehewa makosa aliyofanya. Pamoja na hayo tutazungumzia Riwaya mbili tu hapa moja ikiwa ni ile iliyonukuliwa na Sheikh al-Juwayni as-Shafi' katika kitabu chake mashuhuri cha Faraid as-Simtain kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) kwamba alisema: Mwenyezi Mungu alipomuumba Adam, Baba wa Wanadamu, na kumpulizia roho yake, Adam alitazama upande wa kulia wa Arshi (ya Mwenyezi Mungu). Aliona huko mizuka (pepo) wa nuru ambao walikuwa wamesujudu na kurukuu. Adam akamuuliza Mwenyezi Mungu: Ewe Mwenyezi Mungu! Je, uliwahi kuumba kabla yangu kiumbe yeyote kutokana na udongo? Mwenyezi Mungu akajibu: La. Adam Akasema: Je, Mizuka hawa watano walio na umbo na dhahiri kama yangu ni nani? Mwenyezi Mungu akajibu: Hawa ni watano katika watoto wako ambao kama wasingekuwa wao, basi nisingekuumba wewe. Nimetoa majina ya watano hawa kutokana na majina yangu matano. Kama wasingekuwa ni watano hawa, nisingeumba Pepo na Jahannam, Arshi na Kiti cha Enzi, mbingu na ardhi, Malaika na Wanadamu wala Majini. Mimi Ni Mahmoud na huyu hapa ni Muhammad. Mimi ni Aali (Aliye juu zaidi) na huyu hapa ni Ali. Mimi ni Fatwir (Muumbaji) na huyu hapa ni Fatwimah. Mimi ni Ihsani na huyu hapa ni Hassan na Mimi ni Muhsin na huyu hapa ni Hussein. Ninaapa kwa nafsi yangu kwamba mtu yeyote aliye na chembe ndogo tu ya mapenzi kwa watu hawa moyoni mwake, nitamuingiza Peponi. Ninaapa kwa nafsi yangu, iwapo mtu atakuwa na chembe ndogu tu ya uadui na chuki, kiasi cha haradali, dhidi yao, nitamuingiza motoni na wala sitajali. Ewe Adam! Hawa ni waja wangu wateule, ambapo wongofu na kuhiliki kutoka kwa Mwenyezi Mungu kunahusiana nao. Iwapo una haja yoyote kutoka kwetu tawasali nao (omba kupitia kwao).' Mtume (saw) akaendelea kusema: 'Sisi ni safina (meli) ya wongofu ambapo iwapo mtu ataipanda atanusurika na yeyote anayeenda kinyume atahiliki. Kama mtu ana haja yoyote kutoka kwa Mwenyezi Mungu na amuombe kutupitia sisi Ahlul Bait' (Faraid as-Simtain, Juwayni, juzuu ya 1 ukurasa wa 36).
Riwaya ya pili imenukuliwa na Sheikh Tuosi katika kitabu cha at-Tibyaan, al-Mash'hadi katika kitabu cha Kanzu ad-Daqaiq na Fakhr ar-Razi katika Tafsiri yake ya al-Kabir ambapo wanasema kuwa maneno aliyopokezwa Adam (as) na kumdhaminia toba ni haya yafuatayo:
اللهم لا إله إلا أنت سبحانک وبحمدک رب إني ظلمت نفسي فاغفر لي إنک خیر الغافرین . اللهم لا إله إلا أنت سبحانک وبحمدک رب إني ظلمت نفسي فارحمني إنک أنت خیر الراحمین . اللهم لا إله إلا أنت سبحانک وبحمدک رب إني ظلمت نفسي فتب علي إنک أنت التواب الرحیم اللهم بجاه محمد وآله الطیبین ، بجاه محمد وعلي و فاطمة والحسن والحسین ، والطیبین من آلهم ، لما تفضلت علي بقبول توبتي ، ووغفران زلتي ، وإعادتي من کرامتک إلی مرتبتي
Allahumma! Hakuna Mungu isipokuwa Wewe, umetukuka na sifa zote njema ni zako. Mola wangu! Hakika nimedhulumu nafsi yangu, hivyo nisamehe kwa kuwa Wewe ni mbora wa wanaosamehe. Allahumma! Hakuna Mungu isipokuwa Wewe, umetukuka na sifa zote njema ni zako, Mola wangu! Hakika mimi nimedhulumu nafsi yangu, hivyo nirehemu kwa kuwa Wewe ni mbora wa wanaorehemu. Allahumma! Hakuna Mungu isipokuwa Wewe, umetukuka na sifa zote njema ni zako. Mola Wangu! Mimi nimeidhulum nafsi yangu, hivyo nikubalie toba yangu kwa kuwa Wewe ni mwingi wa kukubali toba, Mrehemevu. Allahumma! Kwa Baraka na utukufu wa Muhammad na Aali zake wema, kwa utukufu wa Muhammad na Ali na Fatwimah na al-Hassan na al-Hussein na wengine wote wema katika kizazi chao, nifanyie wema na unikubalia toba yangu, nisamehe makosa yangu na unirejeshee karama (neema/ukarimu) yako.'
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa sehemu ya pili ya kipindi hiki kipya cha as-Sibtain, ambao ni Imam Hassan na Hussein (as) wajukuu wapendwa wa Mtume Mtukufu (saw), ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena katika kipindi kijacho, tunakuageni nyote wapendwa wasikilizaji kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.